Sunday, August 19, 2012

Slaa: CCM ni mawe


ASEMA WANAIBA HATA FEDHA ZA UKIMWI
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa ameifananisha mioyo ya viongozi na watendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawe yasiyosikia, kuhisi wala kuona jambo lolote, liwe zuri au baya.
Alisema mioyo yao ni sawa na mawe, ndiyo maana wanadiriki kuiba fedha zinazotengwa kupambana na ugonjwa wa ukimwi ilhali waathirika wakiendelea kutaabika kwa kukosa huduma bora ya afya.
Kauli hiyo aliitoa juzi alipokuwa akihutubia katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Msowero na Dumila, ikiwa ni sehemu ya mikutano ya Operesheni Sangara - M4C inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro.
“Kwenye Serikali ya CCM hakuna viongozi wenye mioyo yenye nyama, wote mioyo yao ni ya jiwe kwa kuwa wanaiba hata fedha zinazotengwa kwa ajili ya kupambana na ukimwi,” alisema.
Alibainisha kuwa, vitendo vya ubadhirifu na wizi wa rasilimali za umma ndivyo vinavyowafanya wananchi wengi waendelee kuwa masikini, huku vigogo wachache na familia zao wakiishi maisha ya anasa kila kukicha.
Alisema Watanzania wanahitaji kufanya uchambuzi wa kina juu ya mapato yanayopatikana, yanavyotumiwa na kiasi kilichobaki badala ya kusikiliza kauli za serikali kuwa, imefanya mambo makubwa kwenye maendeleo.
Dk. Slaa alieleza kusikitishwa na kushamiri kwa ubadhirifu na wizi wa fedha za umma kwenye idara, taasisi na halmashauri mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuna uwezekano mkubwa wa kuganda kwa akili za wafanyakazi wa Halmashauri ya Gairo iliyopo mkoani Morogoro, ambao kila kukicha kosa la wizi na ubadhirifu wa fedha za walalahoi linajirudia pasipo watendaji wa ofisi hiyo kuchukua hatua.
“Hivi kwanini tusione kama akili za watendaji hawa zimeganda kwa maana nilipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za serikali za Mitaa tulibainisha uwepo wa upotevu wa zaidi ya sh bilioni moja katika Halmashauri ya Kilosa, hakuna hatua iliyochukuliwa,” alisema.
Maendeleo ya taifa
Dk. Slaa alisema Watanzania wana haki ya kudai chenji yao kwa watawala na wasifungwe na madai kuwa kuna mambo mengi ya maendeleo yaliyofanyika katika miaka 50 ya uhuru.
Alisema ni ujinga kwa serikali kujinasibu kuwa imefanya maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru kwa sababu rasilimali zilizopo hapa nchini hazilingani na kile kilichofanywa.
Alibainisha kuwa, mkwamo wa maendeleo unatokana na kushamiri kwa ufisadi kuanzia ngazi za chini, hivyo serikali haipaswi kujinasibu kuwa imejenga kilometa 11,000 za lami.
“Ugomvi wangu mkubwa na viongozi wa serikali, CCM ni maendeleo tuliyonayo hayalingani na rasilimali zetu. Wao wanasema sisi ni wapotoshaji na vipofu, hakuna anayepinga kwamba hakuna kilichofanyika kwa miaka 50 hii ya uhuru, bali tunahoji kama inalingana na kiasi kinachoingia serikalini,” alisema.
Alisema watu wanapohoji chenji serikalini wanakuwa wameshafanya uchambuzi na kulinganisha utajiri wa rasilimali zilizopo, kodi zinazokusanywa kila siku, madini mbuga za wanyama na vinginevyo.
Amwaga chozi
Dk. Slaa alidondosha machozi mbele ya hadhara alipokuwa akizungumzia madhila yanayowapata wafugaji kwa kugeuzwa chanzo cha fedha na baadhi ya askari wasiokuwa waaminifu.
Kiongozi huyo alifikia hatua hiyo baada ya kuanza kueleza namna mmoja wa viongozi wa wafugaji wilayani Kilosa alivyomfuata na kumweleza kuwa askari wa Jeshi la Polisi, mgambo na viongozi wa serikali za vijiji wanavyowanyanyasa na kuwadhalilisha wafugaji.
“Nikiwa Kilosa mjini juzi, nilifuatwa na kiongozi wa wafugaji akaniambia baada ya kukamatwa, wake zao au mabinti zao hufanyiwa vitendo vya udhalilishaji mbele ya macho yao, lengo likiwa ni kuwafanya wawakomboe kwa haraka katika mateso hayo, hii inasikitisha kuona Tanzania imefikia hapa,” alisema.
Huku akifuta machozi, Dk. Slaa alisema inasikitisha kuona watu waliopewa dhamana ya kuongoza ndio walio mstari wa mbele kuwanyanyasa na kuwatesa wananchi.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment