Tuesday, September 11, 2012

Chadema wawang'ang'ania Waziri Nchimbi, vigogo polisi


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepitisha maazimio saba, mojawapo likitaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, na Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja, kujiuzulu nafasi zao mara moja kutokana na mauaji ya raia katika mikoa ya Morogoro na Iringa kutokea mikononi mwa jeshi hilo, ambalo lipo chini ya usimamizi wao.

Kimesema iwapo waziri huyo pamoja na viongozi hao wa jeshi hilo watashindwa kuwajibika, basi Rais Jakaya Kikwete, awafukuze kazi mara moja.

Wengine ambao wametakiwa na chama hicho kujiuzulu mara moja kwa tuhuma hizo, ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na Mkuu wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Morogoro.

Pia kimetaka askari waliosababisha mauaji ya raia wasio na hatia katika mikoa hiyo wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

Chama hicho pia kimeazimia kutoshiriki shughuli zozote zitakazosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, hadi atakapoondolewa katika nafasi yake na kuteuliwa msajili mwingine.

Maazimio hayo yalipitishwa na Kamati Kuu ya Chadema katika kikao chake maalum kilichofanyika jijini Dar es Salaam juzi, ambacho pamoja na mambo mengine, kilijadili hali ya siasa nchini kufuatia mfululizo wa mauaji yanayofanywa na jeshi hilo katika shughuli za chama hicho.

Pia kilijadili mipango ya baadhi ya viongozi wa serikali ya kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa mbinu haramu.

JK AANDIKIWA BARUA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akisoma maazimio hayo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema Kamati Kuu imeamua kumuandikia barua Rais Kikwete kumtaka achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka yake na kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

“Iwapo serikali haitazingatia, Chadema itawaongoza wananchi kwa njia za kidemokrasia ikiwamo maandamano ya amani kushinikiza hatua za haraka kuchukuliwa kwa maslahi ya Taifa,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Tutaitisha maandamano ambayo hayajawahi kutokea katika nchi hii. Tutatangaza tutakapokuwa tayari. Haki ya Mungu hatutanii.”

Alisema anashangaa kuona Nchimbi akishangaa kuona Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akiwa huru, wakati waziri huyo, IGP Mwema, Chagonja, makamanda hao wa polisi, wakuu hao wa FFU pamoja na askari hao ndiyo wanaostahili kuwajibika kwa kuwa ushahidi kuhusiana na tuhuma dhidi yao uko wazi.

Mbowe alisema kwa maslahi mapana ya Taifa, Rais Kikwete anapaswa kuunda tume huru ya kiuchunguzi ya kimahakama kuchunguza vifo vilivyotokea katika mazingira tata katika mikoa ya Arusha (Arusha Mjini na Arumeru), Singida, Morogoro na Iringa, kama ambavyo Chadema wamekuwa wakisisitiza siku za nyuma.

Alisema Chadema haiitambui kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, kwa kuwa haina msingi wa kisheria na kwa hiyo, hawatatoa ushirikiano wowote kwa kamati hiyo.

TENDWA KUSUSIWA

Kamati Kuu pia imemtangaza Tendwa kuwa ni adui wa demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyonayo, kutokana na utendaji dhaifu, unaoegemea upande mmoja na wa kipropaganda unaoonyeshwa naye.

“Kamati Kuu imeazimia kuwa pamoja na kuendelea kuheshimu sheria ya vyama vya siasa, Chadema haitashiriki shughuli zozote zitakazosimamiwa na John Tendwa hadi hapo atakapoondolewa katika nafasi yake na kuteuliwa msajili mwingine,” alisema Mbowe.

Alisema Tendwa amekuwa na kauli tata kuhusu vyama vya siasa nchini, ambazo haijulikani kama anashinikizwa au anajipendekeza.

“Huyu ni mtu hatari. Ajiuzulu au awajibishwe. Hatutafanya kazi yoyote na John Tendwa. Hatutachukua amri ya John Tendwa.
Tutaheshimu sheria. Tutakuwa tayari kuchukua maelekezo ya karani kuliko ya John Tendwa.

Akituita hatumsikilizi hadi atakapoomba radhi. Vinginevyo hatutakwenda kwenye mikutano yake. Na ajaribu kufuta Chadema. Siyo Tendwa hata Kikwete jaribu kufuta Chadema,” alisema Mbowe.

Alisema pia Kamati Kuu inalihimiza Jeshi la Polisi kusimamia, kufuata, kuheshimu na kusimamia kwa haki sheria zinazoongoza shughuli za vyama vya siasa, ikiwamo kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa inayotoa fursa kamili kwa vyama vya siasa kufanya mikutano na maandamano kama sehemu ya kazi ya uenezi ya vyama hivyo.

Mbowe alisema Kamati Kuu imeazimia pia kuwa Operesheni ya M4C iendelee na kazi zake kwa kufuata kikamilifu ratiba iliyopitishwa na Baraza Kuu na Kamati Kuu katika vikao vya awali, ikiwa ni sehemu ya kutimiza dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganaizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.

YAVUNJA UONGOZI, YATIMUA MADIWANI 


Alisema pia Kamati Kuu imepokea taarifa ya kamati iliyoundwa na Katibu Mkuu wa chama kuchunguza chanzo cha mgogoro wa chama mkoani Mwanza na imeamua kuwavua uanachama madiwani wawili; Adam Chagulani (Kata ya Igoma) na Henry Matata (Kata ya Kitangiri) kwa kukiuka kanuni na maadili ya chama ikihusisha tuhuma za ufisadi.

Mbowe alisema Chadema itakuwa tayari kuwajibika kwa lolote litakalotokea huko mbele kufuatia uamuzi wao dhidi ya madiwani hao.

Kamati Kuu pia imeuvunja uongozi wa chama mkoa huo kutokana na uzembe uliofanyika katika eneo lake la kazi na kwamba, utaratibu wa kuweka uongozi mpya utafanyika.

Alisema ‘madiwani’ hao walishapewa onyo na karipio, hivyo walikuwa chini ya uangalizi na kwamba, kabla hatua ya juzi ya Kamati Kuu walipewa pia nafasi ya kujieleza.

Mbowe alisema uamuzi huo wa Kamati Kuu ni onyo kwa viongozi wote wa Chadema kwamba, chama hakitaweza kumvumilia mtu yeyote anayeonekana kukwamisha tumaini la Watanzania kufanikisha ukombozi wa mabadiliko ya kimfumo na kiutawala kwa kukikabidhi chama hicho madaraka mwaka 2015.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment