Saturday, February 2, 2013

Arfi aibana serikali ubovu wa barabara


MBUNGE wa Mpanda Mjini, Saidi Arfi (CHADEMA), ameibana serikali na kuitaka ieleze ni lini itakamilisha ujenzi wa barabara ya Tabora-Mpanda-Kigoma.
Akiuliza swali la nyongeza jana mbunge huyo pia alitaka kujua serikali ina mpango gani wa dharura wa kuinusuru barabara hiyo kutokana na kuwa katika hali mbaya.
Awali katika swali la msingi la mbunge wa Manyoni Magharibi, John Lwanji (CCM), alitaka kujua ni lini ujenzi wa barabara ya Mkiwa-Itigi-Rungwa –Makongolo utaanza.
Akijibu maswali ya wabunge hao Naibu Waziri wa Ujenzi, Greyson Lwenge, alisema kuwa kuhusu barabara ya Tabora – Kigoma, serikali inajipanga kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Alisema kuhusu barabara ya Mkiwa-Itigi-Rungwa na Makongolosi, upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni ulishafanyika na kukamilika mwaka 2011 kwa gharama ya sh bilioni 3.6.
Alisema kuwa baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina, serikali itatafuta fedha za ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami.

No comments:

Post a Comment