Thursday, September 20, 2012

Viongozi wa Chadema Meatu washambuliwa


Viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, juzi walipata wakati mgumu kwa gari lao kushambuliwa kwa mawe na bendera zilizokuwa zkipeperushwa katika gari hilo  kunyofolewa na kutupwa kusikojulikana.

Tukio hilo lilitokea Septemba 17 majira ya saa 10 jioni katika kijiji cha Mwandoya, wakati viongozi hao wakiwa wanaelekea katika mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), aliyekuwa amewaalika kushiriki katika mkutano wake.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa gari la viongozi hao wa Chadema aina ya Nissan Patrol lilishambuliwa na wananchi wanaodaiwa kuwa wafuasi wa  CCM  wakiwemo baadhi ya viongozi wa  chama hicho wa wilaya ya Meatu.

Kiongozi wa msafara wa viongozi wa Chadema Joshua Mgema aliwaambia waandishi wa habari kuwa, gari lao likielekea kushiriki maandamano ya Mbunge wa Kisesa yaliyokuwa yameanza muda mfupi baada ya kukabidhi msaada wa vifaa katika kituo cha afya Mwandoya kuelekea uwanja wa mkutano, lilishambuliwa kwa mawe na kusababisha ufa mkubwa katika kioo cha mbele ya gari hilo.

Viongozi wa Chadema waliokuwa katika gari hilo lilokuwa likiendeshwa na dereva James Daud  ni Zacharia Magembe ambaye Mlezi wa Chadema wilaya ya Meatu, Jackson Kimwaga Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Meatu, Hadija Kidati Mwenyekiti wa Wanawake wa Chadema Wilaya ya Meatu na Joseph Lutoja Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Meatu.

Akizungumzia tukio hilo, Mpina alisema amesikitishwa na kitendo hicho na amelaani tabia ya vurugu na kusema kuwa viongozi hao walikuwa ni miongoni mwa wageni waalikwa kushiriki katika mkutano wa mapokezi yake kurudi jimboni baada ya kumaliza kikao cha Bunge la  bajeti ya 2012/13.

“Hizo ni sisa za zamani, nimesikitishwa sana na kitendo hicho, mimi ni mbunge wa wananchi wote na sio chama fulani licha ya kuwa ni wa CCM, lakini ikumbukwe kuwa ugeni wa viongozi wa kambi ya upinzani ni faraja kwa chama cha Mapinduzi na nikuonyesha kukomaa kisiasa na siyo vurugu” alisema Mpina.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Salumu Msangi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na tayari viongozi wa Chadema wameripoti tukio hilo polisi na hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment