TAMKO LA CHAMA KUKANUSHA SHUTUMA ZA CHAMA CHA CUF KUFANYIWA VURUGU NA
CHADEMA.
Ndugu
wananchi na wanahabari,
Siku ya terehe 27 Alhamisi Septemba 2012 chama cha
wananchi CUF walitoa taarifa ya malalamiko kwa vyombo vya habari na mitandao
kuwa wanachama wa CHADEMA wamewafanyia vurugu kwa kuwapiga mawe na kuwa jambo
hilo limehamasishwa na viongozi wa chama katika mkoa wa Arusha pamoja na Mhe
Godbless Lema.
Wote tunafahamu kuwa siku hiyo hiyo katika viwanja
vya soko la Kilombero wafanyabiashara ndogo ndogo walikuwa wamevamia na
walikuwa wakijigawia maeneo, baada ya eneo la awali walilopewa la viwanja vya
NMC kushindwa kuwachukua wafanyabiashara wote na halmashauri kushindwa kutoa
majibu kwa wafanyabiashara hawa ambao waliwaambia wote waende NMC.
Kwanza tunapenda kutoa pole kwa viongozi wa CUF kwa
jambo hili lililowapata. Wao kama watu na Watanzania wenzetu tunawapa pole
sana.
Pili, CHADEMA inakanusha kuhusika na jambo hili. Hii
si tabia ya CHADEMA na kamwe haiwezi kuwa tabia ya CHADEMA kufanya siasa chafu
za namna hiyo. CHADEMA tunajali sana amani na upendo, na hii ndiyo tabia na
makuzi yetu Watanzania.
Katika mazingira haya, CHADEMA tunachukua fursa hii
kuvikaribisha vyama vyote mathalani CUF, Arusha ni yetu sote na tutumie
demokrasia vizuri kufanya kazi nzuri ya siasa kwa ajili ya kusababisha na
kuleta matumaini kwa Watanzania hawa ambao serikali ya chama cha mapinduzi
imeshindwa kuwaletea.
CHADEMA hatuna shida na ushindani wa kisiasa katika
mazingira ya kidemokrasia kwa maana ndio wakati pia wa wananchi kupima na kujua
nani mkweli na ama nani anafanya kwa dhati ya kweli. Hivyo tunawakaribisha CUF
karibuni Arusha na wala wasitafute kisingizio cha kuegemea ili CUF ianze
kutajwa tajwa kwa kutumia mgongo wetu.
Sambamba na hili, CHADEMA mkoa wa Arusha
tumesikitishwa sana na tamko la CUF lilitolewa na Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na haki za BInadamu Mhe Abdul Kambaya, tamko lenye matisho na lugha
isiyofaa. Moja na maneno ya tamko hilo wamesema, nukuu “Uwezo wa kuwafanya tutakavyo
tunao na kwa sababu wameanza tunaweza kumaliza”. Wakazi wa Arusha na
Watanzania wapime na waone, haya si maneno yanayoweza kutoka kwenye kichwa cha
mtu anayefikiri vizuri, mtu anayeipenda nchi yake na kuheshimu utawala wa
sheria. Zaidi ya hapo tamko hilo limesema pia, “Ile ngangari kwa polisi
tunaweza kuwahamishia wao wakose pa kukaa”.
Katika yote haya, niwaombe wakazi wa Arusha,
Wanachadema na hata wanachama wa vyama vingine tuwapende na tuwakaribishe CUF
Arusha na sote tufanye kazi ya siasa kwa nguvu za hoja. CUF wanaweza kufanya
hicho wanachotaka kufanya lakini CHADEMA kamwe hatupo tayari kwa vurugu ya aina
yoyote, aidha tunawakaribisha kwa moyo mmoja na kama wapo tayari basi tufanye
siasa zenye tija na manufaa kwa wakazi wa Arusha.
Aidha nitoe onyo kali sana kwa mamluki ambao
wamekuwa wakijifanya kondoo kumbe ndani ni mbwa mwitu. Mara kadhaa watu hawa
wamekuwa wakisababisha fujo ili kukifanya CHADEMA kionekane kuwa ni chama cha
vurugu. MAMLUKI ni sumu, tukimgundua na kumthibitisha mtu wa aina hiyo katikati
yetu tutamtangaza mbele ya jamii kuwa yeye ni sumu na kuomba wananchi wamtenge
maana anapingana kwa kuleta hila na unafiki kwenye kazi ya kuwakomboa
Watanzania. Niwatangazie mamluki hamtatuweza na tutawagundua tu.
Mwisho, tunapoelekea kwenye marudio ya uchaguzi
mdogo kwenye kata za Daraja II kwa Arusha mjini na Bangata kwa wilaya ya
Arumeru Magharibi, nirudie kusema maneno ya Mhe Lema kuwa iwapo viongozi na
watumishi wa umma watajihusisha na kushiriki kwa kufanya kampeni za kisiasa
wakiwa wanatumia magari na vifaa vingine vya serikali watu hawa tutawakamata na
tutawapeleka huko wanakostahili kupelekwa wezi na vibaka wengine. Hii ni
tahadhari tunamaanisha kweli na wananchi wote wawe makini “wakamate mwizi” lengo
likiwa ni kuweka adabu kwa watumishi na viongozi umma wanaovunja sheria ya
utumishi wao kwa umma na matumizi ya rasilimali kwa namna isivyotakiwa
kisheria. CHADEMA tutashiriki chaguzi hizi na tunawaomba wakazi wote wa maeneo
haya tushiriki kwa utulivu na amani.
WANACHADEMA wote tuendelee kuwa majasiri, tusiwe
waoga na tusimamie kweli na haki.
“Hakuna kulala Mpaka Kieleweke”
Amani
Sam Golugwa
KATIBU
WA CHADEMA MKOA WA ARUSHA:
golugwa@gmail.com
No comments:
Post a Comment