Wednesday, September 5, 2012

Mauaji ya Daudi Mwangosi Polisi wanabeba lawama


JESHI la polisi halikuwa na sababu ya msingi ya kujaribu kuwatawanya kwa nguvu wanachama na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo waliokuwa wamekusanyika katika jengo la ofisi yao mpya kwenye kijiji cha Nyololo, Mufindi huko Iringa.
Uamuzi wa kuwatawanya wananchi hao ambao hawakuwa tishio kwa namna yoyote ile na kwa mtu yeyote ule ni sababu pekee inayonifanya niamini kuwa mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi yalitokana na uzembe uliokubuhu, ukosefu wa hekima na ubabe usio na mfano wa jeshi la polisi.
Kama Watanzania wengine nilishtushwa na habari za kifo cha mwandishi huyo ambaye alikuwa anazidi kupanda chati nchini lakini zaidi ni undani wa mauaji yake.
Kwa muda huu nimeamua kwa makusudi kupuuzia kabisa maelezo yanayotolewa na jeshi la polisi ambalo ni mtuhumiwa nambari moja wa uhalifu huu.
Habari za toka mwanzo wa tukio ziko wazi kabisa. Kuna vitu ambavyo havina utata kwani vimeshuhudiwa na watu waliokuwa karibu na kurekodiwa kwa dunia nzima kuona.
Kwamba – Daud Mwangosi alikuwa ni mwandishi mwenye kuheshimika na kujulikana pale Iringa halina utata. Licha ya kwamba amekuwa ni mwakilishi wa Channel Ten (siyo mwajiriwa wa moja kwa moja) huko Iringa.
Mwangosi alikuwa ndiye mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari. Kutokana na nafasi yake alijulikana na wanasiasa na bila ya shaka na viongozi wa serikali mkoani Iringa. Alikuwa ni sura ya waandishi wa habari mkoani pale na sauti yao vile vile.
Kwamba – tukio la kukamatwa kwa muda kwa mwandishi Godfrey Mushi wa Nipashe aliyekuwa anafuatilia tukio hilo la CDM pale Nyololo ikiwa ni maandalizi ya mikutano mingine wilayani Mufindi lilivuta sikio la Mwangosi ambaye bila kujali nafasi yake na akiamini kuwa polisi wana hekima ya kuweza kukaa na kuzungumza naye aliamua kwenda kuhoji kulikoni mwandishi wahabari ameshikiliwa. Ni uongozi usio na mfano wa kumfuata mtu mbele ya mitutu ya bunduki kwenda kuwahoji polisi.

Kwamba – Polisi wetu hawana hekima ya kupima mambo zaidi ya kutumia ubabe si jambo geni. Badala ya kumsikiliza walimuona kama ni mtu anayejifanya ana uthubutu wa kuzungumza na polisi. Badala ya kukaa naye na kusikiliza hoja zake waliamua kuondoka naye na kumpa hoja za kupigwa.
Kwamba – kabla ya kuuawa Mwangosi alipigwa vibaya nalo halina shaka. Washuhuda karibu waliokuwa pale walishuhudia jinsi kama mbwa mwitu maafisa wa polisi wakiwa na usongo wa kumkamata mbaya “wao” walimpiga.
Kimsingi polisi hawa wote ni wahalifu. Mwangosi hakuwa tishio la namna yoyote na kama alikuwa tishio polisi wangeweza kumtia pingu na kumdhibiti kwa njia za kipolisi na kuondoka naye na baadaye kumletea mashtaka (kama yapo) ili afikishwe mahakamani.
Lakini kundi hili la polisi waliamini kuwa wao wako juu ya sheria ya nchi, walimtuhumu Mwangosi, wakapitisha hukumu ya kupigwa na baadaye mmoja wao akajipa madaraka ya kutoa hukumu ya kifo. Wakamuua ndani ya dakika 30 tu kesi yake ilifikishwa kwao, ikasikilizwa bila yeye kuulizwa, na akahukumiwa kifo tena cha hadhara! Hili nalo halina utata.
Kwamba – hili limetokea mbele ya Mkuu wa Polisi wa Mkoa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya nalo halina utata. Kamanda Michael Kamuhanda anajulikana kama kamanda aliyesimamia mauaji ya wananchi wanne Iringa na ambaye badala ya kutiwa pingu na kupelekwa jela liwe somo akahamishwa na kupewa mkoa mwingine akilindwa na IGP Mwema na kamishna Chagonja ambaye kama ilivyokuwa Songea amekuja tena na maelezo yasiyo na kichwa wala miguu. Akimlaumu aliyeuliwa kwa mauaji yake tena bila kupepesa macho!!
Kwamba – matukio haya ya mauaji ya raia yana maagizo kutoka juu nalo halina shaka. Haiwezekani wananchi wawe wanauawa kinyama na uongozi wa juu wa taifa unatuambia “tumeunda tume tusubiri matokeo.”
Tume imeundwa Arusha, tume imeundwa Mbeya, tume imeundwa Songea, Tume imeundwa Morogoro na sasa wanaunda tume nyingine Iringa. Cha kushangaza sana uamuzi wa kuunda utume unachukuliwa na watuhumiwa wenyewe! Lakini cha kuudhi zaidi ni kuwa hakuna tume hata moja ambayo imeweza kuonesha matokeo yake na yakabadilisha utendaji wa polisi. Labda ipo haja ya kuunda tume itakayochunguza tume zilizoshindwa!!
Jambo kubwa la msingi ambalo liko wazi ni kuwa jeshi la polisi halikuwa na sababu ya msingi ya kuwatawanya wananchi kwa nguvu wakati wanachi hao hawakuwa tishio kwa namna yoyote.
Hoja ya kwamba ati sensa ilikuwa inaendelea ni hoja ya kipuuzi. Hivi watu hawaendi misibani leo? Mbona Fiesta ya Mwanza ilifanyika hadi usiku na polisi walikuwepo kutoa ulinzi? Au sensa ina uzito pale ambapo CDM wanafanya mikutano yao tu? Ingekuwa na uzito kama mikutano yote ya watu Tanzania nzima ingesitishwa.
Ikumbukwe kuwa wananchi waliotawanywa hawakuwa barabarani; hawakuwa wanaandamana, na wala hawakuwa kwenye harakati za maandamano. Walikuwa kwenye shughuli ya kufungua tawi la chama chao; wafungue, washangilie, watupe madongo ya kisiasa, watawanyike!
Sasa polisi wetu wakaamini – kwa udhaifu wao – kuwa kwanini CDM wafanye mkutano wa kisiasa? Kwamba wakakosa hekima kabisa kwa vile mtu kawaambia “msiwaache wafanye lolote” na kina Kamuhanda kama maroboti yaliyovunjika ufunguo wanaanza “tawanyika tawanyika!” Hekima inatusukuma kuuliza. Lipi lilikuwa rahisi? Polisi kukaa pembeni ya ofisi za CDM na kuwapatia ulinzi hadi wamalize shughuli zao au kwa polisi kuwatawanya kwa nguvu?
Hoja mbaya zaidi na ya kukera ni hii ambayo inatolewa na watu ambao nina mashaka na uwezo wao wa kufikiri ulipofikia. Hoja hii kimsingi iko hii: Mwangosi asingeuawa kama CDM wasingefanya shughuli yao ya kufungua tawi hasa kwa vile serikali ilikuwa imepiga marufuku mikutano hiyo.
Na wengine wanaenda mbele zaidi kutoka hapo: wanasema-serikali ikishasema ni lazima ukubali maana huwezi kushindana na serikali. Mawazo haya wapo watu kwenye polisi na Ikulu wanaamini. Nina uhakika watu wanakumbuka ile hotuba ya Mbayuwayu ambapo Rais Kikwete aliwaambia wafanyakazi kuwa wakiwasikiliza kina Mgaya (katibu wa OTU) wasije kushangaa wanapigwa na polisi na kina “Mgaya hamuwaoni.”
Sasa hoja hii inavutia kama ukiwa kwenye madaraka na kama unaamini serikali kwa kila kitu. Na inavutia zaidi kama wewe ni mtu ambaye hufikirii kuwa serikali kwa asili yake ni kandamizi na kwamba zikiachwa bila kukataliwa zina kawaida ya kutawala kwa mabavu. Serikali hazipendi kukosolewa na kwa hakika hazipendi kuoneshwa kuwa zinachukiwa.
Na kwa vile serikali ni watu (siyo mashine), basi hupenda kuonekana wanapendwa, wanakubaliwa na kufuatwa fuatwa kwa haiba nzuri. Matokeo yake serikali inapojikuta inapingwa na kupata upinzani inaweza kufanya lolote, kwa yeyote na kwa namna yoyote bila kujali matokeo!
Hivi ndivyo serikali za Kikoloni zilivyoishi na kutawala. Hazikutaka wananchi waulize, na hawakutaka wananchi wapinge. Ukipinga na kuletwa pale Bomani basi utakiona cha moto.
Wananchi hawakutakiwa kabisa kupinga utawala wa kikoloni. Ndio sababu kina Robert Makange, Kheri Rashid Baghelleh walitiwa pingu na mkoloni baada ya kuandika makala ambayo watawala wa kikoloni waliiona ni ya kichochezi.
Ni sababu hiyo hiyo iliyomfanya Nyerere ahukumiwe kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kutoa kauli ambazo zilionekana ni za kichochezi. Yeye aliamua kulipa faini. Watawala hawapendi kuoneshwa kuwa wanatawala vibaya!
Lakini hoja hii ikikubaliwa kina Mandela hawakutakiwa kupinga utawala wa kikaburu na kina Steve Biko hawakutakiwa kuhamasisha mwamko wa mtu mweusi.
Kwani wote hawa walisimama kinyume na kile ambacho serikali ya Kaburu ilitaka. Hoja hii ikikubaliwa mapinduzi yaliyomuondoa Hosni Mubarak Misri yasingewezekana kwani wananchi walikataa kutii amri halali kabisa za jeshi la polisi zilizowataka kutawanyika!
Hoja hii ikikubaliwa Bashir Assad wa Syria angekuwa anatawala kwa raha mustarehe tu na wananchi wake wasingeinuka dhidi yake! Hoja hii ndugu zangu ikikubaliwa Watanzania watatawaliwa wasivyotaka kutawaliwa. Kwani kila mtu akihoji serikali ataambiwa ‘serikali imesema’ na yeye atanywea!
Hii inanikumbusha makala yangu ya huko nyuma juu ya kuabudu sanamu ya Mfalme Nebukadneza wa Uajemi. Ilitolewa amri na serikali kuwa watu wote wapige magoti mbele ya sanamu hiyo.
Nabii Daniel anaandika kuwa mawaziri, wakuu na maliwali pamoja na maelfu ya watu waliitii amri hiyo halali ya serikali! Amri halali ambayo ilishindana na dhamira za vijana watatu marafiki wa Daniel – Shedrack, Meshack na Abednego. Hawa hawakuwa tayari kutii amri ya serikali – japo halali – kwa sababu dhamira zao zilikataa kufanya kufuru!
Walipoambiwa kuwa wasipokubali kupiga magoti watatupwa kwenye tanuru ya moto walisema kwa ujasiri kuwa wako tayari kwenda kwenye tanuru hiyo kwani Mungu wao anaweza kuwaokoa bado na kama hatowaokoa basi wataonana upande wa pili wa maisha!
Ndugu zangu hoja hii ya mwisho ni ya hatari sana. Ni ya kitumwa. Kina Martin Luther King Jr. walipewa amri halali ya kukataza maandamano kutoka Selma Alabama huko.
Walikatazwa na jeshi la polisi kufanya mikutano mbalimbali, lakini wakiamini katika ukuu wa dhamira zao waliendelea.
Matokeo yake ni kulazimisha serikali dhalimu kubadilika.
Ndugu zangu, polisi hawawezi na hawapaswi kuja kukuambia utoke nyumbani kwako bila sababu na wewe ukiwa na akili timamu unaamua kutoka kwa sababu ‘serikali imesema.’
Polisi wanahitaji kuwa na sababu ya msingi na inayoweza kushawishi kutaka watu waondoke mahali. Maana kila watanzania wanapokubali kusukumwa na serikali yao ndivyo serikali nayo inavyothubutu zaidi kuwasukuma.
Tumeona watu wanaondolewa kwenye nyumba zao walizoishi na wao wanakubali huku wakilia “serikali yetu serikali yetu,” tumeona mamia ya watu ambao waliamua kujitafutia makazi huko Tegeta ambapo serikali ikaenda na kuwavunjia vibanda vyao maskini wa Mungu na wao wanabakia “serikali itufikirie” Tumeona jinsi wananchi wanavyohamishwa kwenye maeneo yenye ardhi yenye rutuba (Katavi na Usangi) na wao wakikaa pembeni wanalia. Kwa sababu wanaamini serikali ikisema haitakiwi kupingwa.
Wananchi wetu bado hawajatambua ukuu wa dhamira ya mwandamu dhidi ya watawala. Kama mtu mmoja alivyosema baada ya tukio la Morogoro kuwa wao (Polisi) wanajifunza kuua basi wao wananchi wanajifunza kufa.
Kimsingi alisema kuwa dhamira zao zitakuja kusimama kiasi kwamba watakuwa tayari kufa. Na polisi wasije kufikiria kuwa kwa kuendelea kuua wananchi bila kujali matokeo (with impunity) basi wananchi wataogopa kujitokeza kwenye mikutano ya CDM au wataogopa kukataa serikali dhaifu ya CCM.
Kwa kadiri siku zinavyoendelea, ndivyo serikali hii ikitumia vyombo hivi vya mabavu inavyozidi kujijengea chuki kwa wananchi. Na kina Mwema, Chagonja, Kamuhanda na wenzao ambao wanaamini leo vimulimuli na nyota ni kinga yao wakae wakijua kuwa siku moja watasimama kulipishwa. Na kulipa watalipa kwani damu ya Watanzania haitoenda bure! Hata kama CDM haitaweza kuwalipisha kwa sababu ya woga au kutojua cha kufanya wajue kuwa kipo kizazi cha Watanzania kinachowaangalia na kuwafuatilia na kuwahesabia makosa yao.
Watakuja kulipa tu; damu ya kina Zona na Mwangosi, damu ya vijana wa Arusha, Songea na Mbeya; ni lazima ije kulipiwa. Na wanaodhania kuwa watatawala milele wafikirie tena kwani na wao watakuja kulipishwa tu.
Waache waendelee kukaa pembeni na kuunda tume juu ya tume huku wakilizuga taifa. Wananchi watakumbuka na siku yao itakapofika watasimamishwa kizimbani. Hakutakuwa na saluti hapo, hakutakuwa na ving’ora na hakutakuwa na “mzee”. Watakuwa ni wahalifu tu kama wengine!! Watalipa.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment