Thursday, December 27, 2012

Mnyika: Bila wanasheria makini tungevuliwa ubunge

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kama kisingekuwa na wanasheria wenye uwezo na umakini wa kusimamia sheria, wabunge wao wangevuliwa ubunge kwa kufunguliwa kesi za ajabu na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hiyo, imetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati akichambua taarifa ya Naibu Katibu wa CCM, Mwigulu Nchemba, aliyetangaza mwaka 2013, chama hicho kitategemea nguvu ya Mungu kufanikisha mikakati yao ya kuwatumikia wananchi.

“Kabla ya yote, nianze kwa kauli yao juu ya hukumu ya Godbles Lema, iliyotolewa Mahakama ya Rufaa Tanzania, ambapo walisema ni dalili tosha kwa CCM kuheshimu misingi ya sheria na utawala bora, jambo hilo si kweli bali ni kujikosha na unafiki wao.

“Kama kweli, wanaheshimu misingi ya sheria na utawala bora wanapaswa kukumbuka waliofungua kesi kule Arusha ni mamluki wa CCM ambao walipata baraka zote kuanzia kwa mbunge na chama, sasa iweje wanajikosha kwamba chama kina demokrasia.

“Tuliwahi kuilalamikia Ikulu kuingilia masuala mbalimbali, ikiwamo kesi ya Lema, lakini cha ajabu CCM ndiyo iliyokuwa ikijitokeza kujibu, sasa watuambie kwa nini wanasheria wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, walitoa ushindi kwa wale wanachama wao, huku Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, ikitoa ushindi kwa Lema.

“CHADEMA mara zote, tunasema kama tusingekuwa na wanasheria wenye uwezo na umakini katika kuichambua sheria ya Tanzania, basi wabunge wetu nikiwamo mimi tungevuliwa ubunge kwa kufunguliwa kesi za ajabu tena za kusingizia zisizo na vielelezo na hata Lema asingerudishwa bungeni,” alisema Mnyika.

Alisema kitendo cha CCM kuibuka na kauli ya kutegemea nguvu za Mungu, baada ya CHADEMA kutoa kauli yao, ni kutaka kujaribu kuwalaghai Watanzania wasiamini Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), pamoja na kauli yao ya mwaka 2013 ya kutumia nguvu ya umma kuisimamia Serikali ili kutekeleza hoja za msingi za wananchi.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo mwaka 2013, Mnyika alisema CCM haiwezi kuleta maendeleo wala kutekeleza ahadi zao kwa miaka iliyobaki kufika 2015 na kuongeza kuwa, kama wameshindwa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania ndani ya miaka 7 itakuwezaje kwa miaka mitatu.

“Ilani yao ya mwaka 2005, ilisema maisha bora kwa kila Mtanzania na mwaka 2010 wakarudia tena, hebu fikiria CCM wanaibuka wanasema wanategemea nguvu ya Mungu kukamilisha miradi ya maendeleo, niwaombe wasilitaje jina la Mungu kwani wanamkosea.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment