DK. SLAA ADAI HOJA YA MBATIA ILIKUWA NA MAJIBU YOTE
SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume maalumu ya kuchunguza matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni, wanasiasa na wasomi wamempinga wakidai ni kupoteza muda na fedha kwa kuwa hoja binafsi ya Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia ilikuwa na majibu.
Kwa nyakati tofauti katika mahojiano na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana walihoji ni tume na kamati ngapi zimeundwa na kutolewa taarifa kuhusu matatizo ya elimu katika miaka 15 iliyopita na hatua zipi zimechukuliwa kurekebisha dosari zilizoonekana.
Dk. Slaa alishangazwa na hatua hiyo ya Waziri Mkuu kuunda tume kwa ajili ya kufuatilia kufeli kwa wanafunzi, akisema ni juzi tu Bunge limemaliza kikao chake Dodoma na kuitupilia mbali hoja binafsi ya Mbatia.
Alisema hoja binafsi ya Mbatia ilikuwa na nia ya kupitisha azimio la Bunge kuunda kamati teule ya kuchunguza tatizo la udhaifu katika sekta ya elimu, lakini kwa ushabiki wa wabunge wa CCM akiwemo Waziri Mkuu, ilikataliwa.
“Wiki mbili hazijapita wameumbuliwa na matokeo, na sasa Waziri Mkuu anaunda tume. Huku ni kuwadanganya Watanzania. Pinda ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni na kiranja wa mawaziri wote, Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa alilidanganya Bunge na taifa kuhusiana na swala la mitaala, ambalo lina uhusiano mkubwa na ubora wa elimu.
“Waziri Mkuu alikuwepo, hakuchukua hatua wala ya kumsahihisha Kawambwa au kusema ukweli na kuchukua hatua kwa waziri huyo kwa jambo lililotokea mbele ya macho na masikio yake,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa hilo, Pinda hastahili kuchukua hatua ya kuunda tume, bali kujiuzulu kwa kushindwa kuwajibika na pia kushiriki kulidanganya taifa.
Dk. Slaa alisema kuwa Serikali ya CCM imeunda tume na kamati nyingi, lakini taarifa zilizotolewa hazijawahi kufanyiwa kazi, na kwamba kama hali ndiyo hiyo, hata tume hii inayoundwa hakuna jipya.
“Suala la elimu halihitaji kuundiwa tume wala kamati ya uchunguzi. Serikali ya Rais Kikwete na Pinda kweli hawajui matatizo yanayofanya elimu yetu kudorora mpaka waunde tume?” Alihoji Dk. Slaa na kuongeza kuwa Serikali ya CCM haijui kwamba bajeti ya elimu ni ndogo ikilinganishwa na zile za majirani zetu katika sekta hiyo.
Dk. Slaa alisema kuwa ni usanii na kuendeleza ufisadi kwani tume itaendelea kuangamiza fedha kwa vile serikali haijaonesha utashi wa kisiasa kuboresha elimu ya watoto ya Watanzania.
Alisema kinachotakiwa sasa ni kuunganisha nguvu na kukataa usanii wowote katika masuala ya msingi. Kwamba wale wote waliodanganya taifa wawajibike kwa kujiuzulu au wawajibishwe.
Aliongeza kuwa, watoto waliofeli waandaliwe utaratibu wa kunusuru maisha yao badala ya kuunda tume wakati maisha yao ya baadaye yakivurugika.
Naye Dk. Bana alimbeza Pinda kwa hatua hiyo ya kuunda tume kwa masuala ya mtihani, akisema tatizo la kufeli kwa wanafunzi halihitaji tume kwani kasoro ziko wazi.
Alisema kuwa matatizo ya walimu yanajulikana, huku serikali ikijidanganya kutengeneza sera ya elimu kinyemela bila kushirikisha wataalamu.
“Mtihani ni sehemu ndogo sana, lakini siasa za zimamoto ndizo zimetufikisha hapa. Tujue kuwa siasa za zimamoto hazisaidii Watanzania, tunapoteza muda na fedha zetu, lakini mfumo wa elimu unapaswa uangaliwe kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.
“Utaratibu huu wa kuanza kuunda tume kila darasa likifeli zitaundwa ngapi?” alisema na kuongeza kwamba tatizo la elimu ni la kitaaluma, si siasa.
Alisema kuwa wanangoja kuona wale watakaoteuliwa kutoka katika chuo hicho kuingia kwenye tume ya Pinda kama watakuwa tayari kwenda kuungana na suala hili ambalo halizingatii utaalamu, badala yake linatibu ugonjwa na kukwepa dalili zake.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment