Thursday, January 31, 2013

Mtei: Katiba Mpya iunde tume ya kuchuja wagombea urais


ALIYEWAHI kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei jana alipata fursa ya kutoa maoni yake ya kuundwa kwa Katiba Mpya na kupendekeza kuwa Katiba ijayo ianzishe Tume Maalumu itaka yotumika kuwachuja wagombea urais.
Mtei alisema vyama vya siasa vikishapitisha majina ya wagombea urais, wanatakiwa kuyapeleka kwenye tume hiyo ili wafanyiwe usaili kwa ajili ya kupima uzalendo, uadilifu na uwezo wao wa kielimu ili kujiridhisha kama wanafaa au la.
Aliongeza kuwa ushindi wa kiti cha urais unatakiwa kuwa zaidi ya asilimia 50 na siyo chini ya hapo. Alisema baada ya hapo uchaguzi urudiwe kwa wagombea wawili ambao wamefuatana kwa kura na atakayeshinda ndiyo awe rais wa nchi.
Alisema mgombea urais ni lazima atokane na chama cha siasa chenye sera zinazojulikana na mwenye wafuasi ili Watanzania wawe na imani naye zaidi tofauti na mtu asiyekuwa na chama wala wafuasi kwani watu watakuwa hawana imani naye.
Mzindakaya
TUME ya Mabadiliko ya Katiba jana iliendelea kukusanya maoni kutoka kwa watu maalumu na jana ilikuwa zamu ya Mbunge Mstaafu, Chrisant Mzindakaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), Thomas Ngawaiya kuwasilisha maoni yao mbele ya Tume hiyo.
Mzindakaya alipendekeza mambo mbalimbali, huku akitoa onyo kwa watu wanaopendekeza kuvunjika kwa Muungano. Alisema yeye amependekeza Muungano uendelee  kuwapo na kuwe wa Serikali mbili kwani ni uhai wa Taifa hili.
Alisema kinachotakiwa ni kuwapo kwa chombo cha kikatiba kitakachoshughulikia matatizo ya Muungano kwa maslahi ya taifa na siyo kuongeza Serikali tatu au kupunguza iwe moja.
Alisema kuna watu wanaongojea kwa hamu  kuona Muungano huu unavunjika ili waweze kurudi hapa nchini  kwa nia ya kuwagombanisha Watanzania  na kupora rasilimali za nchi. Mzindakaya alisema Katiba ijayo pia inatakiwa kulinda maslahi ya wananchi na siyo viongozi wachache wanaotamani kupata vyeo kila kukicha.
Ngawaiya
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (CEGODETA), Thomas Ngawaiya amependekeza Katiba ijayo iruhusu Watanzania wanaoishi nchi za nje kuwa na uraia wa nchi mbili na uwekwe utaratibu wa kuwatoza kodi ili fedha hizo zirudi nyumbani na kusaidia maendeleo ya Taifa.
Ngawaiya amependekeza Katiba ijayo irudishe Serikali ya majimbo chini ya Rais mmoja. Alisema magavana watakaopatikana watatokana na uchaguzi wa wananchi wenyewe na majimbo yawe 10, Bara kuwe na majimbo 8 na   Zanzibar mawili.

chanzo vijimambo blog

No comments:

Post a Comment