Saturday, January 19, 2013

Waziri mwingine aihujumu CHADEMA


BAADA ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira kutajwa kuwa nyuma ya mkakati wa kukihujumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waziri mwingine ametajwa kufadhili kundi la vijana wasaliti wa chama hicho.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumamosi, umebaini kuwa kigogo huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni naibu waziri wa wizara moja nyeti, juzi alifadhili kikao cha kutathimini athari za tamko la aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa wa Baraza la Vijana la CHADEMA Taifa (BAVICHA) aliyefukuzwa, Juliana Shonza.
Naibu huyo pia anadaiwa kutumia siasa za ukanda na ukabila kuwarubuni vijana waliofukuzwa uanachama wa BAVICHA.
Baadhi ya vijana hao waliofukuzwa uanachama na kuungwa mkono na naibu waziri huyo, ni Shonza, Mtella Mwampamba aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki 2010 na Habib Mchange aliyegombea Kibaha Mjini.
Vijana hao walivuliwa uanachama baada ya BAVICHA kujiridhisha kuwa walikuwa wakitumiwa na CCM pamoja na baadhi ya viongozi wawili ndani ya CHADEMA ili kutoa matusi kwa viongozi waandamizi wa chama na kuwazushia uongo.
BAVICHA pia iliwataja Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martine Shigella na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba, kuwa nyuma ya mkakati huo.
Mmoja wa wajumbe walioshiriki kikao hicho juzi usiku, alisema kuwa watatathmini kazi aliyokuwa amepewa Shonza.
Alisema kuwa Shonza alipewa kazi ya kutoa tamko la kuwatukana viongozi wakuu wa CHADEMA, kukishambulia chama na kuwashambulia baadhi ya viongozi wa BAVICHA, hasa mwenyekiti wake, John Heche.
“Tulikutana pale Mikocheni kwenye nyumba moja, tukajadili kwa mapana mkutano wa Shonza na waandishi wa habari baada ya kufukuzwa. Sikujua nyumba ni ya nani, lakini aliyekuwa mwenyeji zaidi ni Shigela,” alisema.
Aliwataja wengine waliohudhuria kikao hicho kuwa ni Mwampamba, Tambwe Hiza, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM, Salumu Hapi pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mbozi, mkoani Mbeya, Wareni Kamnyoge.
“Katika mkutano ule, Shigella alimuuliza Shonza anaendeleaje baada ya kutoa tamko na athari zake kwa jamii. Shonza alijieleza na baadaye wajumbe wakamsifu kwa kusema CHADEMA ni chama cha Wachaga na cha ukanda,” aliongeza.
Aliongeza kuwa Shigella alisema kuwa; “Hapa kwenye ukanda na ukabila, nakwambia Juliana umetufurahisha. Maana sasa, tutakuwa tumefanikiwa sana. Tutatembea na agenda hii hadi mwaka 2015.”
Shigela hakupatikana kuthibitisha madai hayo, lakini Tambwe aliliambia gazeti hili kwa ufupi kuwa; “Mikakati ya kuwatumia vijana wa CHADEMA inaendelea vizuri.”
Akizungumza kwa kujiamini, Tambwe alisema juzi hakwenda Kinondoni hasa Mikocheni, lakini akathibitisha kuwa; “unachokisema cha kuwatumia vijana wa CHADEMA ni kweli maana mikakati ni ushindi katika uchaguzi mkuu 2015.”
Kuhusu kuwapokea CCM vijana hao, Tambwe alisema hayo mengine ya kutumika au kupokelewa waulizwe viongozi maana hao ndiyo wasemaji.
Shonza hakupatikana ili kuzungumzia madai hayo, ingawa kuna taarifa kuwa wameahidiwa kazi kulingana na elimu zao. Shonza inadaiwa kuwa ataajiriwa kwenye kazi za ustawi wa jamii, Mwampamba ameahidiwa ualimu.
Chanzo hicho kinaongeza kuwa, kwa mujibu wa mkakati huo, Shonza na kundi lake, wamepanga kufanya ziara mikoani, wakianzia Mbeya, Iringa na baaye Mwanza.
Naibu waziri anayedaiwa kuwafadhili inasemekana anatumia ukabila na ukanda akisema kuwa waliofukuzwa ni vijana wa Mbeya, na hivyo anataka kuwatumia kuivuruga CHADEMA mkoani humo hasa Jimbo la Mbeya Mjini analojitapa kutaka kulirejesha CCM.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment