Wednesday, February 6, 2013

Chadema wamwakia Spika Makinda


Juzi Naibu Spika, Job Ndugai naye aliahirisha kikao cha Bunge kilichokaa kwa dakika 43 ikiwa ni muda mfupi zaidi baada ya kutokea vurugu zilizoanzishwa na kambi ya upinzani ikiongozwa na wabunge wa Chadema waliodai kuwa hawatendewi haki.
Akizungumzia hoja ya Mnyika, Spika Makinda alisema, “Kulingana na maelezo hayo ya utangulizi, hoja ya Mnyika, ilikidhi vigezo na alipewa nafasi na akawasilisha hoja yake.
Baada ya hoja hiyo kuwasilishwa na kwa mujibu wa kanuni ya 53(6) (c), Waziri wa Maji ambaye ndiye Msemaji wa Serikali kuhusu hoja husika, alipewa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza na kutoa maoni ya shughuli za Serikali.”
Alisema maoni hayo ya Waziri wa Maji yalizingatia Kanuni ya 57(1) (c) inayoruhusu kuingiza au kuongeza maneno mapya kwenye hoja.
Makinda alisema: “Kwa masikitiko makubwa sote tulishuhudia vurugu zilizojitokeza katika Bunge hili hasa wakati wa mjadala wa hoja binafsi za wabunge. Kimsingi huu ulikuwa ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kutokea katika historia ya Bunge letu.”

Dk Slaa amshukia
Akizungumza hukusu matukio hayo, Dk Slaa alisema amewazuia wabunge wake kuonana na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kama wakiitwa hadi hapo rufaa zao 10 zitakazotolewa uamuzi.
“Tumeshawaeleza wabunge wetu wasiende kwenye kamati hiyo hadi Spika wa Bunge na Naibu wa Spika watakapotoa uamuzi wa rufaa zetu 10 mbele ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano,”alisema Dk Slaa.

Dk Slaa alisema wanalaani kitendo cha Spika wa Bunge, Naibu wa Spika na wenyeviti wa Bunge kwa kitendo cha ubaguzi wa wazi kwa wabunge wa upinzani, kinyume na Kanuni ya 8 ya Bunge inayotaka watende haki, uadilifu bila chuki kwa wabunge wote.
Alilaani kitendo cha Naibu Spika Ndugai kuleta ubaguzi wa kutopitisha hoja binafsi ambazo zingeleta tija kwa wananchi zilizowasilishwa bungeni na Mnyika.
“Jana ilitokea fujo bungeni hivyo Naibu Spika alitakiwa asitishe Bunge kwa muda hadi utulivu utakaporejea, lakini alichokifanya ni kafuta hoja ya Mnyika aliyoiwasilisha bila ya kuwahoji wabunge. Huu ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge zinavyosema,” alisema Dk Slaa.
Alisema alishangazwa na uongo wa Spika Makinda bungeni akieleza kuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisimama kwa kifungu 53 (c) wakati alisimama kwa kutumia kifungu 51(c) akipendekeza kuondolewa bungeni kwa hoja binafsi ya Mnyika.
“Spika amekuwa mpotoshaji, muongo na kumsemea, Waziri wa Maji amesimama kwa kutumia kanuni ya 53(c) wakati alitumia kanuni ya 51 (c), kanuni inataka kama hoja imefikishwa bungeni isiondolewe. Kilichotokea hoja imeondolewa,”alisema Dk Slaa.

Nasari alalama hoja
kuzimwa
Nassari aliyekuwa awasilishe hoja yake, kuhusu mwenendo wa Baraza la Mtihani la Taifa unavyoathiri elimu nchini, alisema kuwa atakata rufaa kupinga uamuzi wa Spika.
“Nitakata rufaa Kamati ya Uongozi, hoja yangu iliahirishwa mkutano uliopita, halafu leo inaondolewa bila sababu, kweli sikubali kwa sababu hoja yangu haihusiani na vurugu zilizotokea,” alisema.

Lukuvi apigilia msumari
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema: “Kamati ya Uongozi ndiyo inayopanga shughuli za Bunge na ndiyo inayomshauri Spika inapoona kuna tatizo kabla, wakati na baada ya Bunge.
“Sasa, imeamriwa hivyo kufuta hoja na iko katika kanuni...Unajua Kamati ya Uongozi, mimi naingia kwa nafasi yangu pamoja na Mwanasheria Mkuu,.Sasa hizi hoja binafsi ilikuwa ni ‘favour’ (fadhila) tu sasa tunaona zinakoelekea siko na uamuzi tuliofikia ni kuziondoa.”
Mwananchi

No comments:

Post a Comment