Friday, February 8, 2013

Mitaala ya Elimu: Kamati yasema ni halali; Mbatia asisistiza ni batili

Bunge limethibitisha kwamba Mitaala ya Elimu iliyowasilishwa na Serikali Bungeni ni halali wala haijachakachuliwa.
Mitaala hiyo iliwasilishwa bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa baada ya kuombwa na Bunge wiki iliyopita kuwaisilisha ili kuhakikisha kwamba serikali inayo.

Akitangaza taarifa ya Kamati iliyoundwa na Bunge kuchunguza uhalisi wa mitaala hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema, kamati imepitia na kubaini ni halali na hivyo watawagawia wabunge.

Spika Makinda alisema, mitaala hiyo iliyowasilishwa na Serikali kama ilivyoomba na Bunge kufanya hivyo, ilipitiwa na kamati ya wabunge sita chini ya Mwenyekiti, Margareth Mshashu (CCM) na kubaini haijachakachuliwa.

Hata hivyo, wakati wa majadiliano chini ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu Azzan, kutokana na Bunge kuthibitisha mitaala hiyo kuwa inafaa, Mbunge wa Namanyere, Ali Keisy (CCM) aliomba mwongozo wa Spika kumtaka Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ajiuluzu kama alivyoahidi. 

Awali Januari 30, mwaka huu, Mbatia aliwasilisha hoja binafsi akilalamika kwamba Serikali haina mitaala akaomba apatiwe na serikali ikaahidi kuwasilisha Februari 6, na ilifanya hivyo.

Mbatia mwenyewe amesema hatajiuzulu kwa kuwa mitaala iliyowasilishwa bungeni ni feki.  Aidha, amesema badala ya kuendeleza vuta-nivute, Wizara pamoja na yeye wakubali kujadili Bungeni mitaala hiyo aliyosisitiza si halali, ili waboreshe sekta ya elimu.

Msingi wa hoja za Mbatia ni kwamba mitaala hiyo si rasmi na imekosa namba kutoka International Standard Book Number (ISBN), haikusainiwa na mtu yeyote. Alisema  Kamishna wa Elimu alipaswa awe ameisaini.

---
via Lukwangule blog



KUTOKA JF
HakiElimu: Tanzania Haijawa na Mtaala wa Elimu Kwa Miaka Mingi

Sakata la ama Tanzania ina mitaala ya Elimu ama la limezidi kuwa songombingo.Jana ITV katika taarifa yake ya habari ya saa mbili usiku Februari 6, 2013 waliwaonesha maofisa wa taasisi ya HakiElimu wakisema kwa utafiti wao walioufanya wamegundua kwamba tanzania haijawa na mitaala ya elimu kwa miaka mingi.

HakiElimu wamesema katika baadhi ya wilaya na shule walizozipitia hawakuona mitaala hiyo; zaidi ya nyaraka na maagizo ya nini kifanyike. Baadhi ya walimu wa shule mbali mbali walioulizwa kuhusu mitaala walijibu kuwa hawajawahi iona.

Je, sasa ukweli ni upi? Jambo moja liko wazi sana. Shule za msingi zinazofundisha kwa kiingereza masomo yao zimekuwa zikitumia vitabu vya kutoka Kenya. Mfano, wa vitabu hivyo ni vile vya hisabati. Humo utaona picha na michoro ya fedha na sarafu za Kenya. Katika somo la jiografia, historia na uraia hali ni tete.

Aidha, walimu wamekuwa wakiandaa ''Maandalio ya Somo'' ( Lesson Plan) kwa kufuata sura za vitabu hivyo. Hapa watoto wanaandaliwa kuwa raia na watumishi wa nchi jirani. Ieleweke kwamba kupitia elimu mtoto anaandaliwa kuwa raia mwema, mzalendo, mtumishi, na mwendelezi wa taifa lake kwa miaka kadhaa atapofikia utu uzima. 

Mfano, mwingie ni kwamba kupitia masomo ya lugha na fasihi mwanafunzi anajazwa amali za jamii yake; anashehenezwa utamaduni wa taifa lake; anajengwa kuwa mzalendo mwelewa; anajifunza kutatua migogoro; anafundishwa na kukuzwa uwezo wa kujieleza, kujifafanua, kujipambanua, kujithamini, kuijua thamani yake halisi, kuona thamani ya utu wake na utu wa mwenzie, kuelewa haki zake; kwa jumla lugha na fasihi ni somo linalomfanya mwanafunzi aufikie utu wake kamili.

Hivyo, kwa mwendo huu, wa 'kukopi' na 'kupesti' mitaala, vitabu nk utazaa taifa lisilojijua. Vijana hawa hawatawaacha viongozi wa leo salama hata(viongozi hawa) watakapokuwa makaburini.

1 comment:

  1. Alafu hao(MAGAMBA) ndio walitoa ahadi za kishindo tena, Rais wa nchi alisema mbele ya hadhara kule Igunga kuwa mwezi wa kwanza wanaajiri waalimu takribani elfu ishirini na sita, sasa mbona holaa au wameajiri kimya kimya? Na watoto wetu wanakosa elimu bora mashuleni waalimu hakuna... Kwanini lakini jamani wananchi wa hali ya chini tunaumizwa hivi? CHDEMA, simamieni hili.

    ReplyDelete