Friday, September 21, 2012

Hoja ya Lissu yapigwa kufuli


HOJA ya uteuzi wa majaji wasio na sifa iliyotolewa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), imeonekana kuitesa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na hivyo kutangaza kuzuia mjadala huo kwenye vyombo vya habari.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi, jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa vyombo vya habari na jamii hawapaswi kuzungumzia hoja hiyo kwa madai kwamba kufanya hivyo kunaingilia uhuru wa kamati yake.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo kwa sasa suala hilo bado linashughulikiwa kamati yake na watakapokamilisha kazi hiyo uamuzi wake utatolewa katika kikao kijacho cha Bunge.
“Kwa sasa bado kamati yetu inaendelea na uchunguzi kuhusu suala hilo hivyo basi tunashauri watendaji wa serikali, wa mahakama, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kutoendelea kujadili ili kuiwezesha kamati yetu kufanya kazi yake kwa uhuru kama inavyotakiwa,” alisema Ngwilizi.
Aliongeza kuwa kamati inafanya kazi zake kwa usiri na haitakiwi suala hilo kujadiliwa nje ya Bunge, hivyo kwa wanaoendelea kutoa maoni yao nje ya Bunge wanakiuka kanuni za uwepo wa kamati hiyo.
Alisema kamati hiyo imekuwa ikishuhudia majadiliano na malumbano makali yanayoanzishwa kupitia vyombo vya habari kuhusu jambo hilo huku vingine vikirejea taarifa zinazodaiwa kusemwa ndani ya vikao vya kamati.
Alitoa rai kwa vyombo vya habari au taasisi zinazodhani kuwa zina maoni kuhusiana na hoja hiyo iliyotolewa na Lissu, kuyawasilisha kwa Katibu wa Bunge ili ziwasilishwe kwao na kufanyiwa kazi.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment