VIONGOZI na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) jana walifanya maandamano na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara
uliofanyika Temeke, jijini Dar es Salaam ambako chama hicho kilitangaza nia ya
kuandaa hoja ya kuwang’oa viongozi wa Bunge.
Hoja hiyo itawasilishwa katika mkutano ujao wa Bunge kwa ajili
ya kuwapigia kura za kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu
wake, Job Ndugai kwa madai ya kukwamisha mijadala yenye masilahi ya wananchi
bungeni.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja
wa Temeke Mwisho, Dar es Salaam, wabunge wa chama hicho wakiwa na uongozi wa
juu, waliwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo kujiandaa na maandamano ya
kuwang’oa spika hao.Kana kwamba hiyo haitoshi, wabunge hao walitangaza namba za
simu za viongozi hao wa Bunge ili wananchi wazitumie kuwashinikiza wang’oke.
Akihutubia katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho
(Bara), Zitto Kabwe alisema Spika Makinda ameshindwa kuwajibika na hivyo
anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha nchi kwenye kipindi cha
kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (Epa).
Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati
hiyo alisema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti ya wabunge wa upinzani
wanaozungumzia masilahi ya wananchi.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliohudhuria mkutano
huo, Zitto alitaja mbinu za kumng’oa Spika Makinda akisema kuwa hoja hiyo
imeshakamilika.
“Kuna njia za kumng’oa Spika Makinda, kwanza kwa kupeleka hoja
ya kutokuwa na imani naye na nimeambiwa hapa kwamba imeshakamilika. Au
tuandamane hadi pale Shule ya Msingi Bunge… au tutumie namba zake kumpigia na
kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…” alisema Zitto na kumruhusu Mbunge wa
Arusha mjini, Godbless Lema kutaja namba za Spika Makinda na Naibu wake.
Baada ya kutaja namba hizo wananchi walionekana wakizipiga na
wengine kutuma ujumbe wa simu.
Mwananchi lilipompigia simu Spika Makinda, simu yake ilikuwa
inaita, kisha inakatika bila kupokewa.
Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto alisema:
“Kamati hii iliundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Spika Samuel Sitta
kwa ushauri wa kina Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu Chadema), waliona kuwa haiwezekani
nchi yenye zaidi ya mashirika 200 yenye thamani ya zaidi ya Sh10 trilioni
yasidhibitiwe na Bunge…Lakini Serikali ya CCM ikaona upinzani umepata sehemu ya
kuzungumzia, sasa wameifuta,” alisema Zitto.
Alitaja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni utendaji wa
kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni kutoka kwenye mifuko
ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
Vyuo Vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo Kikuu cha Arusha.
“Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni
msimamizi tu wa vikao vya Baraza la Wananchi liitwalo Bunge. Makinda lazima
adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia,” alisema Zitto.
Mnyika alia na Maghembe
Katika mkutano huo, Mnyika alitoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji,
Profesa Jumanne Maghembe kuwa ameshughulikia matatizo ya maji kwa Jiji la Dar
es Salaam.
Alisema kutokana na hoja aliyoiwasilisha katika kikao
kilichomalizika mwishoni mwa wiki bungeni kuondolewa, analitaka Bunge lijadili
na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na
ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam.
“Natoa wiki mbili kuanzia leo (jana) Waziri wa Maji (Maghembe)
awe ameeleza hatua anazochukua kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji kwa Dar
es Salaam,” alisema Mnyika na kuongeza:
“Asipofanya hivyo tutaandamana kwenda wizarani kwake
kumshinikiza kutekeleza yale ambayo alisema yanaendelea,” alisema.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa chama hicho, Dk Slaa alimtaka
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kueleza hatua ambazo
amefikia katika ufuatiliaji wa mabilioni yaliyofichwa nchini Uswiss.
Alisema watuhumiwa wa fedha hizo ndiyo vigogo katika Serikali,
ndiyo maana hakuna jitihada zozote zinazofanyika kuhakikisha fedha hizo
zinarudi.
Ahadi ya Mbowe
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema kuwa ule mtindo wa wabunge wa chama hicho kususia vikao vya Bunge
hautakuwepo tena badala yake wataendelea kupiga kelele ndani ya Ukumbi wa Bunge
ili mikutano iahirishwe.
“Tulikuwa tunatoka nje ya Bunge, watu wakawa wanasema kuwa
hatukuwachagua ili mkatoke nje, kwanza ni sawa na kumwachia nguruwe shamba la
mahindi…Sasa hatutoki, tutakuwa tunakomaa na kupiga kelele hadi hoja zetu
zisikilizwe… kama noma na iwe nomaa… kama noma na iwe nomaaa…” alisema Mbowe huku
akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande mwingine Mbowe aliilaumu Serikali kwa kukusanya kodi
nyingi kila mwaka lakini haijali mahitaji ya wananchi.
“Kwa kipindi cha Desemba 2011 hadi Desemba 2012 Serikali ya Rais
Jakaya Kikwete imekusanya kodi ya Sh900 bilioni. Zote wanapeleka hazina, kisha
wanakaa vikao Dodoma na kula na kustarehe. Watoto wetu wanashindwa kwenda
shule…” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kwa upande wa madini, asilimia 60 sawa na Sh256 bilioni
iliyokusanywa kama kodi inatokana na wachimbaji wadogo kama ‘Pay as you earn’
(kwenye mishahara), wakati kampuni kubwa zimelipa Sh56,000 bilioni za kodi.
Hivi wananchi mnasubiri nini? Mapambano haya hayatoshi bungeni tu, ndiyo maana tumekuja
kwa wananchi hadi kieleweke.”
Mapokezi ya wabunge
Wabunge wa Chadema wakiongozwa na Mbowe walipokelewa majira ya
saa nne asubuhi ambapo magari ya chama hicho na idadi kubwa ya wakazi wa Dar es
Salaam walijikusanya kwa ajili ya kujiunga na msafara ulioanzia maeneo ya
Riverside, Ubungo mpaka Uwanja wa Temeke Mwisho.
Shamrashamra za kuwapokea viongozi hao, zilifanyika mpaka majira
ya saa 7.00 mchana baada ya kuwasili katika eneo hilo tayari kwa msafara wa
kuelekea kwenye uwanja huo.
Magari zaidi ya 70 yaliyokuwa kwenye msafara huo yaliyokuwa
yamefurika katika Barabara ya Mandela kwa takriban saa tatu huku magari ya John
Mnyika, Tundu Lissu, Zitto Kabwe na Godbless Lema yakivamiwa kwa furaha na
wakazi hao katika kona ya kuingia Tandika.
Imeandikwa na Elias Msuya, Kelvin Matandiko, Ibrahim Yamola
Mwananchi
No comments:
Post a Comment