Tuesday, August 7, 2012

Waziri Membe abanwa


ATISHIA KUJIUZULU, SERIKALI YAFUNGA MJADALA, CHENGE SAFI
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akisema hakuna rushwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada kutoka nchini Uingereza, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamemkalia kooni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, wakimtaka awataje watuhumiwa na kashfa hiyo.
Wabunge hao walitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa wakichangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa na kwamba mbali na kutajwa kwa watuhumiwa hao pia serikali iwachukulie hatua na si kufurahia tu chenji yake ambayo imerejeshwa nchini hivi karibuni.
Mbunge wa Viti Maalum, Rachel Mashishanga (Chadema), alisema kuwa Waziri Membe alipata kueleza anawafahamu watuhumiwa na kashfa hiyo ni vema akawataja, ili jamii iwatambue.
Naye mbunge wa Gando, Khalifa Khalifa (CUF), mbali ya kumtaka Waziri Membe kuyataja majina ya watu waliohusika katika kashfa hiyo, kwani kitendo cha kutoyataja kinaashiria kuwa naye anahusika.
“Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unahitimisha hoja yako wataje hao waliohusika katika kashfa ya rada…usifurahie chenji ya rada, kwani huo ni udhalilishaji mkubwa kwa serikali yetu.”

Awali, msemaji wa kambi ya upinzani wa wizara hiyo, Ezekia Wenje, alisema kambi hiyo inaendelea kuhoji ni kwa nini mpaka sasa watuhumiwa wa kashfa hiyo wanaendelea kutembea vifua mbele bila kuchukuliwa hatua zozote.
“Mpaka sasa haieleweki ni kwa sababu gani nchi hii pamoja na kudai kuwa ina uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe iliamua kuliachia suala hili kufanyiwa kazi na serikali ya Uingereza, kuanzia uchunguzi hadi mashtaka ya kurudishwa fedha zilizotokana na rushwa ya rada ambayo sasa imebatizwa jina tamu ya chenji ya rada,” alisema.
Wenje ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara hiyo, alisema pamoja na serikali kushindwa kufanya uchunguzi na hatimaye kuwashtaki watuhumiwa wa rada, ilipobainika kuwa inatakiwa kurudishwa chenji ya rada serikali ilikuwa mstari wa mbele kufuatilia chenji hiyo na kuipangia matumizi.
“Tunashindwa kuelewa umakini wa serikali uko wapi, kwamba inaweza kuweka msisitizo katika kuhakikisha fedha za rushwa ya rada zinarudishwa nchini, lakini haiwezi kuthubutu kushughulikia wale waliosababisha upotevu wa fedha hizo kwa njia ya mkataba,” alisema.
Alibainisha kuwa taarifa mbalimbali zinazotokana na utafiti wa suala hilo, zinaeleza namna wizi huo ulivyofanyika ukiwahusisha Watanzania wengine wakiwa ni viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali ya CCM na kwamba Watanzania wanashangaa watuhumiwa hao sasa wanachaguliwa kuongoza mhimili muhimu wa Bunge.
Serikali yalazimisha kufunga mjadala
Akijibu hoja za wabunge kuhusu kashfa hiyo ya rada, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alisema serikali imefunga mjadala kwani hakuna rushwa katika suala hilo.
Alisema, hata Uingereza iliyochunguza suala hilo imeeleza bayana kwamba hakuna rushwa na katika hatua hiyo serikali haiwezi kumfikisha mahakamani mtu yeyote.
“Katika hali kama hii tukimpeleka mtu mahakamani na ushahidi tunaoutegemea, ni upande ule wa BAE na SFO maana huku hakuna mashahidi… sasa kule hata kumtaja mtu hauruhusuwi na serikali hii iliingia mkataba na hawa, tukisema tunataka kumwita mtu aje kutoa ushahidi huku hawatakubali,” alisema.
“Kwa hiyo naomba jambo hili lifike mwisho hakuna rushwa katika rada ambayo inawahusu Watanzania tunaowajua,” alisema.
Alieleza kuwa kabla ya kuzungumza hayo aliwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kumuuliza kama kuna kitu kipya na alimwambia hakuna anayehusika.
Alisema kuwa alilieleza suala hilo Julai 5 mwaka jana na kudhani kuwa limekwisha, lakini anaona bado linajirudia na kusema inaonekana jambo hilo halijaeleweka kwa wananachi.
“…Jamani hakuna kesi ya rada dhidi ya mtu yeyote hapa Tanzania kuhusu sakata la rada…Niliomba kama kuna mtu ndani au nje mwenye ushaidi aulete, maneno maneno mahakamani hakuna unatakiwa ushahidi unaojitegemea.
“Sasa nikaambiwa kuna kitabu kimeandikwa na mimi nimekisoma na wale waliotajwa kama ningekuwa mshauri wao ningewashauri wamfungulie mashtaka mwandishi wa kitabu hicho maana msingi wa kitabu chake ni magazeti. Anasema fulani mwizi ananukuu This Day, fulani mwizi ananukuu The Guardian.”
Wiki iliyopita Rais Kikwete wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema hakuna rushwa kwenye ununuzi wa rada na badala yake kulikuwa na makosa ya uchapaji.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina, lakini kwa kauli hiyo ni dhahiri kwamba alimsafisha Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa hiyo kutoka Kampuni ya BAE- System ya nchini Uingereza.
Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi.
Mwingine anayehusishwa na kashfa hiyo, ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashid.
Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu wa kati wa biashara hiyo.
Mchakato wa ununuzi wa rada, uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Blair anatajwa kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza BAE-Systems. Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi maskini kabisa duniani, kutumia sh bilioni 40 kununua rada katikati ya umaskini unaonuka.
Waziri Membe atishia kujiuzulu
Katika hatua nyingine, Membe ametishia kujiuzulu iwapo atajitokeza mtu atakayeweza kuendesha wizara hiyo kwa bajeti ya asilimia 42.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia hoja yake, Waziri Membe alisema wizara hiyo inapata mgao kidogo wa bajeti isiyokidhi mahitaji na katika mwaka wa fedha ulioisha wizara hiyo ilipata asilimia 44 ya bajeti iliyoombwa.
“Kama atajitokeza mtu anayeweza kuendesha wizara hii kwa bajeti ya asilimia 42 nitakuwa tayari kujiuzulu, kwani wizara hii imekuwa ikipata mgao kidogo wa bajeti, hivyo tuna changamoto nyingi,” alisema.
Alisema pamoja na mapungufu hayo, wizara hiyo ambayo ni kiungo muhimu cha nchi yetu na nchi za nje imeendelea kushirikiana kwa karibu na wizara, idara na taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi kuhakikisha nchi inafaidika kwa kadri iwezekanavyo na fursa mbalimbali zenye manufaa kwa nchi.
Alitoa mfano kuwa wizara hiyo imeshirikiana na ubalozi wa China na Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha nchi inapata dola bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment