KWA mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 (Toleo la 2005), Bunge ni chombo kikuu kilichopewa madaraka kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba (tazama Ibara ya 63(2) kwa ufafanuzi).
Kwa maana hiyo, Bunge, pamoja na mambo mengine lina kazi mbili; yaani, kuisimamia serikali na kuishauri!
Kwa vyovyote vile Bunge la Jamhuri ya Muungano haliwezi kukwepa kazi zake na kuiacha serikali ijisimamie yenyewe kwa kazi ambazo Bunge lilipaswa kufanya.
Nimewajibika kuandika mada hii katika kuwakumbusha wasomaji juu ya hali halisi inayojitokeza kwa Bunge kushindwa kuisimamia serikali na vyombo vyake na au kuishauri juu ya utendaji unaowiana na kazi zilizopangwa kwa minajili ya maendeleo ya watu na nchi kadhalika.
Mwaka 2012 niliandika juu ya kichwa cha habari; ‘Kiti cha Spika kinapwaya: Bunge limekosa mwelekeo’. Nilijaribu kuonesha ni jinsi gani Bunge linavyotumika na nguvu ya wingi wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)! Na kwa wingi wa wabunge wa CCM ndivyo walivyolifilisi Bunge!
Mada ya wiki hii imekuja baada ya Bunge kupokea hoja binafsi ya James Mbatia (Mbunge wa Kuteuliwa, NCCR-Mageuzi). Hoja ya Mbatia ni juu ya ‘kuporomoka kwa ubora wa elimu ya Tanzania.’
Kwa utumizi wa ujanja wa kisiasa, baadhi ya wabunge wa CCM waliochangia hoja hiyo walionekana kukwepa (kwa makusudi) dhima (kazi) yao ya msingi ya kuisimamia serikali katika suala la ubora wa elimu kama lilivyowasilishwa na mtoa hoja ( Mbatia).
Kwa utumizi wa ujanja wa kisiasa, baadhi ya wabunge wa CCM waliochangia hoja hiyo walionekana kukwepa (kwa makusudi) dhima (kazi) yao ya msingi ya kuisimamia serikali katika suala la ubora wa elimu kama lilivyowasilishwa na mtoa hoja ( Mbatia).
Hoja ni nzito na imegusa sekta nyeti ambayo serikali ya CCM pamoja na kujinaki na kujifanidi katika kuiboresha hali inazidi kwenda kombo huku kiwango cha ubora wa elimu kikishuka kwa kasi na kila mwaka!
Kana kwamba wabunge hawajui kazi yao ya kikatiba kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; msisitizo wa wabunge wa CCM waliochangia ukitiwa munda na kiti cha spika wanamtaka mtoa hoja na wabunge wa upinzani waliochangia wakubali kuiacha serikali ifanye upitizi wa sera ya elimu na kuileta kwa Bunge kwa minajili ya kuijadili!
Hapa kuna shida kubwa kwa wabunge wengi wanaotawala Bunge kwa wingi wao (yaani, wabunge wa CCM) katika kile kinachodhaniwa ni kuilinda serikali inayoundwa na CCM katika udhaifu wa utendaji kwenye sekta nyeti ya elimu na mafunzo ya ufundi.
Hoja ilihitaji Bunge kuchukua dhima yake ya kuishauri serikali juu ya kushuka kwa ubora wa elimu nchini!
Kwa ujumla, Bunge haliwezi kuishauri serikali kama halijafanya utafiti na upembuzi wa kina juu ya tatizo na au matatizo yanayoikabili sekta ya elimu Tanzania.
Kwa jinsi hiyo, Bunge lilihitaji kuunda kamati teule ya wabunge kufanya utafiti wa kisayansi kwa kukusanya data, taarifa na takwimu juu ya matatizo ya kimuundo na kiutendaji kwenye sekta ya elimu na kisha kuandaa mapendekezo ambayo yangewasaidia wabunge katika kuishauri serikali juu ya uboreshaji wa sekta ya elimu na hatimaye uboreshwaji wa ubora wa elimu inayotolewa nchini kwenye ngazi husika!
Wabunge wa CCM pamoja na kiti cha spika walisimama kidete katika kupinga uundwaji wa kamati teule ya wabunge kufanya kazi ambayo ni wajibu kwa Bunge katika kutimiza kazi ya kutoa ushauri kwa serikali ili kurekebisha hali ya elimu ya Tanzania.
Ibara ya 63(3) (a) ya katiba inatamka kwamba: “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake; Bunge laweza kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;” kwa jinsi hiyo, ni madaraka ya Bunge kumuuliza Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa, juu ya kuporomoka kwa ubora wa elimu na hata kumtaka aoneshe mtaala (au mtaala) wa elimu (kama ungalipo)!
Inasikitisha sana, tena inatia kinyaa kwa Bunge kushindwa kuitaka serikali kuonesha jinsi inavyoendesha sekta ya elimu katika uandaaji wa sera ya elimu na mitaala husika, kusimamia mchakato wa utoaji wa elimu, mchakato wa tathmini ya kutahini na kupima matokeo ya uelimishaji (kwa mitihani), na usimamizi wa mfumo na utendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Tanzania.
Ushahidi wa moja kwa moja unaonesha kwamba elimu ya Tanzania kuanzia ngazi ya awali, shule za msingi, shule za upili (sekondari) na hata vyuo vikuu imeporomoka kwa kiasi cha kuandaa wanafunzi wasiokuwa na sifa za kitaaluma.
Ukosefu wa maarifa, stadi na maadili ya elimu kwa sehemu kubwa umeifanya sekta ya elimu kuonesha upungufu mkubwa wa kimfumo na kiutendaji hususan kwenye uandaaji wa sera, mitaala ya elimu, na usimamizi wa mchakato wa kufundisha na kujifunza; hali inayowafanya wanafunzi kushindwa kujifunza katika mazingira rafiki na kupata elimu inayoweza kukidhi mahitaji ya taifa na ya kujiajiri kwenye sekta za ujasiriamali na elimu ya kujitegemea.
Elimu ya msingi na ya sekondari imekuwa elimu ya lazima isiyohitaji ubora na ndiyo kusema ‘elimu ya fastafasta’ huku ubora wake ni wa shaka kubwa kwa wanafunzi wengi wanaosoma kwa kiwango husika!
Serikali ya CCM imetumia mafanikio ya kuongeza miundombinu ya madarasa ya shule za msingi na sekondari pasipokuzingatia elimu inayofundishwa kama inakidhi viwango vya ujenzi wa jamii ya wanafunzi walioelimika kwa elimu yenye manufaa, kwa wanafunzi wenyewe na taifa kwa ujumla.
Elimu inayotolewa ni duni kwa vile sehemu kubwa ya shule za msingi na za sekondari (za kata/wananchi) hazina walimu wenye sifa na wa kutosha, hakuna vifaa vya kufundishia na au kujifunzia vya kutosha na vya kisasa, hakuna maabara za kutosha na au vifaa vya sayansi vya kutosha katika kukidhi elimu ya sayansi na teknolojia.
Vilevile, shule nyingi za sekondari hazina maktaba na au vitabu vya kutosha kwa idadi ya wanafunzi. Kwa ujumla, elimu ya msingi na sekondari kwenye shule nyingi imetelekezwa kiutendaji na ubora wa elimu yenyewe ni wa kiwango cha chini sana!
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2007, 2008, 2009, 2010, na 2011 ni vielelezo mahususi katika kupima matokeo ya mipango ya elimu ya msingi (MMEM) na mpango wa elimu ya sekondari (MMES) kwamba programu hizi mbili zililenga katika kuzalisha wanafunzi wengi lakini hazikulenga kuongeza kiwango cha juu cha ubora wa elimu yenyewe kwa kuwa malengo yake yamegeuka hasi badala ya kuleta tija na ufanisi kwenye kuboresha elimu ya Tanzania.
Kama hiyo haitoshi, matokeo ya kidato cha pili kwa watahiniwa wa mwaka 2012 yaliyotangazwa na wizara inayohusika na elimu na mafunzo ya ufundi yameonesha hali halisi ya kushindwa kwa sera ya elimu na mitaala isiyozingatia utashi wa maendeleo ya elimu na mafunzo ya ufundi kwa watoto wa Tanzania.
Kiwango cha ufaulu ni kidogo ukilinganisha na kiwango cha kufeli kwa wanafunzi wengi walioshindwa kupata alama za chini za ufaulu (yaani, alama 30).
Kama chombo cha kuisimamia serikali, Bunge lilitakiwa lichukue hatua za makusudi mwaka 2007 pale matokeo ya kidato cha nne yalipoonesha kiwango cha chini cha ufaulu kwa watahiniwa.
Hata hivyo, kwa msukumo uleule wa kulinda masilahi ya chama, wabunge wa CCM hawakuona haja ya kuisimamia serikali ya chama chao katika kuhakikisha kwamba elimu ya Tanzania inafanyiwa upitizi katika kufanya maboresho ya makusudi na ya kimkakati katika kuinua kiwango cha elimu.
Badala ya kuongeza miundombinu ya elimu isiyokuwa na tija na ufanisi katika ujenzi wa elimu na maarifa ya wanafunzi wa Tanzania katika kujenga elimu yenye manufaa kwa kizazi cha watoto wa hapa nchini. Jukumu la elimu ya watoto wa nchini kwa sehemu kubwa limeachwa kwa wazazi wenyewe!
Dhana hii ya kutelekeza dhima ya taifa kwa wazazi wenyewe ndiyo chanzo cha matabaka ya elimu. Nikiandikia juu ya matabaka ya elimu katika Tanzania, mwaka 2012 nilionesha ni jinsi gani elimu imefanywa ya kitabaka.
Wakati huu Tanzania ina elimu kwa matabaka matatu: yaani, elimu ya daraja la kwanza kwa watoto wa matajiri na wa kipato cha kati, na kati inayotolewa na shule maalumu zinazofundisha kwa Kiingereza (English Medium Schools).
Elimu ya shule maalumu za serikali zinazopewa kipaumbele na umuhimu wa kipekee kwa wanafunzi maalumu wenye uwezo maalumu wa kiakili na au hadhi ya wazazi husika na elimu ya shule za nje ya nchi ambapo baadhi ya wenye nacho na viongozi wa serikali hupeleka watoto wao; na mwisho ni shule maarufu za wananchi (maarufu kama, shule za kata – Saint Kayumba, shule za vodafasta au shule za yeboyebo)!
Hakuna asiyetambua kwamba elimu ya shule za wananchi, ukiachilia umuhimu wake kwa watoto wa walalahoi na maskini wa nchini, zimekuwa hazina viwango vinavyokidhi vigezo vya elimu bora, kwa kisingizio cha kufanikiwa kuongeza kiwango cha wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na darasa la kwanza na ongezeko la wanafunzi wanaopata elimu ya sekondari, imekuwa ikishuhudia kiwango kikubwa cha wanafunzi wanaoshindwa kupata alama za chini za ufaulu na hata wakati mwingine kushuhudia baadhi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kushindwa kusoma, kuhesabu na kuandika (yaani, KKK).
Mfumo wa utoaji wa elimu umekuwa wa shelabela na shaghalabaghala na usiokuwa na usimamizi makini na wenye kuzingatia utashi wa elimu bora na yenye manufaa.
Bunge, kwa ujumla wake, linatambua kwamba: elimu ya Tanzania imefika njia panda! Wizara na waziri anayehusika na elimu wamekwama na hawawezi kutoka kwenye mkwamo hata ikibidi wasukumwe kwa mamlaka ya umma. Na hakika ya mamlaka ya umma ni Bunge lililopewa madaraka kwa mujibu wa Ibara ya 62(2).
Serikali inahitaji isimamiwe katika uboreshaji wa elimu ya Tanzania. Ndiyo maana wakati wa awamu ya kwanza na sehemu ya awamu ya pili, elimu ilifanywa ya taifa na uandaaji wa sera, mitaala na programu za elimu ulizingatia mahitaji ya elimu ya kujitegemea.Mabadiliko ya mfumo na utendaji wa Wizara ya Elimu haukuzingatia utashi sahihi na wa kimkakati katika ujenzi wa sekta ya elimu inayotoa maarifa, ustadi na maadili ya elimu katika kuwaandaa wanafunzi katika kutumika katika kutafuta majibu na suluhisho la matatizo na changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa na baadaye!
Elimu, kama inavyotambulika, ni sekta mtambuka na ni muhali, kuacha usimamizi wake kwa wizara iliyoshindwa kwa muda mrefu huku hadhi ya elimu inayotolewa ikizidi kuporomoka kwa kiasi cha kutisha!
Utakuwa ni wendawazimu kwa Bunge la wananchi kuiacha serikali iliyoshindwa na kuonesha udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa sera ya elimu ya taifa na uandaaji au ukuzaji wa mitaala yenye manufaa kwa elimu ya Tanzania ijisimamie kwenye mambo nyeti kama ya elimu na mchakato wa uelimishaji kizazi cha taifa!
Taifa linahitaji elimu yenye manufaa; kinyume chake tutakuwa tunaandaa taifa litakalokuja kutawaliwa kirahisi kwa vile sehemu muhimu ya kazi zitakazohitaji utaalamu na elimu maalumu zitachukuliwa na wageni, kwa kuwa kizazi cha Tanzania kitakuwa hakina weledi wa kutosha juu ya sayansi ya menejimenti na utawala.
Ukiitazama Ilani ya CCM ya 2010 hadi 2015 katika maeneo saba (7) yaliyoainishwa kwa utekelezaji katika ilani kuna nukta hizi: 9(a) kuimarisha na kuboresha elimu na 9(b) kuandaa rasilimali watu katika maarifa na mwelekeo.
Ukitazama nukta hizi mbili kwa mapana, batini na matini yake unaweza kuona ni kwa jinsi gani kama utekelezaji wake ungalikuwa makini Tanzania ingelipiga hatua katika elimu; kinyume chake utekelezaji wa ilani umekuwa wa kuongeza idadi ya shule na upanuzi wa elimu kwa idadi kubwa ya watoto wa Tanzania kujiunga na shule za msingi na za sekondari ilhali elimu inayotolewa haizingatii ubora unaohitajika kwa maendeleo endelevu ya Tanzania ya sasa na ya kizazi kijacho!
Hakuna shaka yoyote kwamba idadi ya shule za msingi na sekondari zimeongezeka sana, na hakuna shaka kwamba idadi kubwa ya watoto wa Tanzania wanaandikishwa kwenye elimu ya lazima!
Tatizo kubwa na la msingi ni uduni wa elimu inayotolewa kutokana na sababu zinazojulikana na nyingine zinazohitaji utafiti wa kina ambao kamati teule ya wabunge ingesaidia katika kuishauri na kuisimamia serikali katika kutekeleza wajibu wake wa kutoa elimu bora kwa kizazi cha hapa nchini.
Haiwezekani serikali iachwe ifanye vile inavyoona inafaa; na kwa wabunge wa CCM wanaoona kwamba serikali inaweza kuachwa ifanye marekebisho kwenye sera ya elimu watakuwa wanajidanganya na kwa kufanya hivyo Tanzania itakuwa inajichimbia kaburi na kuizika elimu yenye manufaa badala yake tutakuwa tukisomesha bora elimu badala ya elimu bora!
Inawezekana kuna msukumo wa kufanya Tanzania kuwa nchi ya mbumbumbu (mzungu wa reli) au nchi ya wasomi mazezeta na misukule ya wataalamu wanaoshindwa kutumia rasilimali za nchi katika kuleta maendeleo ya watu na nchi kadhalika badala yake wanawatumikia wawekezaji wanyonyaji na wanyang’anyi wa utajiri wa taifa.
Umefika wakati sasa; Bunge la wananchi lifanye kazi yake kwa mujibu wa madaraka yake ya kuisismamia na kuishauri serikali kwa mujibu wa uhuru, haki na usawa kama wawakilishi wa wananchi.
Bunge lisitumike kuilinda serikali inayoonesha kushindwa kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu, kwani kwa kufanya hivyo si tunaua uwezo wa nchi kujitawala bali pia tutakuwa tunaandaa kizazi cha Tanzania kitakachotawaliwa kielimu kwa kukosa fursa ya elimu sahihi na yenye manufaa kwenye ulimwengu unaokua katika sayansi na teknolojia.
Mwisho, nawapongeza wabunge wa vyama vya upinzani walioonesha kuchoshwa na mfumo wa wabunge wa CCM wakiongozwa na kiti cha spika (alichokalia Job Ndugai), kwa kuzuia mjadala mpana juu ya hoja nzuri na muafaka ya James Mbatia katika kulipatia ufumbuzi suala la kuporomoka kwa ubora wa elimu ya Tanzania.
Wabunge wa CCM wana nafasi nyeti ya kuisimamia na kuishauri serikali inayoundwa na chama chao. Kitendo cha wabunge wengi wa CCM kushindwa kuisimamia au kuishauri serikali kinawapotezea uhalali wa kuendelea kupewa nafasi ya kuongoza shughuli za serikali. Ni wajibu wa kila mbunge kutambua wajibu wake katika kutekeleza madaraka ya Bunge kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 (Toleo la 2005). Tanzania itajengwa na wenye moyo; na wabunge wanatakiwa wawe mstari wa mbele katika mapambano ya kuboresha elimu ya Tanzania! Tanzania inahitaji elimu bora na si bora elimu kama ilivyo sasa.

No comments:
Post a Comment