Tuesday, February 5, 2013

HOJA BINAFSI JUU YA MWENENDO WA BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA UNAVYOATHIRI ELIMU YA TANZANIA

HOJA BINAFSI JUU YA MWENENDO WA BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA UNAVYOATHIRI ELIMU YA TANZANIA

[Chini ya Kanuni ya 54(1), (2) na (3)]

Utangulizi

Mheshimiwa Spika, katika dunia ya leo, ili kila mtu aweze kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu. Elimu ndiyo inayomwezesha mtu kujitambua na kujimiliki yeye mwenyewe kwanza, pia kuzikabili changamoto zinazomsonga, kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake. Ndani ya utandawazi, elimu isiyotosheleza, tafsiri yake ni umaskini zaidi; wakati elimu zaidi tafsiri yake ni maisha bora zaidi.
-
Mheshimiwa Spika, Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika Kusini amewahi kusisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya jamii, kwa kusema kuwa;
“........elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu. Ni kupitia elimu ndipo binti wa mkulima mdogo anaweza kuwa daktari bingwa, kwamba mtoto wa kibarua wa mgodini anakuwa Mkuu wa Mgodi, na mtoto wa kibarua wa mashambani anakuwa Rais wa taifa kubwa”. (Mandela, 1991).
“Elimu inakuwa na maana sana kama malengo yake yalikuwa ni kuhakikisha kuwa kipindi wanafunzi wanamaliza shule, kila mvulana na msichana anapaswa kufahamu kwa kiwango gani hajui, na hivyo kuhamasika kujenga matamanio ya kutaka kufahamu zaidi muda wote maishani mwake” (William Haley, 1901-1987).
-
Mheshimiwa Spika, ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo ni lazima iwe elimu bora-ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii. Elimu ni ukombozi iwapo italenga kumpatia mtu uwezo wa kupambana na changamato zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla. Elimu inamjenga mtu kuwa raia makini na mzalishaji ndani ya nchi yake (Zombwe, 2007)
-
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa michakato ya kufundisha na kujifunza katika kuboresha elimu, bado elimu yetu inapimwa na mtihani ambao hutumika kama mizania ya kupima kufuzu ngazi fulani ya elimu. Kutokana na ukweli huo, ufaulu katika mtihani umekuwa ndio kigezo muhimu cha kuvuka ngazi fulani ya elimu kwenda nyingine na au kupata ajira rasmi. Kwa kifupi, mitihani katika mazingira yetu, ndiyo inayoamua mustakabali wa kiwango cha -maisha atakayoishi mwananchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa mitihani katika kuamua mustakabali wa maisha ya mwananchi, maelezo ya hoja hii yanalenga kuonesha changamoto mbalimbali zinazolikabili Baraza la Mitihani la Taifa, na hatimaye kutoa hoja ya kuliomba Bunge liazimie kuiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za jamii kufanya uchunguzi maalumu kwa Baraza la Mitihani la Taifa kuhusu utendaji wake wa kazi na kutoa taarifa Bungeni ili Bunge liweze kufanya maamuzi stahiki kwa madhumuni kutoa mwongozo wa namna bora ya kushughulikia masuala ya mitihani ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya watu.
-
Majukumu na Wajibu wa Baraza la Mitihani la Taifa
Mheshimiwa Spika, Baraza la Mitihani la Taifa ni taasisi iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge namba 21 ya mwaka 1973. Taasisi hii, pamoja na mambo mengine ina mamlaka ya kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani yote nchini Tanzania isipokuwa kwa vyuo vikuu.
-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Baraza la Mitihani la Taifa ni chombo muhimu sana katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya kielimu au ya kimaisha ya kijana wa kitanzania aliyehitimu ngazi fulani ya elimu. Hii ni kwa sababu walau kwa mazingira ya nchi yetu, kipimo cha kwamba mtu amefuzu ngazi fulani ya elimu kinatokana na alama ya ufaulu wa mtihani mtu huyo aliyopata katika kuhitimu ngazi hiyo ya elimu.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa mitihani katika kuamua mustakabali wa kiwango cha -maisha atakayoishi mtu kutokana na elimu aliyoipata, ni dhahiri kwamba mitihani inatakiwa itungwe kwa umakini mkubwa kufuatana na mitaala ya elimu inayotumika kwa wakati huo, ilindwe na isimamiwe kwa uangalifu mkubwa ili ikidhi mahitaji yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uzito wa jambo hili, hitilafu yoyote katika kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani hiyo, inamwathiri sana mtahiniwa mwenyewe na Taifa kwa jumla. Mtahiniwa anaathirika hasa pale atakapofutiwa mtihani kwa makosa ambayo hakuyafanya yeye, na vilevile taifa linaathirika sana hasa pale udanganyifu katika mitihani unapofanyika na hivyo kuwapata wataalamu bandia (wasio na sifa) na hivyo kuendelea kulisababishia taifa hasara kubwa. Aidha taifa linapata hasara pale mitihani inapofutwa kutokana na udanganyifu na hivyo kuingia gharama kubwa katika kurudia mitihani hiyo.

Mheshimiwa Spika, madhara ya kutosimamia na kudhibiti mitihani ipasavyo yanawaathiri vilevile wazazi au walezi wa wanafunzi. Hii ni kwa sababu adhabu za kufuta matokeo kutokana na kuvuja kwa mitihani au udanganyifu katika mitihani zinawasababishia wazazi/walezi msongo wa mawazo juu ya mustakabali wa maisha ya watoto wao. Maumivu wanayoyapata wazazi na walezi yanatokana hasa na gharama kubwa walizotumia kuwasomesha watoto wao ambao ghafla wanafutiwa matokeo yao kwa sababu ya udhaifu wa watendaji wa Baraza la Mitihani.


Changamoto zinazolikabili Baraza la Mitihani la Taifa-

1. Kuvuja kwa mitihani
Mheshimiwa Spika, tatizo la kuvuja kwa mitihani hapa nchini ni la muda mrefu. Madhara ya kuvuja kwa mitihani hapa chini hali kadhalika ni makubwa. Katika historia ya Tanzania, uvujaji mkubwa wa mitihani ulitokea -Novemba 1998 wakati wa mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya sekondari ya kawaida (kidato cha nne) na hivyo kusababisha mtihani huo kufutwa na kupangwa kufanyika tena Januari 1999. Inakadiriwa kwamba gharama zilizotumika kwa kurudia mtihani huo zilikuwa ni Shilingi 969,651,329/80 (sawa na Dola za Marekani 1,243,142.72), hii ikiwa ni tofauti na gharama za mwanzo. -
-
Mheshimiwa Spika, matatizo ya kuvuja kwa mitihani yamesababisha pia wanafunzi kufutiwa matokeo yao na hivyo kuwafanya waishi kwa hofu bila kujua mustakabali wa maisha yao. Kwa mfano kwa mwaka 2011 peke yake, jumla ya wanafunzi 9,736 -wa shule za msingi na wanafunzi 3,303 wa shule za sekondari walifutiwa matokeo yao ya mtihani wa Taifa kutokana na udanganyifu katika mitihani ambao kimsingi ulitokana na kuvuja kwa mitihani. Pamoja na Serikali kutoa msamaha kwa wanafunzi hao lakini taifa linakwenda kuingia katika gharama nyingine kubwa ya kwaandalia wanafunzi hao mtihani mwingine, gharama ambazo zingeweza kuepukika kama mitihani ingekuwa inasimamiwa kwa uaminifu.
-
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya kichocheo cha kuvuja kwa mitihani kinatokana na mfumo wetu wa elimu. Mfumo wa elimu tulionao unasisitiza zaidi ufaulu wa mtihani wa mwisho kuliko uwezo aliojengewa mwanafunzi wa kukabiliana na changamoto za maisha. Hiki kinaweza kuchangia tatizo hili kwa kiasi kikubwa kwani kutokana na hali hii, mwanafunzi analazimika kutumia mbinu zozote zile ili kuhakikisha kuwa anafaulu mtihani wake wa mwisho ambao ndio utakaoamua hatma ya maisha yake. Kwa kweli hili ni tatizo kubwa ambalo linatakiwa kufanyiwa tathmini na wadau wa elimu kwani linaathiri maendeleo ya elimu nchini. Kuna haja ya kuweka utaratibu wa kutathmini uwezo wa mwanafunzi kwa kipindi chote awapo shuleni badala ya kukazania mtihani wa mwisho tu. Kuna umuhimu wa walimu kuweka msisitizo wa kuelewa zaidi kuliko ufaulu peke yake. Hii ingewajengea wanafunzi ari ya kujitahidi kuelewa zaidi wawapo shuleni.
-
2. Ongezeko la Matukio ya Kughushi Vyeti vya Elimu Vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.
Mheshimiwa Spika, matukio ya kughushi vyeti vya elimu vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa ni dosari nyingine inayomomonyoa ubora wa elimu hapa nchini. Aidha tatizo la kughushi vyeti vyenye nembo ya Baraza la Mitahani la Taifa kunalipotezea Baraza hilo la Mitihani Sifa na Mamlaka ya kuendelea kutoa vyeti hivyo kwa kuwa limeshindwa kudhibiti mzunguko wa vyeti bandia.
-
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba matukio ya kuvuja kwa mitihani na kughushi vyeti vya elimu si tu yanasababisha watu kukosa imani na Baraza la Mitihani la Taifa, lakini pia yanashusha kiwango cha ubora wa elimu yetu na pia yanashusha hadhi ya mfumo wa elimu hapa nchini. Aidha, Serikali inapata hasara kwa kuingia katika gharama zisizo za lazima za kurudia mitihani, na kuwalipa wafanyakazi bandia wenye vyeti bandia wanaojipatia fedha za walipa kodi kwa njia ya udanganyifu.
-
Mheshimiwa Spika, matukio ya kughushi vyeti yamekuwa yakiongezeka jambo linaloashiria kuporomoka vibaya kwa ubora wa elimu ya Tanzania. Kati ya mwaka 1990 hadi 2001 kumeripotiwa matukio 583 ya kughushi vyeti vya elimu (Tazama Jedwali na.1)
-
Jedwali 1: Matukio ya Kughushi Vyeti vya Elimu Tangu 1990 hadi 2001-
-
MWAKA
MATUKIO YA KUGHUSHI VYETI
1990
25
1991
41
1992
45
1993
11
1994
26
1995
21
1996
34
1997
45
1998
149
1999
32
2000
95
2001
60
-
Chanzo: Hotuba ya Waziri wa Elimu 2002
-
3. Kushuka kwa Viwango vya Ufaulu
Mheshimiwa Spika, kushuka kwa viwango vya ufaulu ni miongoni mwa mambo yanayowapa wasiwasi wadau wakubwa wa elimu hasa wanafunzi wenyewe na wazazi/walezi na hivyo kutilia shaka mfumo mzima wa utendaji kazi wa Baraza la Mitihani la Taifa. -Pia kupungua kwa viwango vya ufaulu na badala yake kuongezeka kwa idadi ya wanaoshindwa mtihani kunaliweka Taifa katika hali ya hatari ya kutumbukia katika umasikini uliokithiri kwani idadi hii ya wanaoshindwa mtihani wengi wao watokosa fursa za ajira na hivyo kuwa tegemezi. Kwa mfano, katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne, mwaka 2011, ni asilimia 9 tu waliopata daraja la I – III na asilimia 91 waliambulia daraja la O – IV
-
Mheshimiwa Spika, ongezeko la idadi ya wanaoshindwa mtihani linatia shaka kwani haijulikani alama za wanafunzi zinakokotolewa kwa kutumia vigezo gani. Aidha haijulikani vilevile kama mwanafunzi anapimwa kwa mtihani ule wa taifa peke yake au maendeleo yake ya kitaaluma (Countinous Assessment) anapokuwa shuleni yana mchango katika ufaulu wake katika mtihani wa Taifa.
-
Mheshimiwa Spika, wasiwasi unazidi kuwa mkubwa pale ambapo kunakuwa na idadi kubwa sana ya wanafunzi wanaoshindwa mtihani na Baraza la Mitihani kukaa kimya bila hata kushauri nini kifanyike ili kunusuru elimu ya Watanzania. Ukimya na usiri wa utendaji kazi wa baraza la mitihani unawakosesha wadau wa elimu wakiwemo wanafunzi, walimu na wazazi taarifa za msingi ambazo kama wangezipata mapema na kwa usahihi pengine wangefanya vizuri zaidi.
-
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya -Baraza la Mitihani la Taifa halitoi taarifa muhimu kwa umma -zinazohusu namna mtihani utakavyofanyika ili wadau wote wajiandae vema. Jambo hili halina taswira nzuri mbele ya jamii kwani linaonesha kwamba Baraza la Mitihani linawavizia wanafunzi ili washindwe mtihani. Kwa mfano Baraza la Mitihani la Taifa halikutoa taarifa kwa umma kwamba -lingebadili mfumo wa utahini kwa wanafunzi wa darasa la saba ambao wangefanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wa Septemba, 2012.(Mfumo mpya ulikuwa ni maswali ya kuchagua na mwanafunzi alitakiwa kutia kivuli (shading) katika jibu sahihi. Na hii ilikuwa ni kwa maswali yote -ya mitihani ikiwemo na hisabati). Matokeo ya kutotoa taarifa hizo mapema ni kwamba kuna uwezekano mkubwa sana wa wanafunzi wa darasa la saba kushindwa mtihani huo si kwa sababu hawana uwezo kiakili, bali ni kwa sababu ya mfumo mpya wa utahini ambao hawajauzoea. Tayari matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba, 2012 yameshatoka na yanadhihirisha maelezo niliyoyatoa hapo juu.
-
-Mheshimiwa Spika, Jambo la kusikitisha ni kwamba licha ya kelele nyingi tunazopiga kuhusu tabia hii mbovu ya Serikali ya CCM ikishirikiana na Baraza la mitihani kuwafaulisha wanafunzi ambao wamefeli mtihani bado imeendelea kuwa kiziwi na kuendelea na mchezo huo mbaya wa kuiangamiza elimu ya Tanzania. Kwa mfano katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba 2012, karibu asilimia 70 ya watahiniwa walishindwa kupata alama 100 kati ya alama 250 (ambayo ndio ilikuwa alama ya juu kabisa). Matokeo ya wanafunzi wengi kushindwa mtihani huo (massive failure) baadhi ya sekondari zilikosa wanafunzi kwa kuwa hawakutimiza vigezo vya kuingia sekondari. Jambo hili lilipelekea Serikali kutoa agizo la kushusha wastani wa ufaulu kutoka alama 100 hadi alama 70 kati ya alma 250 ili kujaza wanafunzi katika sekondari ambazo awali zilikosa wanafunzi.
-
Mheshimiwa Spika, huku ni kuwaibia wazazi fedha za michango katika shule mbalimbali kwa kuwa ni dhahiri uwezekano wa wanafunzi waliofaulishwa kwa njia za ujanjaujanja namna hii hawataweza kuvuka kidato cha pili. Aidha hiki ni kitendo kiovu, hakina tofauti na mwanafunzi aliyeiba mtihani ili afaulu. Sasa kama Serikali nayo inaiba mitihani ili wanafunzi wake wafaulu, kuna haja gani ya kuwa na mitihani?
-
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika katika matokeo ya mitihani ya Mock ya kidato cha pili mwaka 2012, katika kanda mbalimbali hapa nchini yanaonesha kuwa wanafunzi wengi hawakufanya vizuri. Ila jambo la kushangaza ni kwamba katika mtihani wa Taifa wamefaulu vizuri sana. Hii inatia shaka kwa kuwa hakuna uwiano wa ufaulu kati ya mtihani wa Mock na mtihani wa Taifa. Jambo la ajabu hapa pia ni kwamba mtihani wa kidato cha pili mwaka 2012, umeratibiwa na wizara ya elimu badala ya baraza la Mitihani. Swali hapa ni kwamba: Ni kwanini mtihani wa kidato cha pili usimamiwe na wizara wakati una lengo/kusudio moja sawa na mitihani mingine inayoratibiwa na baraza la mitihani?
-
4. Kufaulu Mitihani ya Baraza la Mitihani bila Kujua Kusoma na Kuandika
Mheshimiwa Spika, maajabu ya kufaulu mtihani bila kujua kusoma na kuandika ni kashfa na aibu kubwa iliyolikumba baraza la Mitihani la Taifa hivi karibuni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Haki – Elimu ya Aprili 2012, ni kwamba wanafunzi 5,200 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2012, hawajui kusoma wala kuandika. Hili ni jambo la ajabu kabisa na Tanzania inastahili kabisa kuingia kwenye Kitabu cha Kumbukumbu za Maajabu ya Dunia (The Guiness Book of Records) kwa kushika nafasi ya kwanza kwa kufaulisha wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika. Hii ni kashfa kubwa na Baraza la Mitihani la Taifa haliwezi kukwepa kuhusishwa na kashfa hii. Tukio hili, licha ya kuhujumu ubora wa elimu ya Tanzania lakini pia limelipotezea Baraza la Mitihani la Taifa sifa na mamlaka ya kiuadilifu (moral authority) ya kuendelea kusimamia mchakato wa mitihani ya taifa.
-
5. Baraza la Mitihani la Taifa Kutunga Mitihani bila Kuzingatia Mwongozo wa Mtaala.
Mheshimiwa Spika, mtaala wa sasa unatoa mwongozo kwamba mwanafunzi afundishwe ili awe na uwezo wa kutenda/kufanya jambo kutokana na somo alilofundishwa (competence based curriculum). Hii ina maana kwamba, mtihani utakaotungwa kwa mujibu wa mtaala huu unatakiwa kupima uwezo wa mwanafunzi wa kutenda/kufanya jambo ambalo atakuwa amejifunza darasani. Tofauti ya mtaala wa zamani ni kwamba ulikuwa umejikita zaidi katika maudhui ya somo (content based curriculum)
-
Mheshimiwa Spika, Mgogoro uliobainika kati ya mitaala na Baraza la Mitihani ni kwamba baraza la mitihani limetunga mtihani kwa kutumia mtaala wa zamani bila kutoa taarifa kwa umma na kwa wadau wote wa elimu. Hii imeonekana wazi katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi ambapo maswali yote katika masomo yote yalikuwa ni ya kuchagua. Maswali ya kuchagua majibu (multiple choice) hayana tatizo kama yatatumika kupima ngazi ya kwanza kabisa katika kujifunza.
-
Mheshimiwa Spika, licha ya kuwa maswali ya kuchagua yana umuhumu katika kupima uwezo wa wanafunzi kukumbuka mada walizofundishwa darasana lakini pia aina hii ya maswali ina hasara zake kama ifuatavyo:
i. Maswali haya hayampatii nafasi mwanafunzi kujieleza ili kuweza kupima uwezo halisi wa mwanafunzi katika kufikiri na ubunifu.-
ii. Si kweli kwamba mada nzima inaweza kueleweka kwa jibu moja tena moja tu sahihi. Mfano mzuri katika hili ni masomo ya kijamii (social studies) ambayo majibu yake hutegemea mazingira na maoni ya mtu.-
iii. Tatizo jingine ni kwamba maswali ya kuchagua hasa kwa shule za msingi ni kwamba hata kama mwanafunzi hajui jibu sahihi, kitendo cha kuchagua majibu bado kinampa asilimia 20 ya kuchagua jibu sahihi.
iv. Maswali ya kuchagua hayampi fursa mwalimu au mtoa mtihani kujua tofauti kati ya wanafunzi wenye uelewa mkubwa na wale wenye uelewa mdogo. Ni muhimu kutambua kwamba njia nzuri ya kuongeza ubora wa mtihani ni kutunga maswali yanyopima ngazi mbalimbali za uelewa. Mtihani mzuri kwa maana hiyo ni ule unaoanza na maswali rahisi (ya kuchagua) kupima uelewa mdogo na kuendelea na maswali magumu kupima uelewa mkubwa.
-
6. Mapungufu ya Sheria ya Baraza la Mitihani la Taifa ya 1973
Mheshimiwa Spika, sheria hii ya Baraza la Mitihani la Taifa, licha ya nia yake njema, ni kwamba imepitwa na wakati. Ni wazi kwamba mazingira yetu na mahitaji ya elimu ya mwaka 1973 hayawezi kwa namna yoyote ile kufanana na mazingira na mahitaji ya elimu nchini kwa sasa. Toka mwaka 1973 hadi sasa ni kipindi cha takribani miaka 40. Katika kipindi hiki kuna mabadiliko mengi yametokea hapa yakiwemo mabadilko katika idadi ya wanafunzi, shule, na mitaala, nchini ambayo yanahitaji mabadiliko vilevile ya mfumo wa elimu, mitihani na sheria yenyewe inayotoa mwongozo wa mambo hayo. Ni rai yangu kwamba ili kuliboresha baraza la mitihani la taifa, basi ingekuwa ni busara kutazama upya vile vile Sheria hiyo ili kuona kama inakidhi mahitaji ya sasa.
-
7. Kukosekana kwa Chombo Huru cha Kushughulikia Rufaa za Mitihani
Mheshimiwa Spika, wasiwasi mwingine uliotanda miongoni mwa wadau wa elimu hasa wanafunzi na wazazi/walezi ni juu ya kutokuwepo kwa chombo huru kinachoshughulikia rufaa za mitihani ya wanafunzi. Hali hii inaleta mashaka kama haki itatendeka kwa wanaoomba rufaa ili mitihani yao isahihishwe upya kutokana na kutoamini kwamba kushindwa kwao mtihani uliotangulia kulikuwa halali.
-
Mheshimiwa Spika, imani ya haki kutendeka inakosekana kwa sababu katika rufaa hii, mlalamikiwa ni Baraza la Mitihani, anayepokea rufaa ni Baraza la Mitihani, na anayetoa hukumu ya Rufaa ni Baraza la Mitihani. Kwa kutumia akili ndogo tu ni kwamba Baraza la Mitihani ni lazima litetee uamuzi wake wa awali na kwa maana hiyo mlalamikaji ana hatari kubwa ya kutopata haki yake. Mfano kidogo hapa ni kwamba katika jumla ya wanafunzi wote wa kidato cha nne na sita waliokata rufaa mwaka 2011, matokeo ya rufaa yalikazia matokeo ya awali. Vivile hakuna sababu iliyotolewa kwamba ni kwanini alama hazikubadilika kwa hata mmoja.
-
Mheshimiwa Spika, Angalizo: Rufani ya Matokeo ya Islamic Knowledge ya kidato cha sita 2012, isitumike kama kigezo kwamba Baraza la Mitihani linatenda haki sana katika rufani za mitihani kwa sababu rufani hii ilikuwa na msukumo au shinikizo la Taasisi za dini na pia kulikuwa na tishio la maandamano juu suala hili, kwa hiyo, Baraza lilikuwa katika mbinyo mkali na pia Serikali kupitia Wizara ya Elimu iliingilia kati katika kusukuma rufani hiyo kushughulikiwa mapema ili kunusuru vurugu ambazo zingeweza kutokea endapo maandamano yangefanyika.
-
8. Makosa katika Ukokotoaji wa Alama (Marks) za Watahiniwa
Mheshimiwa Spika, tatizo jingine katika Baraza la Mitihani la Taifa, ni makosa katika ukokotoaji wa alama za watahiniwa baada ya kusahihisha mitihani hiyo. Mfano mzuri hapa ni makosa ya ukokotoaji wa alama yaliyofanyika katika mtihani wa kidato cha sita katika -somo la Islamic Knowledge mwaka 2012. Makosa haya yalifahamika kwa kuwa yalikumba kundi kubwa la watahiniwa ambao walilamika na kuweka shinikizo la kuchunguza jambo hilo. Hii ina maana kwamba kuna uwezekano wa watahiniwa wachache ambao ukokotoaji wa alama zao hukosewa, na kwa kuwa hawaleti malalamiko alama zao hubaki vilevile kimakosa. Makosa kama hayo huathiri alama ya mtahiniwa na hivyo huathiri pia mustakabali wa maendeleo ya mtahiniwa huyo kielimu na hata kimaisha.
-
9. Baraza la Mitihani kutokuwa na Ofisi katika kanda za Elimu au Mikoani
Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba kitendo cha Baraza la mitihani kuwa na ofisi Dar es Salaam pekee, kushughulikia masuala yote ya mitihani nchi nzima ni changamoto ambayo bila mashaka yoyote inaweza kuathiri utendaji mzuri wa kazi na ufanisi wa Baraza la Mitihani.
-
Mheshimiwa Spika, kutokuwepo na ofisi za Baraza la Mitihani katika kanda za elimu au mikoani kwa vyovyote vile kunaleta ugumu katika upatikana wa habari muhimu kuhusu mambo ya mitihani. Aidha ni adha kubwa kwa wadau wa elimu wenye matatizo yanayohitaji majibu ya Baraza la Mitihani la Taifa kufunga safari kutoka mikoani had Dar es Salaam kupata ufumbuzi wa matatizo yao. Hivyo ni rai yangu kwa Serikali, kutazama jambo hili na kujenga ofisi za baraza la mitihani mikoani kupunguza mrundikano wa mashauri ya mitihani katika ofisi moja ya Dar es Salaam ili kuleta ufanisi wa kazi za Baraza la Mitihani la Taifa.
-
Mheshimiwa Spika,
KWA KUWA Baraza la Mitihani la Taifa ni chombo kilichopewa mamlaka kwa mujibu wa sheria kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani yote katika Tanzania isipkuwa kwa vyuo vikuu;
-
NA KWA KUWA ngazi ya elimu anayofuzu mhitimu inapimwa kwa mtihani wa mwisho wa kuhitimu elimu hiyo;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na matukio ya kuvuja kwa mitihani jambo ambalo linaathiri moja kwa moja ubora wa elimu ya mhitimu na kuliingizia taifa hasara kwa gharama zinazotumika kurudia mitihani iliyofutwa kutokana na kuvuja;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na matukio ya kughushi vyeti vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa jambo ambalo limewapotezea wadau wa elimu imani na baraza hilo kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo;
-
NA KWA KUWA viwango vya ufaulu vinazidi kupungua huku baraza la mitihani likishindwa kueleza kiini cha anguko hilo na kutoa ushauri kwa serikali ili kuondoa hali hiyo;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na tukio la ajabu la wanafunzi 5,200 kufaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi uliosimamiwa na Baraza la Mitihani la Taifa bila kujua kusoma na kundika jambo ambalo limeshusha hadhi ya baraza la mitihani na kudhalilisha mfumo wa elimu wa Tanzania;
-
NA KWA KUWA wanafunzi wanaokata rufaa za mitihani wanakosa haki yao ya msingi ya kutendewa haki katika rufaa hivyo kutokana na kutokuwa na chombo kingine kinachoshughulikia rufaa za mitihani;
-
NA KWA KUWA kumekuwa na makosa ya ukokotoaji wa alama za watahiniwa jambo ambalo linaathiri maendeleo ya kielimu na ya kimaisha kwa wa wahitimu;
-
NA KWA KUWA utaratibu wa kukokotoa alama ya mwisho (final grade) ya mwanafunzi hauko wazi na hivyo kumnyima mwanafunzi haki ya kujua alama yake imetokana na mchanganuo upi wa kazi/mitihani aliyofanya; kwa mfano makosa yaliyofanyika wakati wa ukokotoaji wa matokeo ya mtihani wa “Islamic Knowledge” wa kidato cha sita 2012 na Serikali kukiri makosa hayo kufanyika;
-
NA KWA KUWA sheria ya baraza la mitihani ya mwaka 1973 inaonekana kutokidhi mahitaji kwa mazingira ya sasa;
-
NA KWA KUWA mtihani wa mwisho (wa taifa) kwa darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita unalenga kuchuja wanafunzi watakaoendelea na masomo ya juu na watakaostahili kupata fursa mbalimbali za ajira na hivyo kujenga matabaka miongoni mwa wananchi;
-
NA KWA KUWA kutokana na ukubwa wa nchi ya Tanzania, na kuongezeka kwa idadi ya watahiniwa baraza linashindwa kusimamia mitihani kikamilifu katika maeneo yote jambo ambalo husababisha udanganyifu wa mitihani katika baadhi ya maeneo;
-
HIVYO BASI, naliomba Bunge lako tukufu liazimie,
1. Kuiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kufanya uchunguzi maalumu kwa Baraza la Mitihani la Taifa -kwa kuzingatia hadidu za rejea zifuatazo:
-
i. Mfumo wa utendaji kazi wa Baraza la Mitiahani la Taifa.-
ii. Mchakato wa utungaji, usambazaji na usimamizi wa mitihani.
iii. Mfumo wa usahihishaji na ukokotoaji wa matokeo ya watahiniwa.
iv. Mchakato wa kupokea na kushughulikia rufani za mitihani.
v. Uhusiano kati ya Baraza la Mitihani, Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
vi. Uwazi na uwajibikaji wa watendaji wa Baraza la Mitihani
vii. Mfumo wa utoaji habari kwa wadau wa elimu kuhusu mabadiliko au mambo ya msingi ya kuzingatia kuhusu mitihani.
viii. Uwezo wa Baraza la Mitihani -kumudu kazi zake za msingi za kutunga, kusambaza, kusimamia, kusahihisha na kutoa matokeo sahihi kwa watahiniwa.
ix. Kupitia upya sheria ya Baraza la Mitihani ili kuona kama inakidhi mahitaji ya Baraza la Mitihani katika mazingira ya sasa.
x. Kutoa mapendekezo kwa Bunge juu ya namna bora ya kushughulikia masuala ya mitihani ili ikidhi malengo yaliyokusudiwa, na pia kutoa ushauri juu ya muundo wa chombo kitakachokuwa kinashughulikia mambo ya mitihani.
-
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
-
-
______________________________ _____
JOSHUA SAMWEL NASSARI (MB)
MBUNGE WA ARUMERU MASHARIKI

No comments:

Post a Comment