CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mvomero, kimezindua kampeni ya udiwani wa Kata ya Mtibwa kwa ahadi mbalimbali ikiwemo kudai chenji ya fedha za mfuko wa jimbo kwa Naibu Waziri wa Utamaduni na Michezo na Mbunge wa jimbo hilo, Amos Makala, zinazodaiwa kutofanya kazi tangu mwaka 2010.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye uwanja wa Kambombe Madizini B, ulihudhuliwa na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mkoa na wilaya za jirani, ulizinduliwa na Mwenyekiti wa Madiwani wa chama hicho mkoani hapa ambaye pia ni diwani wa Gairo, Dastan Mwendi.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mwendi alisema: “Uoga na vitisho vya nguvu za dola ikiwemo kuua kwa makusudi raia nchini umetufikisha kwenye dimbwi la umasikini wa kutupwa tulio wengi na kuwanufaisha wachache walioko madarakani…wakati tunauawa na watoto kukosa elimu yenye tija inayotokana na kukosa huduma na vifaa wenzenu wananepa. Mchagueni Lucas Mwakambaya,” alisema huku akihoji zilipo fedha za jimbo tangu mwaka 2010”.
Akiwahimiza wapiga kura kumchagua Mwakambaya kuwa diwani wa Kata ya Mtibwa, Mwendi alisema muda wa Watanzania kugeuzwa ‘kuku wa kienyeji’ na kuwa wenye thamani wakati wa matatizo na furaha umepitwa na wakati kwa kuwa sasa wanaelewa haki zao.
Mwenyekiti wa chama hicho wa manispaa, Zuberi Kiloko na Mwenyekiti wa Vijana Mkoa, Boniface Ngonyani, waliungana na hoja hizo kwa nyakati tofauti na kusema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelemewa na uongozi mbovu uliojaa rushwa na uonevu kwa wanachi.
“Chama makini huonekana hata katika uendeshaji wa michakato midogomidogo ya kichama, leo hii CCM inanuka rushwa hadi mwenyekiti wao Jakaya Kikwete amewashitukia na kutoa tamko kali kuwa atakayebainika kutoa rushwa atafutiwa uanachama, hii inatokana na kukithiri kwa rushwa,” alisema Kiloko.
Akijinadi mgombea udiwani wa Mtibwa, Mwakambaya, alitaja changamoto tisa zinazomkosesha usingizi na anazokusudia kuzifuatilia na kuzisimamia kikamilifu ikiwemo ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutosoma taarifa za mapato na matumizi, upotevu wa sh milioni 28 kila mwezi na kutelekezwa kwa mnada miaka nane bila kuboreshwa huduma za kijamii.
Changamoto nyingine ni dhuluma zinazofanywa na kiwanda wa sukari cha Mtibwa ikiwemo ya kutolipa mafao ya wastaafu kwa miaka minane na fidia kwa waliohamishwa kupisha Sekondari ya Mtibwa, tatizo la ukosefu wa zahanati, soko, kuifuta michango isiyo na tija na kuikagua upya miradi yote iliyopo katani hapo.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment