- Wanasiasa wanaotoa lugha ya vita hawana hekima na ni hatari
- Wengine wanatafuta ujiko wa kisiasa
- Tusizungumzie vita kama hatuko tayari kupigana
- Vita si lelemama
Sikutegemea kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje Bw. Lowassa kutoa kauli ambayo ikiunganishwa na ile ya Sitta na ya Membe inazidi kuchochea hali ya kutotafuta suluhu. Wote hawa watatu bila ya shaka wanasema kutokana na nafasi zao lakini pia yawezekana wanasema kwa sababu wote watatu wanatajwa vile vile kama wagombea watarajiwa wa urais mwaka 2015. Hata hivyo nazipima kauli hizi kwa jambo la kwanza na si kwa hilo la pili.
Vita si jambo dogo na si jambo la mzaha kama watu wengine wanavyochukulia. Nimeona tangu Wamalawi walipozungumza suala la kudai "ziwa zima" la Nyassa kuwa ni lao baadhi ya watu wetu mwitikio wao wa kwanza umekuwa ni "tupeleke majeshi" au "tupeleke vijana wetu" na sasa leo Lowassa ananukuliwa na vyombo vya habari mbalimbali kuwa JWTZ liko tayari kwenda vitani na Malawi kuhusu suala hili. Hili ni jambo la kusikitisha na kushangaza.
Kufikiria vita siyo jambo dogo na wala si jambo la kutafuta ujiko au siasa. Ni sawa na kuamua kushika bunduki na kumuelekezea mtu. Polisi huwa wanaambiwa kuwa usielekeze Bunduki kama hauko tayari kuitumia. Wale ambao wanabeba silaha (nao ni raia) wanajua kabisa kuwa hutoi silaha kibindoni kama hauko tayari ku-pull the trigger. Maana ya yote haya ni kuwa kutoa silaha na kuishika mkononi siyo suala la ubishoo, urembo au kujionesha kuwa unaweza.
Tusipokemea hili la wanasiasa mwisho tutaona watu wanaanza mazoezi ya kutuonesha vifaa vya kivita ili kuwapiga mkwara wa Malawi. Na kweli wapo ambao wanatamani kuona "vijana wetu" wanaanza kuelekea mpakani au kwenye ukingo wa Ziwa Nyassa ili kutuma ujumbe kuwa tuko tayari. Sasa hili ni zuri na linasisimua akili na hisia za "kizalendo". Lakini tusije kuwa ni mambo ya Wag the Dog ambapo ili kushinda uchaguzi timu ya wanamkakati wa kampeni waliamua kutengeneza 'vita isiyokuwepo' ili kupoteza mawazo ya wapiga kura.
Ninachoogopa zaidi ni kuwa wakati watawala wetu tumewabana kuhusu uongovi wao mbovu, sera zao zilizoshindwa na ukosefu wa maono usiokoma suala la mgogoro wa Ziwa Nyassa limewapa 'gia' ya kutokea na sasa hata watu waliokaa kimya wakati wananchi wetu wanauawa nakudhalilishwa na vyombo vya usalama wanasimama pasi ya kuomba radhi na kutaka tusimame nyuma yao. Nimeshangaa kuona Lowassa leo ameweza kukutana na vyombo vya usalama na kupewa taarifa zinazohusu vita lakini huyu huyu hajakutana na vyombo hivi wakati maisha ya wananchi wetu yanahatarishwa na vyombo hivi. Alikuwa wapi kwenye matukio ya Arusha, Mbeya (Tukuyu), Tarime na Songea? Kote huku hakuonesha kujali sana lakini leo ameibuka na kuonesha kuwa ana uwezo wa kufuatilia vyombo vya usalama?
Kama nilivyosema hapo juu vita si lelemama kama baadhi ya watu wanafikiria. Najua wapo ambao wanafikiria kuwa vita dhidi ya Uganda ilikuwa ni uamuzi wa haraka na papara. Wengi (labda vijana zaidi) wanakumbuka tu maneno ya "nia tunayo na sababu tunayo" lakini ni wachache (hata wazee yumkini) wanaokumbuka kuwa kabla ya kufikia maneno hayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alielezea juhudi mbalimbali za kutatua mgogoro wetu na Uganda licha ya "chokochoko" zilizoanza miaka karibu mitano nyuma. Kwa Tanzania kwenda vitani ilikuwa ni uamuzi wa mwisho pale ambapo njia zote za amani na kidiplomasia ziliposhindwa.
Leo viongozi wetu tena wakubwa na wenye dhamana nzito zaidi wanazungumza kana kwamba tumeshindwa kabisa kutafuta njia za amani na za demokrasia na sasa wanataka kuifanya Malawi kama wanavyofanyia wananchi wetu. Wananchi wakiandamana wanapigwa virungu na kuuawa na wakigoma wananyamazishwa kwa ghafla. Na hata mazungumzo wanataka yawe kwa masharti yao. Matokeo yake wamejenga fikra wanaweza kum-bully mtu yeyote, vyovyote, na kwa lolote kiasi kwamba wanataka kuanza kuibully Malawi. Hili linafanywa kwa sababu moja tu kuwa Tanzania ni kubwa kuliko Malawi na inawezekana ina uwezo mkubwa wa kuishinda Malawi.
Wanaozungumza hivi wanafikiria vita inapigwana na wingi wa watu tu na vitu. Vita ni mikakati na mbinu lakini vile vile vita ni kujitoa muhanga. Tunapozungumzia lugha ya vita sijui kama tunafikiria viongozi wetu wanaweza kuhamasisha taifa kama ilivyokuwa miaka ya 1970 ambapo watu walichangia kuku, mbuzi na ng'ombe. Wangapi kati yetu leo watakuwa tayari kutoa magari na mabasi yao kwenda vitani? Wangapi wataamua kwa hiari yao kwenda kupigana chini ya viongozi hawa hawa? Itakuwaje kama watu wakiwa vitani kashfa kubwa ya ufisadi nyumbani inanguruma tena (mafisadi kwa asili hawabadiliki).
Tunapozungumzia vita tunazungumzia maisha ya watu kuuawa. Watu wasifikiri kuwa tukienda vitani na Malawi au nchi nyingine yoyote jirani basi tutakuwa kama tunamsukuma mlevi. Ni wangapi wanafikiria kulipuliwa kwa miji yetu inayozunguka ziwa Nyassa? Mbamba Bay, Kyela, Tukuyu, Rungwe, Mbeya, hata Songea? Kweli kina Lowassa wanapozungumza lugha ya vita wanafikiria kabisa kuwa tumesahau jinsi Amin alivyolipua Mwanza? au ndio viongozi wetu hata historia tena wamesahau? Au watu wamesahau jinsi tulivyolazimika kuchimba mahandaki na kufanya mazoezi ya kujihami hadi kuwa na kuku ndani kwa ajili ya kukimbia nao kwenye mahandaki? Au watu wameshasahau jinsi Idi Amin alivyoweza kuua mamia ya watu wetu pale vikosi vyake vilipovuka Mutukula na kuingia Kagera?
Ninachosema ni kuwa ipo haja ya haraka ya viongozi wetu kuonesha hekima ya kukwepa lugha ya vita. Si kwa sababu hatuna uwezo wa kupigana na Malawi (naamini tunao tena mkubwa na naamini tunaweza kushinda) lakini bado hatujawa na sababu ya kufanya hivyo. Watu kudai "ziwa zima" wakati sisi tumejenga bandari na watu wetu wanavua na kuishi kwenye ziwa hilo na tuna meli miaka nenda rudi na Wamalawi hawajarusha hata baruti ni jambo la kutufanya tufikiri. Kama kweli Wamalawi wangekuwa wanataka vita au ugomvi mbona wao sababu "wanayo" kuwa tumeingilia Ziwa lao na tunafanya vitu kinyume cha sheria?
Wamalawi walipozungumza kwa lugha ya Vita mara moja walitambua kuwa hakuna sababu ya ku-escalate tension kwenye eneo hilo hasa kwa vile tayari tumeshawahi kuwa na tension sana. Ndio maana Waziri wa Mambo ya Nje aliamua kupunguza makali ya lugha ya vita. NI wakati kwa viongozi wa TAnzania nao kupunguza ukali usio wa lazima na kuchochea lugha ya vita. Na sisi wananchi tusiuziwe kirahisi vita kwani ina gharama kuliko watu tunavyoweza kufikiria. Ikumbukwe vita ya Uganda iliigharimu Tanzania kuliko watu wengi wanavyojua na imeacha mojawapo ya majeraha makubwa katika mwelekeo wa uchumi wetu ambayo hadi leo tunasikia maumivu yake. Sijui kama tunataka vita nyingine hasa kwa sababu ambazo ni za kidiplomasia na kisiasa.
Hekima itusukume kufikiria mara mbili. Tutoe nafasi kwa diplomasia na mazungumzo ya amani na nina uhakika wa Malawi kama ni watu wa amani watanyosha mkono wa amani. Njia mojawapo kama tukitaka na sisi kutumia mbinu za diplomasia ni hilo nililosema kwenye mada nyingine badala ya kupeleka vifaru na askari wetu karibu na Ziwa Nyassa na sisi tuanze utafiti kwenye eneo tunaloamini ni letu na kuwaacha Wamalawi wafanye kwenye eneo lao. Kama wanafanya hivyo kwenye sehemu ya eneo letu basi tuna sababu ya kuhakikisha hizo 'incursions' hazitokei na hapo ikibidana kuweka boti zenye silaha kuhakikisha hayo hayatokei.
Endapo juhudi hizi za kuonesha sisi ni watu wa amani hazitapokelewa na kama juhudi za kidiplomasia zitashindwa na Wamalawi watapuuzia kabisa madai yetu na kuanza kutenda kanakwamba hatuna la kusema basi ni wakati huo Watanzania waandaliwe kwa kitu ambacho kinaweza kutokea - vita. Na hili lisizungumzwe na kila "dick, tom and harry" kwa sababu wanavaa suti za vyeo mbalimbali. Mtu pekee wa kuweza kulizungumzia hili kama uwezekano ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Endapo tutaacha wanasiasa ambao wanatafuta ujiko kwenye macho ya wananchi walizungumzia na kututia hamasa wakati wao wenyewe hawatoenda vitani na yawezekana hawana mtoto au ndugu hata mmoja JWTZ basi tutajikuta tunapelekwa vitani kisiasa na siyo kwa sababu tunatishiwa au tunajihami. Ni matumaini yangu viongozi wa upinzani (CHADEMA) hawatoingia mtego huu wa kuzungumza lugha ya vita. Hili waachiwe CCM na mashabiki wake mpaka pale ambapo juhudi zao za kisiasa zitakpokuwa zimeshindwa basi waseme tunaenda vitani na hapo viongozi wa upinzani watolee maoni na msimamo wao. Wapinzani wasizungumze lugha ya vita bali ya amani.
Ndio maana kwa upande wangu ninaangalia sana watu wanaotaka kuwa ma-amiri jeshi wakuu, tusipoweza kuwaangalia wanavyoweza kutumia hekima watu hawa watakuja kutupeleka vitani na tukajikuta tunapigana na tukiulizwa tunapigania nini hatujui kumbe watu walitukaniana mama zao na taifa likaingizwa vitani. Na matumaini yangu JWTZ halitaingia kwenye hili suala la kisiasa na kidiplomasia. Tunataka JWTZ letu litakapozungumza iwe ni baada ya tangazo rasmi la vita nje ya hapo JWTZ iwaache wanasiasa wafanya mambo yao.
Siasa na Diplomasia vikishindwa tujiandae kwa ushindi wa Kivita. Hapo ndio tutoe silaha zetu kibindoni na kuzielekeza kwani tutakuwa tayari kuzitumia.
MMM
No comments:
Post a Comment