Waomba hukumu ya Mahakama ya Rufaa ipitiwe upya
Makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopinga ubunge wa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na kufanikiwa kumvua ubunge kabla ya Mahakama ya Rufaa kumrejesha wadhifa wake, wamewasilisha maombi ya kutaka hukumu ya mahakama hiyo ipitiwe upya.
Makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopinga ubunge wa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na kufanikiwa kumvua ubunge kabla ya Mahakama ya Rufaa kumrejesha wadhifa wake, wamewasilisha maombi ya kutaka hukumu ya mahakama hiyo ipitiwe upya.
Kwa mujibu wa taarifa za kimahakama, makada hao waliwasilisha maombi yao Februari 13, mwaka huu chini ya hati ya dharura wakitaka yasikilizwe haraka.
Desemba 21, mwaka jana Mahakama ya Rufaa ilimrejesha tena Lema bungeni baada ya kukubali rufaa yake dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge wake.
Makada hao waliolalamikia ushindi wa Lema wakiwa ni wapigakura wa Jimbo la Arusha Mjini, wanadai kuwa na sababu sita za kutaka mahakama hiyo ipitie uamuzi wake kwa madai kuwa kuna maeneo ambayo hayakuamuliwa vizuri. Jana NIPASHE ilizungumza na Wakili wa Lema, Method Kimomogoro, ambaye alithibitisha kuwa na taarifa za maombi hayo na kuahidi kutoa ufafanuzi baadaye.
Naye wakili wa wanachama wa CCM, Alute Mughway, jana alithibitisha kuwa wateja wake wamewasilisha maombi hayo Mahakama ya Rufaa.
Wanachama hao wa CCM, ambao ni Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, walifungua kesi dhidi ya Lema katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kupinga ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Walikuwa wakidai kuwa katika kampeni zake, Lema alikuwa akitumia lugha za matusi, kejeli na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Buriani.
Kufuatia kesi hiyo, Lema alivuliwa ubunge na mahakama hiyo, Aprili 5, mwaka huu, katika hukumu iliyotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo. Jaji Rwakibarila aliisikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Aloyce Mujulizi aliyekuwa amepangiwa kuisikiliza kesi hiyo kujitoa kufuatia ombi la Lema kuwa hakuwa na imani naye.
Hata hivyo, baadaye mwishoni mwa mwaka jana, Lema kupitia mawakili wake, Kimomogoro na Tundu Lissu, alikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyomvua ubunge wake.
Hukumu ya kumrejeshea ubunge Lema ilitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Nathalia Kimaro. Wengine ni Salum Massati na Bernard Luanda.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment