Tuesday, January 29, 2013

Gavana Ndulu ataka Katiba iipe uhuru BoT


Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetaka katiba mpya kuwekwa kipengele kitakachoiwezesha kufanya  kazi kwa uhuru pasipo kuingiliwa kisiasa.

Kauli hiyo  ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT,  Profesa Benno Ndulu,  wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema endapo BoT itawekewa ulinzi kikatiba, itaweza kufanya kazi zake  kwa uhuru zaidi.

“Tumezungumzia nafasi ya Benki Kuu na umuhimu wa kuhakikisha kunakuwapo na kinga ambayo itaiwezesha kufanya kazi zake kwa uhuru  pasipo kuingiliwa kisiasa,” alisema.

Jambo jingine ambalo alisema wametaka liwapo katika katiba ni kuhusiana na kutenganishwa kwa mamlaka zinazohusika na utoaji wa fedha na zile zinazohusika na utunzaji wa fedha.

Kadhalika, alisema wametaka kuwapo na udhibiti wa utoaji wa fedha zaidi kwa ajili ya kulinda uchumi wa nchi.

“Kutenganisha mamlaka zinazotunza fedha na zile zinazotoa fedha pamoja na kuweka udhibiti kwa watu kutoa fedha zaidi katika akaunti  kutasaidia uchumi wa nchi kulindwa,” alisema na kuongeza:

“Hiyo itasaidia hata wale wanaoenda kuweka fedha nje ya nchi wasiweke na  endapo kutakuwa na kinga ya kutosha katika mamlaka hizo watu wengi watakuwa wanaweka fedha zao na hivyo uchumi wetu utaongezeka.”

Pia alisema mamlaka hizo zote zinatakiwa ziwe na kinga ya kutosha ili ziweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi.

Alisema mpaka sasa ni dola za Marekani bilioni 2.2 ambazo zimetunzwa katika akaunti za watu katika benki za hapa nchini.

Profesa Ndulu alisema pia wametaka sheria za BoT zilizopo katika Bunge ziwekwe katika katiba ili ziwe na nguvu zaidi na  kufanya kazi kwa uhuru.
“Kuna sheria za bunge zinazolinda BoT, lakini tunataka sheria hizo ziainishwe kikatiba na itasaidia  kufanya kazi kwa uhuru zaidi tofauti na ilivyo sasa,” alisema Profesa Ndulu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment