Sunday, October 28, 2012

Mnyika ashtukia ahadi tata ya serikali


KATIKA hali ya kushangaza, serikali imeahidi kufikisha huduma ya maji katika vyoo vya Shule ya Msingi Kilungule ‘B’, Kata ya Kimara, Dar es Salaam, wakati kijiografia eneo hilo linakabiliwa na tatizo sugu la huduma hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, alisema kuwa ameshangazwa na kauli hiyo ya serikali, kwa sababu imeahidi kufikisha huduma hiyo katika vyoo vya shule wakati wakazi wa Kimara kwa ujumla wanakabiliwa na tatizo sugu la huduma hiyo.
Mnyika alionesha shaka ahadi hiyo kutekelezwa kutokana na kile alichosema asilimia 80 ya wakazi wa Kimara wanakabiliwa na tatizo la huduma hiyo hadi sasa.
Alisema, licha ya shule hiyo kukabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya ukosefu wa huduma hiyo hususan katika maeneo muhimu kama chooni, serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO), imefanikiwa kujenga kisima cha maji kilichopo hatua chache kutoka eneo la shule.
Alifafanua kuwa, awali Dawasco iliwataka wakazi wa eneo hilo kuchangishana fedha sh mil. 13 kwa ajili ya kufikishiwa huduma hiyo katika eneo hilo.
Katika hilo, alisema kati ya wakazi zaidi ya 92 walijiorodhesha kwenye mradi wa maji wa Dawacso, badala yake kaya 15 tu ndizo zilizolipia, ambapo walifungiwa mabomba na kwa sasa wananufaika na huduma hiyo.
“Jambo la kusikitisha huduma ya maji iliyopo eneo hili haikidhi mahitaji ya wananchi kwa sababu ni maji chumvi, jambo ambalo limewalazimu wengi wao kununua huduma hiyo kutoka kwenye magari yanayohusika na utoaji wa huduma hiyo,” alisema Mnyika.
Eneo hilo hadi sasa, lina visima vya maji 20 kati ya 27, vilivyoahidiwa na vimejengwa na Shirika la Maji Safi na Maji Taka (Dawasa) kwa kushirikiana na serikali.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment