Sunday, February 24, 2013

Matokeo kidato cha nne yaiweka CCM njia panda


YASHINDWA KULAANI WANAFUNZI WENGI KUFELI
MATOKEO mapya ya kidato cha nne, yamekiweka Chama Cha Mapinduzi (CCM) njia panda, kiasi cha kushindwa kutoa kauli ya kuungana na wananchi wengine wanaohoji na kulaani kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
Habari kutoka ndani ya chama hicho tawala, zinasema kuwa kumekuwa na mvutano mkubwa miongoni mwa viongozi wa juu wa chama hicho na serikali, wa kuweka wazi msimamo wa chama hicho hadharani.
Ugumu wa kuingia kwenye mjadala huo unaotikisa taifa kwa sasa, unatokana na ukweli kwamba hoja kuhusu udhaifu katika mfumo wa elimu iliwasilishwa bungeni na James Mbatia (Mbunge wa Kuteuliwa na Rais), lakini ilizimwa kibabe na Spika wa Bunge, Anne Makinda na naibu wake Job Ndugai, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na wabunge wote wa CCM.
Duru za siasa kutoka ndani ya chama hicho tawala, zinasema kuwa CCM iko njia panda kuzungumzia hilo kwani wabunge wake walifanya makosa kuzima hoja ya Mbatia kishabiki na serikali kupitia Waziri wake, Dk. Shukuru Kawambwa na Mwanasheria Mkuu (AG), nayo ilikuja na majibu ya kupingana na hoja hiyo.
“Mungu si Athuman, leo Mungu katuumbua. Katika mazingira kama haya, CCM ukiungana kulaani wakati wabunge na serikali ilizima hoja hiyo, nani atakuelewa? Hapa Bunge limetuweka njia panda,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya CCM.
Katika mkutano wa Bunge uliopita, Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, aliwasilisha hoja binafsi akitaka Bunge liunde kamati kuchunguza mfumo wa elimu na kuja na mapendekezo ya kuwa na mfumo mzuri zaidi wa elimu.
Katika hoja hiyo, Mbatia aliorodhesha udhaifu mkubwa katika sekta ya elimu na kuongeza kuwa, Tanzania haina mitaala ya elimu na kama atapewa nakala ya mitaala hiyo, atajiuzulu ubunge wake.
Baada ya siku saba, Waziri Kawambwa alikuja na nakala ya mitaala ambayo kwa mujibu wa Mbatia, alidai kuwa ni feki kwani ilikuwa na kasoro nyingi, ikiwemo kutokuwa na saini ya Kamishna wa Elimu nchini.
Hata hivyo, Bunge lilizima hoja hiyo kibabe na wabunge wa kambi ya upinzani kuamua kutoka nje ya ukumbi.
Habari zaidi zinasema kuwa CCM inatamani kuona Waziri Kawambwa na watendaji wengine wa wizara hiyo, wanawajibika ili kuinusuru serikali na chama.
Kwamba tayari Waziri Kawambwa na watendaji wake, wamekuwa wakipokea ushauri wa aina mbalimbali, ukiwemo wa kuwataka wajiuzulu ili kujenga heshima yao, ya chama na serikali.
“Tunajua msimamo wa waziri na watendaji wake kwamba hawana sababu ya kujiuzulu kwani wao sio chanzo cha wanafunzi kufeli, lakini hapa tunaongelea uwajibikaji. Jambo limetokea mikononi mwako, unawajibika kujenga heshima yako, ya chama na serikali iliyokupa dhamana,” alisema mtoa habari wetu.
Mbali ya kuwataka waziri na watendaji wake wawajibike, baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao hawezi kuzungumzia maoni hayo hadharani, wanaunga mkono hoja ya kumtaka rais aunde tume kuchunguza sababu za wanafunzi wa kidato cha nne kufeli kwa kiwango cha kutisha mwaka huu, lakini pia kuja na mapendekezo ya mfumo bora wa elimu.
Ushauri wa kutaka rais aunde tume, juzi ulitolewa pia na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Lowassa alisema tume hiyo itakuja na majibu ya maswali yote yanayoulizwa na Watanzania, hasa baada ya matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne, kuwa mabaya.
Baadhi ya mambo yanayolalamikiwa katika mfumo wa sasa, ni pamoja na suala la mitaala ambapo kila waziri anayekuja, huja na mitaala na mfumo wake kwa kadiri anavyoona inafaa.
Jingine ni matumizi ya vitabu vya kujisomea kubadilika kila mwaka kiasi kwamba kitabu cha mwaka huu cha somo moja, hakiwezi kutumika tena mwakani kwa darasa lilelile, jambo ambalo limekuwa likipingwa mara nyingi na wadau wa elimu.
Mbali na masuala ya kuboresha miundombinu, na mazingira bora ya walimu kufanya kazi, pia baadhi ya wadau wanataka utaratibu wa kuwapata walimu kwa kuchukua wanafunzi waliopata daraja la nne kwenda vyuo vya ualimu, ubadilishwe.
Jumla ya wanafunzi wa kidato cha nne 240,000 wamepata ziro, huku idadi ya waliopata daraja la kwanza ikishuka kwa kiwango cha kutisha.
Pinda aunda tume ya uchunguzi
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameunda tume maalumu itakayofanya uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo yalitangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Kawambwa.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa Jumatatu wiki hii, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne Oktoba, 2012 walifeli.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo amesema tume hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki ijayo, inajumuisha wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (TAMONGSCO), taasisi za Dini zinazotoa huduma ya elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na asasi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazoshughulikia masuala ya elimu.
Wadau wengine watatoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).
Alisema serikali inawaomba wadau wa elimu, wazazi, walezi na wananchi wote kwa ujumla watoe ushirikiano kwa tume ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment