Wednesday, January 30, 2013

Uchaguzi waiva CHADEMA


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema utekelezaji wa mpango mkakati wa nguvu ya umma uliogawiwa katika kanda 10 na vikosi vyake nchi nzima, utakwenda sambamba na uchaguzi wa ndani wa chama hicho kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.
Hayo yalisemwa katika kikao cha dharura cha Baraza Kuu la chama hicho kilichokuwa na agenda nne ambazo ni mapendekezo kuhusu maudhui na mchakato wa katiba mpya, haja ya kufanya marekebisho katika kanuni za chama na kutunga muongozo, mpango kazi, mkakati na mwendelezo wa operesheni ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) na bajeti ya chama kwa mwaka 2013.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao hicho, ambapo ratiba ya uchaguzi wa ndani kwa ngazi ya misingi, matawi, majimbo na wilaya utafanyika Aprili hadi Septemba mwaka huu.
Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa chaguzi za mikoa zitafanyika Novemba na ngazi ya taifa utaanza kwa mabaraza ambapo Desemba 11 utakuwa wa Baraza la Wanawake (Bawacha).
Kwamba Desemba 12, watachaguana Baraza la Vijana (BAVICHA) na Desemba 13 utafanyika uchaguzi wa Baraza la Wazee.
Alisema uchaguzi huo utaendelea Desemba 14 kwa Baraza Kuu, Desemba 15 Mkutano Mkuu, Desemba 16 ni Baraza Kuu jipya na Desemba 17 watamalizia na uundwaji wa kamati kuu mpya.
Mnyika alisema ratiba hiyo ni mwendelezo wa M4C kwa wananchi kuiwajibisha serikali mwaka 2013 na kueneza sera sahihi za chama hicho ili kuwaunganisha na kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi wa mitaa 2014 na ule mkuu wa 2015.
Juzi, chama hicho kilipitisha mpango mkakati kwa kumega madaraka ya makao makuu katika kanda kumi yakiwa ni maandalizi ya kushika dola 2015.



No comments:

Post a Comment