KWA maadili ya vyombo vya habari, magazeti na vingine, ni vigumu kuweka picha ya mwili wa mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyeuawa katika mkutano wa ufunguzi wa tawi la CHADEMA katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa, kwa sababu zinatisha.
Lakini, kwa waliobahatika kupitia mitandao ya kijamii kama facebook na mingineyo ambako picha hizo zimewekwa, huwezi kuamini kama kweli mauaji hayo yanaweza kufanywa na askari wetu walioapa kuwalinda raia na mali zao.
Ukiangalia picha ya mwili wa Mwangosi na mazingira ya kuuawa kwake akiwa amezingirwa na askari wapatao saba, huku mmoja wao akimwelekezea mtutu kummaliza, inatisha na kusikitisha.
Kama sheria za nchi hii inayoimba kuongozwa kwa misingi ya kidemokrasia zingekuwa zinafanya kazi kwa vitendo, kauli za kisiasa zingeepukwa kwenye tukio hili.
Picha zilizopigwa zina majibu yote, viungo vyake vyote vya ndani viko nje, utumbo na kila kitu, kwa hakika inasikitisha!
Inasikitisha kwa jeshi letu ambalo licha ya kuapa kuwalinda raia na mali zao, lakini Mwangosi ameuawa kinyama utafikiri aliyemlalua ni mnyama, kumbe ni binadamu wenzake, tena Watanzania.
Ni tukio la kuumiza na kugadhabisha kwa waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla.
Ukiangalia picha zake jinsi alivyouawa, huwezi kunyamaza kimya, huwezi kuiacha kadhia hii ipite hivi hivi. Najiuliza taifa letu linakwenda wapi?
Kwa vyovyote, katika hili na mazingira ya kifo cha Mwangosi, Jeshi la Polisi linaondoa dhana nzima ya kuitwa walinzi wa raia na mali zao.
Mwangosi ni miongoni mwa watu wachache ambao tukio lake limebahatika kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, lakini leo hii ukiitisha kura ya maoni uwaulize wananchi, ni wangapi wamekutana na kadhia ya polisi na hata kupoteza ndugu zao mithili ya Mwangosi unaweza kupata idadi ya ajabu.
Wapo watu ambao wanawachukia polisi na hawataki hata kuwaona, hawa mioyoni mwao wana vidonda vikubwa ambavyo havijapakwa hata yuso. Ni hatari!
Watu hawa wamepoteza ndugu zao, wapo ambao wamebambikiwa kesi, wengine wameachwa vilema kwa sababu tu ya hila na mioyo ya kishetani ya baadhi ya askari polisi.
Siku moja kiongozi mmoja aliwahi kuniambia kuwa, majeshi yetu yamefundishwa kuua, hayana taaluma ya mahusiano, kila wakati yanafikiri ni vita.
Nilikuwa mgumu kuamini jambo hili, lakini mwananchi au mtu yeyote ambaye amekutana na vitisho vya polisi, atakubaliana na kauli hiyo.
Lakini naona kuna tatizo la msingi katika Jeshi la Polisi la kuingiliwa kwa namna kuu tatu.
Mosi, Jeshi la Polisi limeingiliwa na mamlaka ambayo haitaki kuamini ukweli uliopo.
Ni mamlaka inayotaka kudhibiti sauti na kiu za wananchi kwa njia ya kuwatisha na kuwaogofya.
Kwamba, kwa Jeshi la Polisi kutumia risasi za moto, kutaufanya umma kutodai haki zao za msingi, wanajidanganya.
Namna ya pili ya kuingiliwa, ni vijitabia tabia vya ajabu tu vya baadhi ya polisi wetu ambao wakivaa magwanda yao, basi wanajiona wao ni kila kitu.
Ndani ya magwanda ya upolisi, wanakosa masikio, pia wakijiona wao ni mabwana wakubwa, wanaona nchi hii ni ya kwao peke yao, wengine hawana haki.
Namna ya tatu, kuna baadhi wanaitumia nafasi yao ya upolisi kujineemesha na kupora haki za wengine.
Hawa ni wale wanaotumia nafasi zao kama kitega uchumi, hapa ndipo unapowakuta wala rushwa wakubwa, wasingiziaji ambao wako tayari kuua kwa ahadi nono.
Polisi mmoja mwenye nyota moja ambaye ni mkuu wa kituo kimoja kidogo hapa Dar es Salaam, alinichekesha sana, aliniambia maneno yafuatayo:
“Usinidharau mimi…mimi ni injinia bwana, usinione nimevaa magwanda haya, huku nilikuja kutafuta pesa.”
Kauli yake ilinishangaza sana, imekaa kichwani mwangu siku zote, nikijiuliza maswali lukuki.
Huu ni mfano tu wa baadhi ya makundi niliyoyainisha hapo juu, polisi wa namna hii yuko tayari kusingizia, yuko tayari kuua ili mradi tu ana chake mfukoni.
Katika tukio la kuuawa kwa mwandishi, Mwangosi, ambalo linagusa namna ya kwanza au ya pili nilizozianisha hapo juu, polisi wakumbuke kuwa wamebeba dhamana kubwa ya kulinda raia na mali zao, si kuua wasio na hatia. Wakumbuke viapo na miiko yao.
Binafsi, ninaanza kupata mashaka na mafunzo wanayopatiwa polisi wetu, katika hili sisiti kusema kuwa kuna walakini, kuna mashaka ya kitaaluma!
Pengine ni wakati sasa kwa mkuu wa mafunzo wa jeshi hilo kuwajibika kwanza kabla ya wengine, kwani leo hii askari hawajui mahali na wakati gani watumie silaha ipi. Inatisha!
Lakini, kama polisi wametumwa kwa sababu ya kutii amri za ‘mabwana’ zao, watambue ya kwamba wanajitengenezea tanuri dhidi ya jamii inayowazunguka, kwani ipo siku itasema imetosha.
Nimalize kwa kusema askari wa Jeshi la Polisi wanapaswa kufahamu kuwa utu ni bora kuliko kitu!
Ole wenu askari polisi mnaothubutu kuweka kando maadili na viapo vyenu hivyo kuwa hatari kwa raia badala ya kuwa salama yao.
habar ndo hiyo
ReplyDelete