JIBU LA SWALI LA MBUNGE HAI
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA) ameibana serikali na kuitaka ieleze ni lini itakuwa na mikakati ya kweli ya kuondoa msongamano wa magari unaochangia ucheleweshwaji wa upimaji wa magari katika minzani.
Kauli hiyo ya Mbowe ilitokana na swali la nyongeza aliloliuliza jana bungeni, huku akiitaka serikali ilieleze Bunge juu ya mikakati yake ya haraka ya kuondoa kero ya msururu wa magari unaotumia muda mrefu katika vituo vya mizani.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Vunjo, DkAugustino Mrema (TLP), alitaka kuelewa ni kwanini mizani mikubwa ya magari ya Kijiji cha Kilototoni katika jimbo hilo upimaji wa malori yaliyo tupu husababisha kero na foleni kubwa wakati mizani nyingine hazipimi malori yasiyo na mizigo.
Aidha, alitaka kujua kuna utaratibu gani wa kuhamisha mzani huo ili kuondoa usumbufu wa magari, na kijiji hicho kinapata mapato kiasi gani kutokana na mzani huo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Greyson Lwenge, alisema kuwa kwa sasa serikali inaandaa utaratibu wa kujenga mizani ya magari pande zote za barabara badala ya kujenga upande mmoja.
Lwenge alikiri kuwepo kwa msongamano wa magari katika vituo vingi vya mizani.
Alisema kuwa katika kuondoa msongamano huo, serikali imejipanga kujenga mizani ya kisasa zaidi huku malipo yake yakifanywa kwa njia ya mtandao ili kupunguza vitendo vya rushwa.
Lwenge alisema kuwa fedha zinazokusanywa katika vituo vya mizani nchini uwasilishwa kwenye Mfuko wa Bodi ya Barabara ili zitumike katika matengenezo na ukarabati wa barabara kuu, za mikoa na wilaya.
No comments:
Post a Comment