TAARIFA YA DEMOCRATIC PARTY (DP) KUHUSU
GESI NA MASLAHI YA MTWARA CORRIDOR
DP tunatoa tahadhari kwamba hali inayoendelea kuwa mbaya huko Kusini mwa Nchi yetu, inazidishwa na ukosefu mkubwa wa uzalendo na hekima katika utawala wa juu wa CCM, kiasi cha kuzidi kuumwagia gesi moto unaowaka badala ya kutumia historia ya tatizo lenyewe ambayo peke yake ndiyo inayoweza kuwapa busara ya zimamoto! Tunapenda ieleweke kuwa madai kwamba umeme wa gesi hiyo ufuliwe kule kule Kusini yanatoka katika uchungu wa wananchi wote wa Kusini mwa Tanganyika yaani Mtwara Corridor, uchungu wa kudhulumiwa, kudhalilishwa na kusahauliwa kabisa kimaendeleo tangu tulipotapata uhuru mpaka leo. Serikali ndiyo chombo hasa cha kuzungushia gurudumu la maendeleo, ambalo lilielekezwa Kaskazini tu mpaka Kusini kukabaki pori na giza nene, kiasi kwamba watumishi wa umma walipokuwa wanapangiwa kufanya kazi Kusini, mara nyingi ikiwa kama adhabu, waliamua kuacha kazi. Kupuuza upande mmoja wa nchi kimaendeleo huwa ni bomu la hatari litakaloteketeza hapo baadaye, kama inavyokuwa hivi leo Wananchi wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba sumaku ya wawekezaji wa miradi mikubwa ya kuwaletea maendeleo ni nishati na miundombinu, lakini watawala wa CCM waliwanyang’anya Reli ya Kusini kwa uharamia wa kung’oa mpaka mataruma na kufutilia mbali hata na tuta lenyewe! Wananchi wa Kusini ni binadamu wanaoumia kwamba hata barabara ya kuwaunganisha na dunia nyingine haijaisha mpaka leo, lakini wanayaona makufuru ya ufujaji wa kutisha wa serikali ya CCM hiyo hiyo wa mabarabara ya Jijini Dar es Salaam sasa kukwanguliwa lami nzuri kabisa ya mabilioni ya fedha, ambayo ingeishi zaidi ya miaka saba mingine!Serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka misingi yote ya uchumi wa nchi, kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na maisha bora ya wananchi wenyewe, lakini mbali ya ule uharamia wa kuwang’olea ile reli, fungu la uboreshaji wa Bandari ya Mtwara ambayo ndiyo yenye kina kikubwa zaidi cha asili kinachofaa zaidi kuliko hata bandari ya Dar es Salaam, sasa ni fungu la kujengea bandari ya Bagamoyo nyumbani kwa Kikwete, ambapo ni hatua kadhaa tu jirani ya Dar es Salaam! Zao la pamba ambalo utawala wa mkoloni ulilijengea msingi imara kwa ajili ya uchumi wa nchi na wananchi wake, lilishamiri vizuri zaidi Kusini kama ulivyoshamiri hata mkonge. Lakini kwa kutowathamini watu wa Kusini na kutojali kabisa hatima yao kiuchumi na kimaisha, utawala wa CCM uliyanyima mazao hayo kipaumbele kule na hata ule msukumo unaopasa, wakati kule Kaskazini mwa nchi hiyo hiyo umeme ulisha sambazwa mpaka migombani!
Zao la korosho lililobaki angalau katika uwezo wao ulio duni, limekuwa kama mnyororo wa utumwa, kwa sababu wakivuna hawapati kitu bali kupunjwa kabisa bei kama zikinunuliwa. Ni zao linalotajirisha sana ma--------- kwa kuwakondesha vibaya sana walalahoi wa Kusini.
KUHUJUMIWA KWA MAONO YA SHUJAA OSCAR KAMBONA
Watu wa Mtwara Corridor wanafahamu kwamba shujaa Oscar Kambona ndiye hasa aliyefanikiwa kuiombea Nchi yetu msaada wa China wa Reli ya Uhuru, na uwezo wake wa kisiasa na hasa baada ya kung’ara katika ukombozi wa Afrika na uhusiano wake binafsi na Chou en Lai ulivyotusaidia. Tunajua kwamba kwa ajili ya hazina za Taifa letu za mafuta na gesi kule Kusini, pamoja na rutuba isiyo kawaida kwa ajili ya kilimo, pamoja na raslimali za madini ya thamani njia yote, achilia mbali wanyamapori Selous, na chuma cha Liganga na mkaa wa mawe Mchuchuma, reli hiyo ilikuwa ianzie Bandari ya Mtwara iliyopangiliwa pia uboreshwaji wa nguvu, na ilikuwa iende mpaka Ziwa Nyasa baada ya kona ile ya kwenda Liganga na Mchuchuma hadi Rukwa kwenye shaba. Hauwezi kusahaulika ushuhuda kwamba baada ya shujaa Kambona kuelezea baraza la mawaziri mafanikio haya ya safari yake China, na hasa Bandari ya Mtwara na reli ya uhuru wetu wa kiuchumi, alitukanwa na mkuu wake kwamba ni mkabila sana, kwa ‘kosa’ la kutaka hiyo miundombinu ya bandari na reli iwe Kusini! Mzalendo Oscar Kambona alijitetea kwa hekima ya rohoni kiasi cha kuwatoa machozi baadhi ya wenzake kwamba, “Mimi si mkabila wala sina kosa, kama kuna mwenye makosa basi ni Mwenyezi Mungu”. Alipotakiwa aeleze ana maana gani alisema, ‘Kwa sababu Mungu angetuwekea kule Kilimanjaro au Musoma hizi hazina za gesi, mafuta, madini ya thamani na Selous ya wanyamapori, chuma na mkaa wa mawe na shaba reli ingepita, lakini sasa alikosea akaweka Kusini. Hakuna mwehu wa kubisha kwamba maono haya ya hayati Oscar Kambona yalikuwa ya uzalendo wa hali ya juu kwa ajili si ya watu wa Kusini, bali kwa muujiza wa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa la wana wa Tanganyika kuwa katika kilele cha Afrika na hata dunia. Hatushangai kwamba ingawa shujaa Oscar Kambona ndiye aliyeanzisha Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kwa maono yake binafsi ambayo Nyerere ilibidi ayaafiki, Kambona akayauza kwa rafiki yake mpenzi Ahmed Sekou Toure aliyempa cheki tupu ya kwanza, wakamhusisha shujaa Kwame Nkurumah aliyetoa cheki ya pili, na walipomshirikisha Mfalme Haile Selasie naye akatoa cheki ya tatu, shujaa Oscar Kambona akaupambisha moto wa ukombozi wa Afrika, mpaka wivu ulipompiga vita kali hadi akaikimbia Nchi yake. Ni dhahiri kwamba watu wa Kusini ya Tanganyika au Mtwara Corridor walikuwa na sababu ya kumpenda na kumheshimu hayati Oscar Kambona, kwa sababu maono yake kwa ajili ya hatima ya Taifa letu yalikuwa baraka kwao. Lakini hakuna hata choo ya Jiji iliyoweza kuitwa jina la shujaa Oscar Kambona, licha ya sifa na heshima aliyoiletea Nchi yetu, hii ni aibu! Nyerere alipogeuka kuwa adui mkuu wa shujaa Oscar Kambona watu wengi wa Kusini waliteseka kwa ajili hiyo, na koroboi ya maendeleo Kusini ilionekana kuzimika kiaina, hadi ilipoibuliwa upya na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) mikakati mipya ya maendeleo ya Kusini, kwa jina la Mtwara Corridor, iliyofanyiwa kazi kwa dhati na mzalendo Simbakalia ambaye sasa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Koroboi hiyo ikazimika tena alipoondolewa huyu kutoka NDC.
UFUMBUZI WA MOTO WA HASIRA ULIOLIPUKA KUSINI
Moto huu usipozimishwa kwa hekima ya hali ya juu, si ajabu ukaimeza mikoa yote ya Kusini yaani Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na hata Rukwa, tukakuta yanazaliwa mataifa mawili mpaka ukiwa Reli ya Kati! Tumeeleza kwa kifupi sana historia na sababu za msingi za hasira za watu wa Kusini, kwamba wao pia ni binadamu, na kwamba lugha yao ya amani ilipuuzwa kwa miaka yote 52 tangu nchi yetu ilipopata uhuru. Lakini tunapinga propaganda za uwongo za watawala waliosababisha hasira hii, kwa ukweli kwamba: 1. Watu wa Kusini hawazuii gesi isitoke kwa sababu ni nyingi sana na hazina yetu ni ya pili duniani kwa uwingi. Wao wanataka umeme ufuliwe kule kule kwa sababu utaleta mapinduzi ya maendeleo kule. 2. Faida ya pili ni kwamba nyaya zitakazo zoubeba umeme kuupeleka mpaka Kenya na Uganda tukitaka, lazima njia nzima zitakuwepo transfoma za kuusambaza mpaka miisho yote ya nchi mpaka vitongoji vyote. Kwahiyo wananchi wa Kusini ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 3. Wanataka mabomba ya gesi yaanze kuisafirisha baada ya kufuliwa umeme, ili na yenyewe pia humo njiani yachomekwe mabomba yatakayoieneza nchini kote, kusudi iwe nishati mbadala ya Taifa kwa ajili ya kuiokoa miti yetu kwa ajili ya vizazi vyetu vyote vijavyo. Mungu ametuzibulia hazina ya gesi wakati nchi yetu inaelekea kuwa jangwa kutokana na kuteketezwa miti yote kwa kutumiwa kama nishati. Hawa ndio wazalendo na siyo watawala wa CCM. 4. Ukweli kwamba ufisadi wa kutisha umetembea katika mikakati hiyo ya kuufulia hapa Jijini umeme wa gesi ya Kusini, hivyo kwamba kiburi cha watawala na kutojali maslahi ya Taifa kama umeme utafuliwa kule kule Kusini, ni kwa sababu mafisadi hawana jinsi kwavile mabilioni ya watu walishakula sehemu kubwa, na sasa wanatafuta kulazimisha ili wapate lile fungu nono la mwisho. Saa ya ukombozi ni sasa! Njia pekee ya kuzimisha moto huu kule Kusini na kurejesha amani ni Rais Jakaya Kikwete kutoa Tamko la kukubali kufuliwa umeme kule kule Kusini kwa sababu ni kwa maslahi ya Taifa. DP tupo tayari kufanya usuluhishi kama kutakuwepo uwazi kwa upade wa serikali, kwa ajili ya hatima ya Nchi yetu. Rais Jakaya Kikwete analazimika pia kutamka bayana kipaumbele kwa ubereshaji wa Bandari kuu ya Mtwara, ikibidi hata kwa kusitisha mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Hii ni kwa maslahi ya Taifa letu. Rais Jakaya Kikwete anapaswa kutamka bayana kuhusu ukamilishaji wa barabara ya Kusini.Rais Kikwete anakabiliwa na utanguaji wa ufisadi wote uliofanyika Mtwara Corridor mpaka Ludewa kwenye miradi ya Chuma cha Liganga na Mkaa wa mawe Mchuchuma. Saa ya ukombozi ni sasa! Mchungaji C. Mtikila, Mwenyekiti0713 430516
No comments:
Post a Comment