Thursday, August 30, 2012

Madiwani waliotimuliwa CHADEMA wabanwa


WAKILI wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Method Kimomogoro, ameiomba mahakama kuwapeleka magereza waliokuwa madiwani watano wa chama hicho jijini Arusha endapo mpaka Septemba 3, mwaka huu, watashindwa kuwasilisha mahakamani hapo utaratibu wa namna ya kulipa gharama zilizotumika kuendesha shauri lao lililotupwa na mahakama ya mkoa.
Kimomogoro ambaye pia anamtetea Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe katika kesi hiyo ya madiwani hao kupinga kuvuliwa uanachama, alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Charles Magesa, anayesikiliza shauri hilo la kudai gharama linalowakabili John Bayo, Reuben Ngowi, Charles Mpanda, Rehema Mohamed na Estomii Mallah ambao wanatetewa na wakili, Severine Lawena.
Alisema kuwa amefikia kutoa ombi hilo baada ya kuona shauri hilo limeahirishwa zaidi ya mara nne mfululizo, huku madiwani hao wakishindwa kuieleza mahakama namna watakavyowalipa gharama zao walizotumia kwenye shauri la madai kiasi cha sh milioni 15.1 kama ilivyoamriwa na mahakama.
Aliongeza kuwa, wateja wake wamemweleza kuwa wako tayari kulipia gharama za madiwani hao waliotimuliwa CHADEMA kukaa jela mpaka hapo watakapoamua kulipa deni hilo ambapo kwa mujibu wa sheria wanaweza kukaa huko kwa kipindi kisichozidi miezi sita.
Agosti 10 mwaka jana mahakama ya hakimu mkazi mkoa iliyokaa chini ya hakimu Hawa Mguruta, ilitupilia mbali shauri la madai lililofunguliwa na madiwani hao dhidi ya Mbowe na CHADEMA baada ya kubaini kuwa kulikuwa na mapungufu ya kisheria.
Madiwani watano walikuwa wakipinga kuvuliwa uanachama wa CHADEMA, baada ya kufikia muafaka wa uchaguzi wa umeya wa Jiji la Arusha bila kupata baraka za chama.
Hakimu Mguruta wakati akisoma hukumu yake hiyo, alisema kuwa mahakama haiwezi kuingilia maamuzi ya CHADEMA kwa kuwa ni chama kilichosajiliwa kisheria kama chama cha siasa, hivyo maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu (CC) kwa kufuata katiba yake ni sahihi.
Pia, Mguruta aliwataka madiwani hao kulipa fidia ya gharama ya kesi hiyo kwa CHADEMA na Mbowe.
Hakimu huyo alisema kuwa mahakama yake inakubaliana na pingamizi zote tano zilizotolewa na wakili wa utetezi, ambazo ni kukataa CHADEMA kushtakiwa kwa jina lake, Mbowe kushtakiwa binafsi, mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kutengua maamuzi ya chama isipokuwa Mahakama Kuu.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment