Sunday, February 3, 2013

Mnyika ataka nakala mikataba ya gesi




Mbunge wa Ubungo (Chadema) , John Mnyika, amewasilisha rasmi kwenye ofisi ya bunge barua ya kutaka kupatiwa nakala za mikataba ya gesi ili kubainisha taratibu za uwekezaji katika miradi hiyo.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Mnyika alisema barua hiyo ameiwasilisha rasmi kwa Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah.
Alisema anachukua hatua hiyo kwani hakuridhishwa na maelezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni Alhamisi wiki hii.
Mnyika alisema Pinda akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe lililohoji kuhusu kuwekwa wazi mikataba ya gesi alieleza kuwa mbunge atapatiwa mikataba ya gesi kupitia njia za kibunge. Alisema kufuatia suala hilo aliamua kuchukua hatua kwa kutumia sheria ya kinga, haki na madaraka ya bunge kutaka kupatiwa mikataba ili kujiridhisha kwani anahofia kuna maelezo aliyoyatoa Waziri Mkuu ambayo hayana ukweli kulingana na mikataba hiyo.
Alikitaja kifungu cha 10 cha sheria kuwa kinaeleza kuwa mbunge akitaka nyaraka ana haki ya kupatiwa bila pingamizi.
Mnyika alisema Julai 27 mwaka jana wakiwa bungeni alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kutolea maelezo juu ya mikataba ambapo hakuweza kueleza ukweli wa jambo hilo.
Mnyika alisema maelezo ya Pinda aliyoyatoa hivi karibuni bungeni pamoja na ya Profesa Muhongo hayaridhishi hali iliyomsukuma kuwasilisha barua hiyo kutaka kuona kile kilichopo katika mikataba ya gesi ikiwamo wa Mtwara.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment