Wednesday, August 22, 2012

Dk. Slaa, Nape hapatoshi


KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amemshambulia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa kwamba anazeeka vibaya kutokana na madai yake kwamba CCM imeingiza silaha za moto nchini.
Wakati Nape akitoa kauli hiyo, Dk. Slaa amezidi kuikalia kooni CCM akisema katika hili hawatoki na kuahidi kuanika ushahidi wa tuhuma hizo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara huko Mlali, Langali na Mvomero mjini Morogoro, Dk. Slaa alisema wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga, CCM iliweka vijana wao kwenye kambi ya Ilemo, Iramba na Singida mjini na kuwapatia bunduki iliyotengenezwa China yenye uwezo wa kubeba risasi nane kwenye magazine namba j137.
“Rais Kikwete atuambie, kama Amiri Jeshi Mkuu, silaha hii iliingiaje na kwanini ilikuwa mkononi mwa CCM. Wakiendelea kuropoka nitawamaliza maana katika hili hawatoki,” alisema Dk. Slaa.
Akijibu mapigo ya tuhuma hizo, Nape aliwaeleza waandishi wa habari aliowaita kwenye ofisi ndogo za chama hicho Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam jana kwamba tuhuma za chama chake kuingiza silaha zilizotolewa na Dk. Slaa ni za kijinga.
Nape alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kumhoji Dk. Slaa na kupata ushahidi wake.
Nape alimshambulia Dk. Slaa akidai ameshindwa kukiongoza chama chake kwa sababu uwezo wake wa kufikiri ni mdogo.

“Huu ni uongo uliopitiliza, nadhani huyo anayejiita Dk. Slaa anazeeka vibaya, kama siasa zimemshinda awaachie vijana… kwa taarifa yake hakuna kambi yeyote ya vijana kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi wa chama.
“CCM ilidai uhuru bila silaha, haya madai ya kuingiza silaha ni ya kijinga sana kutolewa na mtu mzima kama yeye, hasa anapoona mambo magumu anatafuta namna ya kutoka.
“Mtakumbuka mwaka 2010 alisema tumeingiza masanduku ya kura wakati anajua anashindwa… katika hili tutamtaka huyo Dk. Slaa awaombe radhi Watanzania,” alisema Nape aliyekiri kwamba chama chake kina utaratibu wa kuweka kambi za vijana.
Nape alisema CHADEMA wamepanga kufanya vurugu siku ya mkutano wake wa mwisho mjini Morogoro na wamegundua kuwepo kwa magari matano yenye vijana wa chama hicho walioandaliwa kwa ajili ya vurugu hizo.
“Tunajua wanazo Coaster (magari) tano zenye vijana walioandaliwa kwa ajili ya vurugu wanazunguka nazo, tena zimeonekana zikielekea Bagamoyo, tunawafuatilia,” alisema Nape na kueleza kwamba wameshatoa taarifa polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema hajapokea taarifa zozote kutoka kwa viongozi wa CCM kuhusu vurugu zilizopangwa na wafuasi wa CHADEMA.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment