MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhani Dau, kutokuwa katibu wa kamati ya ukaguzi wa hesabu za ndani wa shirika hilo.
Zitto alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salam wakati watendaji wa shirika hilo walipokuwa katika mahojiano na kamati hiyo na kushauri kutafutwa mtu mwingine awe katibu wa kamati hiyo.
“Nafikiri yalikuwa yanafanyika makosa makubwa, mkurugenzi mkuu kuchukua nafasi ya katibu wa kamati ya hesabu za ndani na kujikagua mwenyewe … sasa ninaagiza kwamba aondoke ichukuliwe na mfanyakazi mwingine,” alisema Zitto.
Zitto alisema hakuna sheria na si haki kwa kiongozi yeyote kutumia nafasi yake au kuchaguliwa kujichunguza, bali kazi hiyo inapaswa kufanywa na wafanyakazi wengine.
Katika hatua nyingine, Zitto aliitaka NSSF kuielimisha jamii na kuboresha huduma ya mafao ya bima ya afya ambayo yalianza miaka michache iliyopita.
Aliwataka kuwatumia wasanii kuzunguka nchi nzima kutoa elimu ya namna ya kujiunga na kueleza namna mafao ya afya yanavyotolewa.
Pia, Zitto aliitaka NSSF kuangalia namna ya kutengeneza kadi za wanachama tegemezi (watoto), ili kuondoa usumbufu unaojitokeza pale wanapotaka kupatiwa matibabu.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment