MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) ameiomba Serikali kumruhusu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa thamani ya miradi ya maji katika Jiji la Dar es Salaam, inayoanzia maeneo ya Bagamoyo uliogharimu Sh bilioni 240.
Akizungumza Dar es Salaam jana, alisema suluhisho la mvutano wa maji ni kuruhusu CAG kufanya ukaguzi wake kwa kulinganisha ufanisi wa Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Miundombinu ya Majisafi na Majitaka (DWSSP) unaoanzia Bagamoyo, Kibaha hadi Dar es Salaam kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi uliofanywa na Kampuni ya Howard Humphreys.
“Nasema CAG afanye ukaguzi kwa sababu mradi wa DWSSP ulitumia dola milioni 164.6 za Marekani, sawa na shilingi bilioni 240 za Tanzania na hadi sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya Wachina hautoi maji.
“Pia kumekuwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi ambapo hali hii ni kati ya matatizo yanayokera wananchi wa Dar es Salaam, kwa kuwa na mabomba yasiyotoa maji kwa muda mrefu hata kwa mgawo.
“Ni vema Serikali ikawaeleze wananchi sababu ya mabomba hayo kutokutoa maji hadi hivi sasa na lini mabomba hayo yataanza kutoa maji katika maeneo ambayo maji hayatoki na hatua gani zimechukuliwa kwa waliotekeleza mradi huo bila kuzingatia maandalizi ya msingi.
“Ni muhimu hatua zikachukuliwa kwa wahusika kwa kuwa kitendo cha mabomba hayo kukaa muda mrefu bila kutoa maji inafanya miundombinu hiyo kuanza kuharibika au kuharibiwa ambayo ni hasara kwa Taifa, pamoja na fedha zilizotumika kuweka mabomba hayo kupotea,” alisema Mnyika.
Aliomba Serikali kueleza matokeo ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kufanya ukaguzi wa kiufanisi wa miradi ya maghati na visima vya maji takriban 200 ambavyo vilichimbwa na Serikali na kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO).
Alisema anaiomba Serikali kufanya hivyo kwa sababu hali halisi pamoja na tafiti mbalimbali zinathibitisha kuwa matatizo ya kuwa na mabomba yasiyotoa maji hayapo tu katika mabomba waliyofungiwa wananchi, bali pia yapo katika visima na vioski, maghati ya jumuiya.

No comments:
Post a Comment