Tuesday, September 18, 2012

Jerry Muro aibukia Bavicha

Mtangazaji aliyejizolea umaarufu katika vipindi mbalimbali vya Televisheni ikiwemo kituo cha ITV, Jerry Muro, ameibukia katika mkutano wa kamati tendaji ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) na kuwataka vijana kufichua mafisadi wanaotumia vyeo vyao  na fedha ili kuwanyonya wananchi.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa kamati hiyo tendaji, Muro ambaye kwa sasa ni mwanaharakati wa vijana, alisema vijana wanapaswa kupiga vita viongozi wanaotumia fedha na madaraka yao kufanya ufisadi na kusababisha wananchi kuishi katika hali ya umasikini.

Alisema hivi sasa nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendo vya ufisadi hivyo vijana kote bila kujali itikadi ya vyama wanapaswa kuhakikisha wanapigania maslahi ya nchi badala ya kunufaisha watu wachache wenye tamaa.

"Ni lazima mkumbuke kuwa asilimia 18 ya vijana wa hapa nchini ni vijana wasomi huku wakikosa ajira hivyo ni vyema wakachukua nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo kupigania harakati ili kuliletea taifa maendeleo,’’ alisema Muro.

Aliongeza kuwa “nawahimiza vijana muwe mstari wa mbele katika kuitetea nchi na kuhakikisha inapata maendeleo sambamba na kuwafichua mafisadi ambao wamekuwa wakitumia vyeo vyao na fedha katika kuwanyonya wananchi.”

Kadhalika, aliwataka Bavicha kuwa mstari wa mbele kuonyesha nidhamu ili kuwa mfano wa kuigwa na vyama vingine vya kisiasa nchini.

Kwa upande wake akifungua kikao hicho cha kamati tendaji kinachoshirikisha wenyeviti na makatibu kutoka mikoa yote, Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, alisema nchi imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali hususani za kisiasa, kiuchumi na hata kijamii hivyo inahitajika njia mbadala wa kuzitatua changamoto hizo hasa kupitia vijana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment