Tuesday, February 19, 2013

Chadema Tanga yalaani mauaji ya Padri Mushi

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Tanga, kimelaani mauaji yaliyofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki la Minara miwili, ambaye alipigwa risasi tatu kichwani na kupoteza uhai wake.

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa CHADEMA, Mkoa wa Tanga Benson Mramba, alisema kitendo hicho sio cha kibinadamu na ni wazi kinaashiria uvunjivu wa amani nchini, hivyo huku akizitaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha waliohusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vinavyohusika.

Mramba alisema, wakati huu Serikali inapaswa kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kubaini watu ambao wanahusika kufanya tukio hilo ambalo sio zuri na lisipokemewa litaleta machafuko nchini siku zijazo.

Alisema tukio la mauaji ya viongozi wa kidini kupigwa risasi Visiwani humo, limekuwa likichukua kasi siku za hivi karibuni na kuitaka Serikali kukemea suala hilo ili lisiweze kujitokeza tena.

“Vitendo kama hivyo sio vya kufumbiwa macho, hivyo tunapenda kuishauri Serikali ichukue hatua madhubuti, ili kubaini kwa nini matukio ya aina hiyo yanatokea visiwani humo na nini chanzo cha matukio hayo,” alisema Mramba.

Katibu huyo alisema suala hilo lisipofanyiwa kazi ipasavyo, litaweza kuleta madhara siku sijazo pamoja na kuleta picha mbaya katika maeneo mbalimbali hapa nchini.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment