Tuesday, October 2, 2012

Hatima rufani ya Lema kujulikana leo


MAMIA ya wakazi wa Arusha, leo wanatarajiwa kujitokeza tena viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kujua hatima ya rufani ya kupinga kuvuliwa ubunge,  Godbless Lema (Chadema) huku kivutio kikitarajiwa kuwa mawakili ndugu, pande mbili tofauti kwenye rufani hiyo.

Mawakili hao, Tundu Lissu ambaye ameongezwa kumwakilisha, Lema na kaka yake na Alute Mughwai anayewakilisha makada wa CCM waliopinga ushindi wa Lema.

Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande akiwaongoza wenzake, Salum Masati na Natalia Kimaro,  waliahirisha kuanza kusikiliza rufani hiyo kufuatia  kifo cha baba mzazi wa mawakili hao.

Wakili Modest Akida wa upande wa walalamikiwa, aliomba Mahakama ya Rufani kuahirisha kusikilizwa rufani hiyo wiki iliyopita, kutokana na kifo hicho ambacho kilitokea Septemba 16. Tayari mazishi yamefanyika mkoani Singida  Septemba 22, mwaka huu.

Hoja hiyo ya kuomba kuahirisha usikilizwaji rufani hiyo hadi leo, iliungwa mkono na wakili mwingine wa upande wa mrufani, Method Kimomogoro na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Vitalis Timoth anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu (AG).
Hata hivyo, Jaji Chande alisema ili kuhakikisha rufani hiyo inasikilizwa kwa wakati, alitaka upande wa mlalamikiwa kupeleka mahakamani pingamizi la hoja kuhusu rufani hiyo kabla ya Septemba 26, mwaka huu na upande wa mrufani kujibu kabla ya  Septemba 28 sambamba na AG.
Mawakili wa pande zote, jana walithibitisha kukamilisha taratibu za kujibu hoja, Wakili Lissu aliwataka wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani kuendelea kufika mahakamani ili kujua hatima ya kesi hiyo.
“Nawaomba kesho (leo) mje kwa wingi mahakamani kama ilivyo kawaida yenu, ili msikilize rufani ya mbunge wenu Godbless Lema,” alisema Lissu.
Hata hivyo, baada ya leo kusikilizwa hoja za pande zote na kama rufani hiyo ikiendelea, shauri la msingi la kupinga hukumu ya Jaji  Gabriel Rwakibarila  kumvua ubunge Lema  itahamishiwa Dar es Salaam kutokana na kukamilika mkoani Arusha vikao vya mahakama ya rufani.

Katika rufani hiyo, Mawakili wa Lema wamewasilisha hoja 18 za kupinga kuvuliwa ubunge Lema, kutokana na hukumu ya Jaji Rwakibarila ya Aprili 4, mwaka huu kukubaliana na hoja za walalamikaji, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo kuwa Lema alitoa maneno ya kumdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda-Salha Burian.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment