Tuesday, October 9, 2012

CHADEMA yazindua kampeni za udiwani


UMATI mkubwa wa watu, juzi ulijitokeza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani wa kata ya Daraja Mbili wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Prosper Msofe, uliofanyika kwenye mtaa wa Narvoi.
Aidha, viongozi wa chama hicho wakizungumza katika mkutano huo mbali ya kumuombea kura mgombea wao huyo, walitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa jiji la Arusha kuacha kufuata shinikizo la kisiasa katika kutafutia ufumbuzi suala la wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama machinga kwa madai kuwa suala hilo ni kama bomu la muda linalosubiri kulipuka.
Pia waliitaka serikali kutoa majibu yanayoeleweka juu ya tukio la kutoroka kwa washtakiwa wawili wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA, kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, kwa madai kuwa kuna uwezekano nyuma ya mpango huo, kukawa na mkono wa wanasiasa ambao hawataki ukweli ujulikane.
Mwenyekiti wa wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro alisema inashangaza kuona halmashauri ya jiji la Arusha inaamua kuendesha shughuli zake kijima kwa kuamua kugawa uwanja wa NMC.
Nanyaro ambaye pia ni diwani wa Levelosi, aliuataka uongozi wa jiji la Arusha kushughulikia masuala yote kitaalamu kuepuka kuibua migogoro isiyo ya lazima kama ilivyo sasa ambapo licha ya machinga kupewa eneo lisilotosheleza kwenye uwanja wa NMC, lakini idadi ya waliokosa ni kubwa hivyo badala ya tatizo kupungua limeendelea kuongezeka.
Kwa upande wake, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema serikali isifanyie mzaha suala la watuhumiwa hao kutoroka, kwani lina utata mkubwa na pia linaacha maswali mengi kuliko majibu.
Kampeni hizo zinatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, mwaka huu ambapo zinawashirikisha wagombea kutoka vyama vya CCM na TLP.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment