Saturday, December 22, 2012

Godbless Lema


 MAHAKAMA YAMREJESHEA UBUNGE WAKE
MAHAKAMA ya Rufaa nchini jana ilitengua uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wa kumvua ubunge, Godbless Lema (CHADEMA), na kumtangaza kuwa mbunge halali.
Hukumu hiyo iliamsha shangwe kubwa kutoka kwa mamia ya watu walioanza kujikusanya katika viunga vya mahakama hiyo tangu saa moja asubuhi, na kufuatia maandamano ya amani kuelekea yaliko makao makuu ya CHADEMA, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Rufaa ilijiekeleza katika hoja za msingi zilizokuwa zikibishaniwa mbele ya jopo la majaji watatu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo, lililoundwa na Salum Massati, Bernard Luanda na kiongozi wao, Natalia Kimaro.
Lema alivuliwa ubunge Aprili 5, 2012 katika hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalira, kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kutokana na hukumu hiyo, Lema, kupitia kwa mawakili wake, Method Kimomogoro, na Tundu Lissu alikata rufaa Mahakama ya Rufaa, akiwasilisha hoja 18 za kuipinga.
Mawakili wa Lema walidai mahakamani hapo kuwa, Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya katika hukumu yake alivyosema kuwa kesi za uchaguzi hazitawaliwi na kanuni za sheria za Uingereza kwani kuna maamuzi ya kesi mbalimbali yaliyokwishatolewa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu nchini na kuruhusu kesi za uchaguzi ziamuliwe kwa kutumia kanuni na sheria za Uingereza.
Katika hoja ya pili, mawakili hao walidai kuwa Jaji Rwakibalila alijielekeza vibaya kuruhusu wajibu rufaa, wasitaje maneno kwenye hati ya madai ambayo walidai ni ya udhalilishaji wa kijinsia na dini ambayo yanadaiwa kutolewa na Lema, kwenye mikutano ya kampeni dhidi ya Dk. Batilda Burian.
Hoja nyingine ni kwamba, hakuna ushahidi wowote unaoonesha kwamba wajibu rufaa kama kweli waliandikishwa kupiga kura katika Jimbo la Arusha Mjini mwaka 2010 au la.
Kwa mujibu wa wakili huyo, hoja nyingine ni kwamba Jaji Rwakibalila alikosea kisheria kusema kuwa mtu yeyote akiwemo mpiga kura ana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo ambalo yeye ni mpiga kura na kuongeza kuwa, wao wanaomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa wajibu rufaa (wapiga kura wa Jimbo la Arusha waliofungua kesi ile), hawana haki kisheria kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Lema kwani mwenye haki ya kufanya hivyo ni Dk. Batilda mwenyewe.
Mawakili hao waliongeza kuwa, mpiga kura yeyote hana haki ya kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Arusha Mjini kwani haki zao hazikuvunjwa.
Alidai kuwa maamuzi ya Mahakama ya Rufaa katika kesi zile yalisisitiza kuwa lazima kesi ithibitishwe bila kuacha shaka yoyote, lakini katika hukumu ya Jaji Rwakibalila imeacha shaka kubwa.
“Kwa hoja hizo tulizoziwasilisha hapo juu, tunaiomba Mahakama ya Rufani nchini itengue hukumu ya Jaji Rwakibalila kwani haina vigezo wala hadhi ya kuifanya iwe hukumu, na pia tunaiomba mahakama iwaamuru wajibu rufaa walipe gharama za uendeshaji wa kesi hiyo tangu ilipoanza Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na sasa Mahakama ya Rufaa,” alidai wakili Kimomogoro.
Arusha yalipuka
Shangwe na nderemo zilitawala karibu nchi nzima likiwamo Jiji la Arusha na vitongoji vyake jana baada ya kupokea taarifa za ushindi wa rufaa ya Lema.
Mara baada ya habari za uamuzi wa jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, kutangazwa na Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) kwamba umerejesha ubunge wa Lema, mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha walijimwaga barabarani na kushangilia kwa nguvu ushindi huo.
Honi za magari na pikipiki zilizokuwa barabarani zilisikika kwa nguvu na kutawala anga kwa muda mrefu, na kuungwa mkono na wananchi wengi waliofanya maandamano yasiyo rasmi katika mitaa mingi ya Jiji la Arusha.
Shamrashamra hizo zilianzia majira ya saa nne asubuhi ambapo wananchi wengi walianza kukusanyika katika matawi mbalimbali ya chama hicho na kuanza kushangilia huku wakipandisha bendera kila kona.
Magari mengi yaliyokuwa yakitembea mjini humo, yalipambwa kwa bendera za CHADEMA hivyo kuongeza hamasa kwa wanachama wake.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi lililazimika kuimarisha doria kila kona kwa magari yaliyokuwa na askari yakizunguka katika mitaa kadhaa ya jiji hilo kuhakikisha hakutokei uvunjifu wa amani.
Watu hao waliokuwa wakipeperusha bendera ya CHADEMA na kila alama inayotambulisha chama hicho kikuu cha upinzani walisikika wakimsifu Lema na viongozi wa CHADEMA kwa kusimama kidete kutetea haki za wanyonge dhidi ya dhuluma za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Dar es Salaam alikokwenda kusikiliza hukumu hiyo ya kihistoria, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alisema yeye na chama chake wamepokea kwa furaha hukumu hiyo waliyoitarajia kutokana na hoja za kisheria zilizotolewa na nawakili wa Lema, Kimomogoro na Lissu.
“Uamuzi huu umethibitisha kuwa Mahakama ya Rufaa ni chombo huru kinachosimamia maadili na sheria. Pamoja na udhaifu uliotokea katika mahakama ya chini, lakini tulikuwa na uhakika wa ushindi kutokana na makosa ya kisheria yaliyofanywa na jaji katika kumvua Lema ubunge,” alisema Golugwa.
Hata hivyo, katibu huyo alisema ushindi wa jana ni hatua moja katika changamoto ya kutekeleza sera na ahadi za CHADEMA kwa wakazi wa Arusha baada ya kupoteza muda mwingi kukabiliana na kesi hiyo iliyomfanya mbunge huyo kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wapiga kura.
“Pamoja na kesi mbalimbali zinazomkabili mahakamani, mbunge wetu alikosa utulivu wa kuwatumikia wananchi kutokana na kulazimika kuhudhuria mahakamani mara kwa mara kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wake,” alisema Golugwa.
Lissu: Ni ushindi wa kihistoria
Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Wakili wa Lema, Lissu alisema kuwa anatamani ingetolewa miaka kumi iliyopita kwani imekuwa ni ya kihistoria kwa kuwa inawafundisha wale wote wanaohongwa na wagombea wa CCM.
Alisisitiza kwamba, utaratibu mbovu wa wapiga kura kufungua kesi kupinga kwa niaba ya wagombea, uliokuwa unafadhiliwa na CCM umeanza tangu mwaka 1995, ambapo Dk. Willibrod Slaa alipingwa na wapiga kura Karatu, na Makongoro Nyerere alipingwa Arusha Mjini, mwaka 2000.
Aliongeza kuwa, wapiga kura hao hao walimpinga Freeman Mbowe katika Jimbo la Hai 2005, marehemu Chacha Wangwe, Philemon Ndesamburo nao walitendewa hivyo hivyo.
Lissu alisikitikia kitendo cha wagombea wa CCM kuwadhalilisha wapiga kura kufungua kesi mahakamani, kwani hawana hata uwezo wa kujikimu wenyewe kwa mahitaji ya kawaida, lakini wanakuwa na uwezo wa kuwa na timu za mawakili wawili wawili kwenye kesi.
“Uamuzi huu ungetolewa miaka kumi iliyopita tungeokoa uchumi kwa kuacha kuendesha kesi ambazo hazina tija kwa uchumi wa taifa, kulipa majaji kwa kesi ambazo hazikuwepo. Wapiga kura wanayo haki ya kushtaki ikiwa tu haki zao za kujiandikisha, kupiga kura au kuhesabiwa zimekiukwa. Nje ya hapo tunakandamiza demokrasia,” alisema.
Naye Wakili Kimomogoro alisema hukumu hiyo imerudisha heshima ya mahakama machoni mwa wananchi ambayo katika siku za hivi karibuni ilianza kufifia kutokana na namna ilivyokuwa ikifanya maamuzi huku akitolea mfano wa uamuzi uliotolewa kwenye kesi ya mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa UDP, Mchungaji, Christopher Mtikila.
Wakili huyo aliupongeza uamuzi huo wa majaji wa Mahakama ya Rufaa aliouita ni uamuzi mgumu hasa kutokana na kauli mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa serikali akiwemo Rais Jakaya Kikwete zilizokuwa zikionyesha kuunga mkono hukumu ya awali.
Habari zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zimesema kuwa Lema anatarajiwa kupokewa kwa shangwe atakapowasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.




Ndugu ukoo wa Lissu walivyoumana kortini


Pichani kutoka kushoto mbele Alute Mughway, Godbless Lema na Tundu Lisu

MIONGONI mwa mambo yatakayokumbukwa katika kesi iliyotengua na baadaye kumrejeshea ubunge, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ni mawakili wa pande mbili zilizokuwa zikipambana katika kesi hiyo ya kuhistoria.

Kwanza ni mawakili ndugu; Tundu Lissu ambaye alikuwa akimtetea Lema na Alute Mughway ambaye alikuwa wakili wa makada wa CCM waliofungua kesi kupinga ushindi wa Lema.

Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakili mwenzake, Method Kimomogolo walishirikiana kumtetea Lema ambaye ni kada wa Chadema.

Lakini kaka yake (Mughway) alikuwa anawatetea warufaniwa (wajibu rufaa) ambao ni makada wa CCM; Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.

Alute na Tundu wote ni watoto wa Mzee Augustino Lissu Mughwai na Bibi Alu Alute Tundu ambao wote sasa marehemu. Wakati Alute ni mzaliwa wa pili katika familia hiyo ya watoto 12, Tundu ni mzaliwa wa tano.

Alute hivi sasa ni wakili wa kujitegemea akifanyika kazi zake mkoani Arusha wakati mdogo wake Tundu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki ni wakili akifanyia kazi zake jijini Dar es Salaam.

Ndugu hawa walikuwa kivutio katika kesi hiyo kwani wote walionekana kuwa mahiri katika kujenga na kupangua hoja pale walipokuwa wakiishawishi mahakama kuwapa ushindi wateja wao.

Ndugu hawa wawili wamekuwa wakipambana mahakamani kwenye kesi ya Lema tangu ifunguliwe Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2010.

Hukumu ya kesi hiyo ndiyo iliyomvua ubunge Aprili 5, 2012 lakini Lissu na wakili mwenzake Method Kimomogolo awalikata rufaa ambayo jana ilimrejeshea Lema Ubunge.

Hii inatoa picha kwamba katika fani ya ya sheria hasa kwenye uwakili mahakamani huweza kuwakutanisha maadui kutoka pande mbili, mtu na mwanaye katika pande hizo mbili lakini kila mmoja akisimamia kile anachokiamini ili kufanya kazi yake.

Baba anaweza kuwa upande wa utetezi na mtoto anaweza kuwa upande wa mashtaka, kila mmoja akitaka kuonyesha uwezo wake kwa mteja wake.

Wakati mwingine watu huweza kusema kwa nini huyu asizungumze na mwanaye ili asitoe hoja nzito au mtoto asizungumze na baba yake ili asitoe hoja nzito ili kurahisisha kesi. Lakini hayo hayana nafasi pale watu hawa wanapokuwa katika kazi zao hasa za kitaaluma.

No comments:

Post a Comment