Saturday, January 12, 2013

Lissu: Hakuna sababu ya baadhi ya watu kuwa juu ya sheria


MCHAKATO wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi yatakayosaidia katika uundwaji wa Katiba Mpya unaendelea na safari hii ni zamu ya makundi maalumu vikiwemo vyama vya siasa ambavyo vimeanza kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mikutano hiyo kati ya Tume na wawakilishi wa vyama vya siasa inafanyika katika Ofisi Kuu za Tume pamoja na Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Vyama vyote vimepewa fursa ya  kushiriki katika utoaji maoni na baadhi ya mambo ambayo wameyapendekeza kuwamo katika Katiba Mpya ni pamoja na utawala wa majimbo na kuwapo kwa mgombea binafsi.
Kimsingi hoja hizi zimekuwa zikitolewa maoni mara nyingi na wananchi katika mikutano mbalimbali ya Tume iliyokuwa ikifanyika nchi nzima kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, tofauti na sasa ni kwamba wanasiasa wamezieleza kwa undani zaidi na kuzifafanua namna gani zinavyoweza kuingia katika Katiba ijayo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejikita zaidi katika muundo wa Muungano na utawala wa majimbo, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejielekeza kwenye hoja ya mgombea binafsi.
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu anasema kuwa chama chake kinataka kuona Katiba Mpya inakuja na mfumo mpya ambao utaleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali zikiwamo utawala, rasilimali, ulinzi wa mali za umma, haki za binadamu, uwajibikaji serikalini na muundo wa Jamhuri ya Muungano ambao utasaidia kuunusuru usivunjike.
Lissu anasema kuwa kuna kila sababu ya Katiba Mpya kuleta mabadiliko katika muundo wa Muungano ambao Chadema wanapendekeza uwe Muungano wa Shirikisho wa Serikali tatu, yaani Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ndogo ya Jamhuri ya Muungano.
“Hatuwezi kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano kwani una upungufu mwingi. Ni fursa nzuri ambayo tumeipata ya kutengeneza Katiba Mpya ya nchi ambayo kimsingi inapaswa kuleta mabadiliko yatakayounusuru au kuuokoa Muungano usivunjike. Tukikosea tunaweza kujikuta tunatengana kama ilivyo kwa Ethiopia na Eritrea, Sudan na Sudan Kusini, Yugoslavia na Czechoslovakia,” anasema Lissu.
Pia anasema kwa kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa hiari kunatakiwa kuwe na haki ya kujitoa kwa upande usioridhika kuendelea kuwa kwenye Muungano.
Anasema utaratibu wa kujitoa uwe kwa njia ya kura ya maoni itakayopigwa na wananchi wa upande mmojawapo wa Muungano na ikiwa theluthi mbili ya wananchi wakikubali kujitoa basi iruhusiwe wajitoe kwa sababu Muungano huu haukuwa wa lazima.
Lissu anaongeza kuwa kwenye mambo ya Muungano wamependekeza yawemo mambo saba tu ambayo ni ulinzi na usalama, wizara zisizozidi 18, Bunge lisilozidi wawakilishi 300, mamlaka ya uteuzi ya Rais ambayo yanapaswa kupunguzwa, Rais ashtakiwe akifanya makosa ya jinai, pamoja na kuweka bayana suala la umilikaji wa rasilimali za nchi.
Kuhusu mamlaka ya uteuzi ya Rais anaeleza kuwa ni lazima yapunguzwe ili kuiondoa nchi kwenye mfumo wa urais wa kifalme.
Akapendekeza kuwa badala ya Rais kuwateua watu wa kushika nafasi mbalimbali za uongozi, wateule hao watatakiwa kwa mujibu wa Katiba Mpya kuomba nafasi hizo za kazi kupitia tume huru za kitaalamu na wakifanikiwa watatakiwa kuthibitishwa na Bunge.
“Pia kinga ya Rais inatakiwa kuondolewa ili kuleta nidhamu ya utendaji katika ofisi hii ya umma. Akifanya makosa ya jinai ashtakiwe kama mhalifu mwingine, hakuna sababu ya baadhi ya watu kuwa juu ya sheria, kila mtu awe chini ya sheria,” anasisitiza Lissu.
Anabainisha kuwa mwaka 1895 Utawala wa Kikoloni wa Wajerumani walianzisha dhana ya mali ya umma katika umilikaji wa rasilimali za nchi ambapo Waingereza walipenda kuiita mali ya Serikali. Anasema huu ni upungufu ambao Katiba Mpya inapaswa kuuondoa na kutamka kuwa maliasili zote ni mali ya wananchi.
Lissu anafafanua kuwa rasilimali zikiwa chini ya mamlaka ya wananchi, Serikali italazimika kupata ridhaa ya wananchi wa eneo husika kabla ya rasilimali zao kuanza kuvunwa.
Anasema kuwa mfumo wa sasa wa Serikali kuwa ndiyo mmiliki wa rasilimali za nchi hauwatendei haki wananchi wa mahali ambako rasilimali zinatoka au kupatikana.
“Nchini Nigeria kuna eneo linaitwa Niger Delta ambako kuna utajiri mkubwa wa mafuta lakini wananchi wake ni maskini sana, hapa kwetu Mji wa Geita licha ya kuwa na dhahabu nyingi na yenye ubora wa hali juu lakini wananchi wa eneo hilo bado ni maskini, haya ni matokeo ya rasilimali kuwa mikononi mwa Serikali badala ya kuwa mikononi mwa wananchi,” anasema Lissu.
Ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na rasilimali zao, Chadema  wamependekeza kwamba Katiba ijayo itamke kuwa mrabaha  unatakiwa kubaki au kupelekwa kwa wananchi ambako rasilimali husika inavunwa ili kuharakisha maendeleo yao badala ya kila kitu kwenda Serikali Kuu.
Kuhusu utawala wa majimbo, Lissu anasema hauna budi kurejeshwa na akapendekeza yawepo majimbo yasiyozidi kumi ili kuleta uwiano wa matumizi ya rasilimali katika maeneo yote nchini.
Lissu anasema chama chake kimependekeza majimbo hayo na mikoa yake kwenye mabano kuwa ni Jimbo la Nyanza Magharibi (Kagera, Geita na Shinyanga), Nyanza Mashariki (Mara, Mwanza na Simiyu), Ziwa Tanganyika (Kigoma, Katavi na Rukwa).
Majimbo mengine ni  Jimbo la Kati (Tabora, Dodoma, Singida na Iringa), Jimbo la Kaskazini (Kilimanjaro, Arusha na Manyara), Pwani ya Kaskazini (Tanga, Sehemu ya Mikoa ya Pwani na Morogoro), Pwani ya Kusini (Mtwara, Lindi, Wilaya za Mafia, Rufiji na Ulanga),Kanda ya  Nyanda za Juu (Njombe, Mbeya na Ruvuma) pamoja na Jimbo la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Lissu, mfumo  utakaotumika kuwapata viongozi wa majimbo hayo wakiwemo magavana ni ule wa kuchaguliwa na wananchi wenyewe, ila kwa miji yenye hadhi ya Majiji itaongozwa na Mameya wa kuchaguliwa pia.
“Pia tunapendekeza 40% ya mapato ibaki katika Jimbo ili kusaidia shughuli za maendeleo, na asilimia 60 iende Serikali Kuu,” anasema Lissu.
Mwakilishi wa CCM, Andrew Chenge anasema kuwa Chama chake kimeridhia hoja ya mgombea binafsi kuwemo katika Katiba Mpya, lakini akatahadharisha kuwa asipatikane kwa misingi ya udini au ukabila.

No comments:

Post a Comment