MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, amemtaka Waziri wa Fedha na Uchumi Dk, William Mgimwa kueleza ni lini atatoa fedha za kugharimia miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa, katika Kata ya Msigani, Manispaa ya Kinondoni.
Mnyika alitoa kauli hiyo mwisho mwa wiki iliyopita wakati akiwa katika ziara iliyoambatana na ufunguzi wa matawi ya Chadema ndani ya chama hicho.
Akizungumza na wananchi wa Mbezi Malamba Mawili, mbunge huyo alisema baada Benki Kuu ya Tanzania kutangaza kuvuka lengo katika ukusanyaji kodi, ni vyema Waziri wa fedha akaeleza lini atatoa fedha za ujenzi wa madaraja hayo.
Alisema yeye akiwa mbunge anayewawakilisha wananchi wa Msigani, aliamua kufuatilia Hazina, ili kupata Sh500 milioni kwa ajli ya ujenzi wa wa madaraja mawili katika kata hiyo.
Alisema hata hivyo, hakufanikiwa kupata fedha hizo.
“Wananchi wana matatizo ya vivuko yakiwamo madaraja na kwa kutambua umuhimu wa vitu hivyo waliniagiza kufuatilia na nikafanya hivyo, lakini bila mafanikio,” alisema Mnyika.
Alifafanua kuwa alimuomba Waziri wa Fedha na Uchumi, kusaidia upatikanaji wa fedha hizo ili kufanikisha ujenzi wa madaraja, lakini hakujawa na mafanikio.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona wananchi wanapata taabu nyakati za mvua wakati kuna fedha zinazotokana na kodi.
No comments:
Post a Comment