Mh Rais , nakusalimu .
Mh Rais na huu ni ushauri wangu kwako kama Mkuu wa Nchi na mtazamo wangu juu ya matukio yanayotokana na changamoto katika Sensa ya Taifa hivyo nakunifanya nikuandikie waraka huu.
Mh Rais , Kama Taifa hili kwa miezi michache mbele inayokuja Siasa za Udini , Ukabila na ukanda utaendelea kushabikiwa katika kiwango hiki cha sasa , ukweli ni kwamba siku chache zinazokuja Taifa hili litaanguka na halitasimama tena , Propaganda zilizofanyika huko nyuma dhidi ya vyama vya upinzani mbali mbali zilifikiriwa kuwa lengo lake lilikuwa ni kuviangamiza vyama hivyo tu na huku Watawala wakibaki salama, lakini leo tunaanza kuona lugha za Udini zikitawala katika Taifa letu kila siku na ule mpango wa kuangamiza Vyama hivyo umekwenda mbali zaidi na sasa unakaribia kuangamiza Taifa.
Mh Rais Nchi hii haiko salama hata kidogo na pengine wahusika wanaopaswa kulinda usalama wa Nchi wanakupa ripoti za hofu na woga na hivyo unashindwa kupata taarifa kamili ya ukweli wa mambo yanavyoendelea katika Taifa letu, ukitazama suala la Sensa na changamoto zake kwa sasa utagundua kwamba sio faida hata kidogo kulazimisha jambo hili kwa kutumia nguvu kwani sio sahihi hata kidogo kujua tu idadi ya watu bila kuzingatia hofu ya watu hao na mashaka ambayo yamejengeka katika Imani .
Mh Rais , Siasa chafu ambazo zimekuwa zikitafuta Madaraka bila kuangalia siku njema za baadae za Nchi ndio chanzo cha kinachotokea sasa , tulipokuwa Igunga Chadema ilifanyiwa propaganda za Udini sana na kwa bahati mbaya waliofanya hivyo walishinda uchaguzi na huku Watu wale waliofanya hivyo waliamini na kufikiri Siasa hizo za kibaguzi zitaishia Igunga tu na bila kutambua Dini ni Imani na lazima kutaendelea kuwepo na mpasuko mkubwa hata baada ya Uchaguzi .
Mh Rais , Uhuru wa kweli sio Mtu kufanya kila anachotaka bali kile anachopaswa tena katika haki na kweli “ Kama lengo la Watawala kubaki madarakani au kuongoza litafanywa kwa nguvu na namna yoyote hile hata kwa kuwagawa Watu kwa dini zao na kabila , basi siku chache zinazokuja Taifa letu halitaweza kutawalika tena na Mamlaka hayo yanayotafutwa hayataweza kuwa na faida kwa kizazi hiki na kizazi kinacho kuja na ukweli ni kwamba kwani kila aina ya ubaguzi wa aina yeyote unaofanyika ama kwa siri au hadharani hautaacha Jamii yetu kuwa salama .
Mh Rais , Chama tawala siku zote wajibu wake katika kujibu hoja za wapinzani ipasavyo ni kutekeleza ahadi zake ambazo walizitoa wakati wa uchaguzi na huu ni wajibu mkuu katika kutawala kwa Chama tawala , lakini Chama kilichoko madarakani kinapoanza kuwagawa watu kwa dini na kabila ili mradi kifanikishe malengo ya kutawala basi ni lazima tutambue kuwa Viongozi wa Chama hicho wamekusudia kabisa kuipeleka Nchi yetu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mh Rais , siku hizi katika forum mbali mbali zinazojadili mambo ya Siasa katika mitandao ya kompyuta hapa Tanzania , kumekuwepo na maoni mbali mbali na mitazamo haswa wakati wowote ule unapofanya uteuzi au kuchagua mtendaji katika Serikali , Mara nyingi , ghafla utaanza kuona watu wananza kuuliza Kabila au Dini ya mtu aliyeteuliwa au kupendekezwa, hii ni hatari kubwa kuwa na Taifa ambalo sifa ya Mtu ya kwanza kwa wachambuzi na wadadisi inajadiliwa kwa Dini au Kabila ya Mtu fulani , kwani hatuwezi kuongozwa kwa mlinganisho wa Kabila au Dini ili kupata utawala bora . Tabia hii wakati mwingine inapelekea kutafuta viongozi mbali mbali kutoka kila pembe ya Nchi ili kupata mlinganisho wa Ukanda na Kimkoa na hivyo kusababisha kuishia kupata viongozi pengine Viongozi wasiokuwa na uwezo kwa sababu ya kutafuta mlinganisho katika kupanga safu ya uongozi na utawala . Na kwa kweli huu nao ni ubaguzi uliojificha unaoendelea katika Taifa letu.
Utawala thabiti mahali popote , Utazingatia , Uwezo , Sifa , Maarifa ,Uadilifu na Hekima ili Mtu kuchaguliwa kuongoza . Dini na kabila lake sio jambo muhimu hata kidogo katika uongozi, hivi ikitokea katika uchaguzi Dini moja tu na kabila moja ndio likahusika katika uchaguzi wakati wa mchakato wa kutafuta viongozi , je Serikali itaahairisha Uchaguzi kwa sababu watu wengine wa Dini na Kabila nyingine hawakuona umuhimu wa kushiriki Uchaguzi ? ni swali ambalo linaweza kuonekana halina msingi lakini kwa wanaona mbali watajua ni nini namaanisha ? hata hivyo tunakoelekea sasa tusipokuwa makini , tutanza kupokezana Madaraka na Utawala kwa kuangilia Udini na sio Uwezo na Uadilifu na tukifika hapo Taifa hili halitasimama tena .
Mh Rais ni wajibu wako sasa kusaidia Taifa hili kwa Mamlaka uliyonayo ni Imani yangu hata wewe umekwishaona hili na ni matumaini yangu kuwa unalifanyia kazi . Mfano wa wazi ni pale Katibu Mkuu wa CCM Bwana Mkama , alipotaka kuleta Siasa za Kibaguzi katika Msiba wa Marehemu Bob Makani pale Karimjee wakati akitoa salamu za rambi rambi ambapo wewe mwenyewe ulikuwepo kama Kiongozi Mkuu wa Taifa na ulishuhudia upotoshaji wake huo ambao ulionekana kama lengo ilikuwa kuidhoofisha Chadema huku hakisahau kuwa dhambi ya ubaguzi aina mipaka.
Mh Rais , Martin Niemoller , alisema maneno yafuatayo yalipomkuta “ When Hitler attacked the Jews I was not a Jew, therefore I was not concerned. And when Hitler attacked the Catholics, I was not a Catholic, and therefore, I was not concerned. And when Hitler attacked the unions and the industrialists, I was not a member of the unions and I was not concerned. Then Hitler attacked me and the Protestant church -- and there was nobody left to be concerned”
Mh Rais , Tatizo ni kubwa na ni vyema likashughulikiwa kwa nguvu zote sasa na kwa hekima , hata hivyo nafikiri waraka huu hautakukwaza kwani ni ukweli wangu juu ya hali halisi inayoendelea kujitokeza katika Nchi yetu na Mimi nikasema nisikae kimya ni bora niseme , Taifa linakwenda mahali pabaya kama dhambi ya ubaguzi isipodhibitiwa .
Nakutakia Kazi Njema .
“ Only Time Will Tell “
Godbless Jonathan Lema
26/8/2012
No comments:
Post a Comment