Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeazimia kwenda mahakamani wiki hii kumshtaki Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, baada ya kushindwa kukiomba radhi chama hicho pamoja na kutoa faini ya Shilingi bilioni tatu, baada ya kupita kwa muda aliopewa kufanya hivyo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Chadema, Anton Komu, alisema chama hicho hivi sasa kinakamilisha taratibu za kisheria ili kwenda mahakamani.
Alisema "wakati wowote wiki hii tutakwenda mahakamani, leo jioni (jana) nitakutana na mawakili ambao wanashughulikia jambo hilo."
Komu alisema imelazimu suala hilo kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa Nape amekataa kuomba radhi kuhusu madai aliyoyatoa.
Chadema ilimtaka Nape aombe radhi baada ya kukituhumu kwamba kimekuwa kikichangisha fedha kwa wananchi katika mikutano yao wakati kinapokea mabilioni ya fedha kutoka nje ya nchi.
Nape alitoa tuhuma hizo Agosti 12 na kueleza kwamba anao ushahidi kuwa chama hicho kimekuwa kikiwahadaa wananchi kwa kuwachangisha fedha huku kikipokea mabilioni ya fedha kwa wafadhili kutoka nje na kwamba upo uwezekano wa chama hicho kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani.
Baada ya kauli hiyo, bodi ya wadhamini wa Chadema iliagiza wanasheria wake wamwandikie Nape barua ya kumtaka kukiomba radhi chama, kwa kutumia vyombo vya habari.
Chadema inataka kuombwa radhi na fidia ya fedha ni kwa ajili ya fedheha na fundisho kwa kitendo cha uzushi na uongo kilichotolewa na Nape.
Nipashe
No comments:
Post a Comment