Friday, October 12, 2012
CHADEMA kujadili ripoti za Mwangosi
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kinakusudia kufikisha ripoti za kamati mbalimbali zilizochunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha television cha Chanel Ten katika kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.
Hata hivyo, mbali ya hatua hiyo, chama hicho kimesisitiza kuwa ni wakati muafaka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emanuel Nchimbi, kuachia nafasi au awajibishwe na Rais Jakaya Kikwete, kutokana na kutumia fedha za wananchi kwa kamati waliyodai haikuwa na jipya juu ya mauaji ya Mwangosi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Vicent Nyerere, alisema wao kama chama wameona watoe tamko la awali wakati wakisubiri majumuisho ya pamoja kwa ajili ya hatua zaidi.
“Serikali toka awali haikuwa na nia ya kuonesha upungufu uliosababisha kifo cha Mwangosi, na kwa kutambua hili Nchimbi aliunda kamati yenye lengo la kuisafisha jeshi la Polisi kwa kutumia kodi zetu,”alisema.
Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini, aliongeza kuwa ni jambo la ajabu kwa mtu kama Nchimbi kukubali kupokea ripoti ya ajabu na yenye kumdhalilisha kisha akasimama hadharani kuitetea.
Alisema ni wakati muafaka kwa Rais Kikwete kumfuta kazi Dk. Nchimbi kwa kuwa ameshindwa kujitathmini kutokana na mauaji yanayotokea sehemu mbalimbali hasa katika matukio ya kisiasa ili liwe fundisho kwa viongozi wengine katika kusimamia majukumu na maslahi ya Taifa.
Nyerere alibainisha kuwa namna kamati ya Dk. Nchimbi ilivyofanya kazi, imeshindwa kuwaelewesha watanzania kiini cha kifo hicho licha ya kutumia kodi zao, hivyo kushauri kuwa inapaswa kuundwa tume ya kimahakama.
Kuhusu maoni ya kamati ya Dk. Nchimbi juu ya shughuli za kisiasa kuishia bungeni baada ya uchaguzi, Nyerere alisema ni jambo la kushangaza kama leo Bunge litakuwa sehemu ya kunadi sera badala ya kuzungumzia matatizo ya wananchi.
“Kama kamati iliyo chini ya Jaji Ihema ndiyo imekuja na mtazamo huu wa kutaka shughuli za kisiasa na mijadala yake ifanyikie bungeni basi ninasisitiza kauli ya Tundu Lissu juu ya kumpinga Jaji huyu mstaafu ni muhimu zaidi,”aliongeza Nyerere.
Alisema ripoti ya kamati ya Nchimbi ingeweza kutoa taarifa zote hadharani bila kuingilia uhuru wa mahakama na kwamba alitaraji kuona ikiwagusa viongozi wa serikali moja kwa moja wanaoingilia shughuli za vyama vya siasa.
Kamati tatu tofauti zimetoa ripoti zake kuhusiana na mauji ya Mwangozi ambapo ile ya Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri pamoja na ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, zimeeleza wazi kiini cha mauji hayo na kuwataja waliohusika.
Hata hivyo ripoti ya kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi ililalamikiwa kutokana na kushindwa kuweka taarifa kamili wazi kwa madai kuwa kesi ya mauaji hayo iko mahakamani.
Tanzania Daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment