Upelelezi wa kesi ya
kutoa matusi kwa Mbunge wa Iramba magharibi, Mwigullu Lameck Nchemba,
inayowakabili vigogo wawili wa Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA)
umekamilika.
Kutokana na kukamilika
huko, kesi hiyo inayovuta hisa ya wakazi wengi wa mkoa huu, itasikilizwa
uchambuzi wa awali Septemba 3 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini
hapa.
Vigogo hao
wanaotuhumiwa kutenda kosa hilo Julai 14 mwaka huu saa 10 ni Afisa Sera na
Utafiti wa CHADEMA makoa makuu, Mwita Waitara Mwikwabe (37) na mshauri wa
CHADEMA na mhadhiri wa chuo kikuu Dar-es-salaam, Dk Kitila Mkumbo (41).
Wakili wa kujitegemea
wa mjini hapa anayewatetea washitakiwa hao, Raymond Kimu, aliiomba mahakama hiyo
ipange kesi hiyo kusikiliza uchambuzi wa awali Septemba 3 mwaka huu, kwa vile
mshitakiwa Dk Kitila atakuwa na mikutano muhimu kati ya sasa na Septemba 1
mwaka huu.
Hakimu anayesikiliza
kesi hiyo, Ruth Massamu alikubaliana na ombi hilo.
Kwa mujiubu wa mwanasheria
wa serikali, Seif Ahmed, washitakiwa walimtukana Mbunge Mwigullu kuwa ni
malaya, mzinzi na mpumbavu huku wakijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na
sheria.
Seif alisema kuwa
washitakiwa walitenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
kijiji cha Nguvumali.
Katika hatua nyingine,
vijana nane wakazi wa kijiji cha Nguvumali ya Ndago jimbo la Iramba Magharibi
wanaotuhumiwa kumuuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (CCM) kata ya Ndago, Yohana
Mpinga (30), kesi yao imeahirishwa hadi Agosti 13, mwaka huu.
Washitakiwa hao ni
Manase Daudi (40), Williamu Elia (33), Frank Stanley (20), Charles Leonard
(36), Tito Nintwa na Fillipo Edward (30).Mwanasheria wa serikali mwandamizi,
Neema Mwanda, alidai mbele ya hakimu Massamu kuwa mnamo Julai 14 saa kumi
alasiri katika kijiji cha Nguvumali, washitakiwa wote kwa pamoja walimpiga kwa
kutumia fimbo na mawe mwenyekiti huyo kusababisha kifo chake.
Vile vile jumla ya
washitakiwa 12 wanaotuhumiwa kufanya vurugu katika mkutano huo wa hadhara wa
CHADEMA katika kijiji cha Nguvumali na kusababisha kuvunjika kwa amani na
utulivu kesi yao imeahirishwa hadi Agosti 13 mwaka huu itakapotajwa tena.
Ilidaiwa kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Chanzo Audiface Jackson
No comments:
Post a Comment