Saturday, December 8, 2012

CCM yamuangukia John Mnyika


Hatimaye nguvu za kisiasa za Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika,  zimedhihirika baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba kuondoa rufaa inahusu ubunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam.

CCM kupitia mawakili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Hawa Ng’humbi, wamemuomba Mnyika, kukubali shauri hilo limalizike nje ya mahakama na kusamehewa gharama za kesi.

Tayari   Ng’humbi alishashindwa katika kesi ya msingi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Mnyika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kutakiwa kulipa gharama za kesi hiyo.

Wakili wa Serikali,  Issa Maige, aliwasilisha hoja ya  kuliondoa shauri hilo  katika Mahakama ya Rafaa Tanzania jana, kwa maelezo kuwa pande mbili zilikubaliana kufikia suluhu bila masharti.

“Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa sheria namba 102(3)( 4 ), rufaa hiyo inaweza kuondolewa kwa kuwa  wote walikubaliana nje ya Mahakama,”alidai Maige.

Hoja hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo jana, mbele ya jopo la majaji watatu, Nathalia Kimaro, Salum Massati na Catherine  Oriyo.

Akitoa uamuzi wakati wa kuliondoa shauri hilo, Jaji Kimario alisema mahahama hiyo ilikubali kutokana na hoja ya wakili wa serikali.

“Kesi imekwisha baada ya pande mbili kukubalina, hivyo Mnyika anaendelea na jukumu lake  la ubunge  na kuwatumikia wananchi,”alisema Jaji Kimario.

Kwa upande wake, Mnyika mara baada ya shauri hilo kuondelewa mahakamani, alisema kuwa walifikia uamuzi huo baada ya wakili wa mlalamikaji kukutana na wakili wake na  kumshauri wamalize shauri hilo nje ya mahakama.

“Mimi ni binadamu nikaona tumsamehe, lakini gharama za kesi ya hukumu ya Mahakama Kuu itakuwa pale pale,”alisema Mnyika.

Alisema hawezi kuzungumzia gharama halisi  kwa sasa hadi  watakapokaa na wakili wake, gharama sahihi hazikuweza kupatikana kwa kuwa walifahamu kesi inaendelea.

Mnyika alisema kuwa kwa kipindi chote cha miaka miwili alikuwa akiwawakilisha wananchi  bungeni huku akiwa na kesi mahakamani bila ya kukata tamaa, kasi hiyo itaongezeka  zaidi kwa kuwa kesi imemalizika na kuibuka  mshindi.

Alisema kwa kuanzia atafanya mkutano katiika eneo la Manzese, kujadili matatizo ya kiwanda cha nguo cha Urafiki yaliyosababisha ukosefu wa ajira  wananchi hususan vijana.

NG’HUMBI AKANA KUKATA RUFAA


Akizungumza na NIPASHE Jumamosi kuhusu uamuzi huo, Ng’humbi, alikana kuhusika na kukata rufaa hiyo dhidi ya Mnyika, akisema ni hatua iliyofikiwa na CCM mkoa wa Dar es Salaam.

“Mimi sikukata rufaa na ndio maana hamkuona nikilifuatilia suala hilo kwa karibu, nilichokifanya ni kutoa taarifa ofisi za mkoa, sasa labda muulizeni Katibu wa chama (CCM) mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.

Ng’humbi alisema anachokitambua binafsi ni uamuzi wa kuhalalisha ubunge wa Mnyika uliofikiwa na Mahakama Kuu, huku akisisitiza kuwa unapaswa kuheshimiwa.

CCM MKOA YAMSHANGAA

Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Said Mihewa, alielezea kushangazwa na kauli ya Ng’humbi, huku akionyesha kutoamini kama imetoka kwake (Ng’humbi).

“Unasema Ng’humbi ndio katamka maneno hayo ama huko mahakamani, kwa maana mimi nipo ofisini hapa,” alihoji.

Mihewa alisema kimsingi sheria inampa uhuru aliyekuwa mgombea ama mpira kura kufungua shauri mahakamani na si chama cha siasa.

Alisema CCM mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa inapata taarifa zinazohusu shauri hilo mahakamani kwa vile jimbo la Ubungo lipo mkoani humo.

Pia alisema katika utaratibu wa CCM, ofisi za mkoa hazihusiki moja kwa moja na mashauri yanayohusu ubunge, hivyo huenda suala la Ng’umbi likaigusa ngazi ya taifa.

Jitihada za kuwapata Katibu Mkuu ama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,  Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye, hazikufanikiwa.

MNYIKA AANGUA KICHEKO

Lakini Mnyika akiizungumzia kauli ya Ng’umbi, alisema taarifa alizozipata kwa mawakili zake siku mbili kabla ya jana, ni kuhusu kuwepo hoja iliyowakilishwa na mawakili wa aliyekuwa mgombea ubunge huyo.

“Anasema yeye ahusiki na rufaa (anacheka)…kwa vile mahakama ilishanitangaza mshindi hilo si la msingi kwangu bali kurejea kuwatumikia wananchi wa Ubungo,” Mnyika alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment