Thursday, August 30, 2012

Sitta: Tishio Chadema ni Dk Slaa tu

ADAI WENGINE NI WAZOEFU WA KUONGOZA KUMBI ZA MUZIKI, ATAMBA CCM KINA ZAIDI YA WATU 20 WENYE SIFA ZA URAIS, ZITTO AMJIBU
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM, Samuel Sitta amekiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akidai kuwa muda wake wa kutawala nchi bado, kwa kuwa hakina viongozi wa kutosha wa kufanya kazi za Serikali ukimwondoa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.

Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Karagwe, Kagera, alikokuwa katika ziara ya kutembelea ofisi za CCM.

Alisema kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi wa chama hicho, kutokana na kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake akidai kuwa kina baadhi ya viongozi wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki... “Wote hapa mnasikia kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.”

Dk Slaa na Mbowe hawakupatikana jana kuzungumzia kauli hiyo ya Sitta baada ya taarifa kueleza kuwa Mbowe yuko nje ya nchi na alikuwa hapatikani kupitia simu yake ya mkononi kama ilivyokuwa kwa Dk Slaa.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alipinga kauli hiyo akimtaka Sitta aachane na chama hicho kikuu cha upinzani na atumie muda wake kukijenga chama chake ambacho alidai kuwa kina makundi zaidi ya sita.
“Mwaka 2005 tuliweka mgombea Mbowe, mwaka 2010 tukamweka Dk Slaa, mwaka 2015 anaweza akarudi Mbowe, Dk Slaa au mwanachama yeyote wa Chadema,” alisema Zitto.

Alisema Chadema ni taasisi na si chama cha makundi kama ilivyo kwa CCM hivyo hakiwezi kumtegemea mtu mmoja... “Sitta asigombane na Chadema, ajenge chama chake ili tukutane mwaka 2015.”

Akizungumza na viongozi hao wa CCM Karagwe, Sitta alisema hakuna kiongozi mwingine anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza Chadema na kukifanya chama kikubalike kwa umma.

“Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye sifa zinazofanana tofauti na wao wanaye Dk Slaa tu ambaye inasemekana aliukimbia upadri.”

Kuhusu CCM
Akizungumzia chama chake, Sitta aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kutokaa kimya na badala yake wajitoe na kujibu hoja za upinzani wanazozitoa kuikosoa Serikali iliyopo madarakani ili ionekane haijafanya mambo ya maendeleo tangu kupatikana kwa uhuru.

“Serikali ya CCM imefanikiwa katika maeneo mengi ya huduma za jamii kama elimu, barabara, afya na mawasiliano, sasa inashangaza kuona viongozi wa chama mnashindwa kufanya mikutano ya kuwaeleza wananchi mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera na ilani ya chama chetu.”

Sitta aliwataka viongozi chama hicho nchini kuepuka mapambano na chuki miongoni mwao lakini akasisitiza kwamba kinaendelea na mkakati wake wa kuwaondoa viongozi wanaodaiwa kuwa ni mafisadi maarufu kwa jina la “magamba”.
Alisema chuki na mapambano yanayoendelea ndani ya chama hicho ndiyo yanayochangia kukidhoofisha na kuwapa la kusema wapinzani na hata kusababisha baadhi ya wanachama kukihama.

“Mapambano ndani ya CCM ndiyo chanzo cha migogoro na mitafaruku inayosababisha viongozi na wanachama wetu kuombeana mambo mabaya na kutoa mwanya kwa watu wetu kuhamia upinzani.”
Sitta yupo katika ziara ya siku tano ya kiserikali mkoani Kagera kukagua miradi mbalimbali inayohusiana na mwingiliano wa uchumi na kijamii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

No comments:

Post a Comment