Tuesday, September 18, 2012

Waliotimuliwa CHADEMA waomba radhi


MADIWANI wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliotimuliwa kwa tuhuma za kukiuka taratibu za chama na kuingia muafaka wa kumaliza mgogoro wa umeya jijini Arusha wameuomba msamaha uongozi wa juu wa chama hicho.
Madiwani hao ni Ruben Ngowi wa Themi na Rehema Mohamed wa Viti Maalum ambao wameandika barua wakieleza namna walivyoamua baada ya kutafakari na kujiridhisha kwamba walikikosea chama chao.
Madiwani hao ni kati ya watano wa chama hicho waliotimuliwa mapema mwaka huu baada ya kukubali muafaka wa kumaliza mgogoro wa umeya na kugawana madaraka.
Madiwani wengine waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni aliyekuwa Naibu Meya Estomih Mallah (Kimandolu), John Bayo (Elerai) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Uamuzi wa madiwani hao umekuja baada ya juhudi za kumaliza suala lao kupitia vikao vya chama kushindikana hali iliyoilazimu Kamati Kuu ya chama hicho kuwafukuza.
Baada ya kufukuzwa madiwani wote hao walikimbilia mahakamani na kugonga mwamba pale Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha kuitupa kesi yao kabla ya kufungua shauri jingine Mahakama Kuu ambalo hivi karibuni walilitoa mahakamani hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima madiwani hao walikiri kuandika barua hizo ambapo Ngowi alisema haoni sababu ya kuendelea kulumbano na viongozi wa chama anachokipenda hivyo uamuzi wa kuomba radhi ni kutaka arudi kwenye chama.
Kwa upande wake Rehema hakutaka kueleza kwa kina sababu za kuomba radhi kwa madai kwamba yuko kwenye msiba.
“Kwa vile mimi nilijiunga na CHADEMA mwenyewe kwa ridhaa yangu na bila kushawishiwa na mtu ni mapenzi yangu mwenyewe ndiyo maana leo ninaomba radhi nirejeshewe uanachama wangu… sio kikundi.
“Ninaamini kila mmoja anaweza kuwa na makosa yake au upungufu wake hivyo baba Katibu Mkuu na viongozi wangu ninaomba msamaha na niko tayari kufuata yale yote mtakayonielekeza,” ilieleza sehemu ya barua iliyosainiwa na Rehema ambayo gazeti hili limefanikiwa kuiona nakala yake.
Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa alikiri kupokea barua hizo na kusema mamlaka yenye uwezo wa kuwasamehe madiwani hao ni Kamati Kuu kwa vile ndiyo iliyowafutia uanachama wao.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment