Wednesday, September 12, 2012

Uchaguzi mdogo wanukia Sumbawanga Mjini


Uchaguzi Sumbawanga Mjini, unanukia baada ya muda wa kukata rufani kwa mujibu wa sheria za uchaguzi kupita na upande wa mrufani kugubikwa na ukimya.

Katibu wa CCM (itikadi na uenezi), Nape Nnauye, alipotakiwa kuzungumzia msimamo wa chama kuhusiana na rufani hiyo, alisema aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Aeshi  Hilaly, asingeweza kukata rufani bila kuwasiliana na uongozi.

Nape pia, aliongeza kuwa suala la kukata rufani lilitolewa na Aeshi na sio chama ambapo alimtaka mwandishi wa gazeti hili kuwasiliana na mhusika (Aeshi), iwapo anataka kujua hatma ya kauli hiyo.

“Wewe unauliza, lakini  unajua ni nani aliyetoa kauli ya kukata rufani? Tamko la kukata rufani ilitolewa na yeye au chama? Kuuliza wapi tumefikia, muulize yeye. Yeye asingeweza kukata rufani bila kuwasiliana na uongozi,” alisema Nape.

Aidha Nape, alipohojiwa juu ya hatua iliyofikiwa ya ukusanyaji ushahidi wa tetesi za ufisadi kwa baadhi ya makada wa chama hicho wakiwamo wabunge, unaofanywa na kamati ya maadili ya CCM, alisema kwa sasa hawako kwenye nafasi ya kutoa taarifa ya kamati hiyo.

NIPASHE ilipozungumza na Aeshi jana alisema; “Nimekiachia chama, ni muda mrefu umepita…nasubiri majibu. Mimi si msemaji wa chama, nasubiri kukaa na chama ndipo niweze kueleza, maana hata hivyo siwezi kujua kama wewe kweli ni mwandishi wa NIPASHE au la,” alisema Aeshi.

Kwa upande mwingine, NIPASHE ilimtafuta Naibu Spika, Job Ndugai, kujua kama Bunge limeshapeleka taarifa kwa Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC) kwamba jimbo hilo liko wazi baada ya muda wa kukata rufani kupita kisheria, alisema:

“Tutalitolea maelezo Oktoba kwenye mkutano ujao wa Bunge. Hatuna uhakikika, tunataka kujiridhisha kwanza kwa mahakama ili tuweze kulitolea maelezo suala hilo kwenye Bunge lijalo.”

Aprili 30 mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga ilitangaza kuenguliwa kwa ubunge wa Aeshi (CCM), baada ya kushindwa katika kesi iliyokuwa inamkabili ya ushindi wake uliodaiwa kugubikwa na utata dhidi ya aliyekuwa mgombea mwenzake Norbert Yamsebo (Chadema) katika Jimbo la Sumbawanga Mjini, Oktoba, 2010.

Katika uchaguzi huo, Aeshi alishinda kwa zaidi ya kura 17, 328 dhidi ya Yamsebo aliyepapata kura17,132.

Kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2010 ilifunguliwa na Yamsebo.

Uamuzi wa kutengua matokeo hayo ulitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Bethwell Mmilla, ambaye alisikiliza kesi hiyo na kuisoma kwa takribani saa matatu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment