Wednesday, September 12, 2012

Polisi anayetuhumiwa kufyatua bomu lililomlipua Daudi Mwangosi apandishwa Mahakamani

HATIMAYE yule askari Polisi, PC Pacificus Cleophas Simon (23) anayedaiwa kufyatua bomu lililomuua kinyama mwandishi Daudi Mwangosi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, amefikishwa mahakamani leo na kusomewa mashitaka ya mauaji.

Askari huyo mwenye namba za kipolisi 2573, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, Lymo na kusomewa mashtaka ya kumwua Mwangosi bila kukusudia, Septemba 2 mwaka huu. 

Mwendesha Mashtaka, Michael Lwena, aliiambia mahakama kuwa upelelezi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea. Mshitakiwa PC Simon hakutakiwa kujibu lolote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji. Hakimu Lymo aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 26 mwaka huu.

Wakati akiingizwa na kutolewa kwenye viwanja vya mahakama, mshitakiwa Simon alikuwa akilindwa vikali na polisi wenzake ambapo kundi la askari zaidi ya saba walimzingira na kuzuia asipigwe picha na waandishi wa habari.

Habari zaidi zinasema, Askari wote walioonekana kwenye ushahidi wa picha wakimshambulia marehemu Mwangosi, walikamatwa.

Marehemu Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 wakati akiripoti tukio la polisi kuwazuia wafuasi wa Chadema waliodaiwa kuandamana kinyume cha sheria kwenye  tukio la ufunguzi wa tawi la chama chao kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa. Mlipuko wa bomu katika tukio lililomuua Mwangosi ulidaiwa pia kumjeruhi vibaya askari polisi anayetajwa kwa jina la Aceli Mwampamba.

Jana, wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam waliandamana kulaani mauaji ya Polisi dhidi ya mwenzao, Mwangosi. Maandamano hayo yalifanyika kuanzia katika kituo cha Channel Ten na kumalizikia kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam. Katika maandamano hayo ya waandishi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi,  alilazimika kuondoka baada ya waandishi 'kumtimua' kwa kudai kwamba hawajamualika. 


WAVUTI

No comments:

Post a Comment