Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, aache kuhoji fedha ambazo chama hicho kinachangiwa na wananchi kwa kuwa chama chake (CCM) kilingizwa madarakani kwa fedha chafu.
Nape alisema Jumapili iliyopita kuwa Chadema kinawachangisha wananchi fedha huku kikipokea fedha kutoka kwa wafadhili wa nje na kukitaka kiwaeleze wanananchi fedha hizo zinatoka wapi.
Majibu hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, na kusisitiza kuwa Nape na chama chake waliwekwa madarakani mwaka 2005 kwa fedha alizosema ni chafu.
Dk. Slaa alisema Nape hana uhalali wa kufikiria kuwa kuna vyama vina takatisha fedha chafu kwa kupitia michango ya wananchi na badala yake
anapaswa kuwaambia wana-CCM wenzake namna Chama hicho kilivyotumia fedha chafu kuingia madarakani mwaka 2005.
Dk. Slaa aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kilosa Town mjini Kilosa na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
“Nimemsikia Nape akiendeleza madudu yaliyo kichwani mwake kuwa alikuwa anatoa tahadhari tu sasa ninamwambia yule si saizi ya Chadema na Dk. Slaa,” alisema na kuongeza: “Zaidi ninamkumbusha kuwa fedha za Tangold, Kagoda na Meremeta ndizo zilizoiingiza chama chake madarakani hivyo awape tahadhari hao badala ya wananchi wanaokichangaia Chadema kwa mioyo yao ya kutaka kujikomboa.”
Dk. Slaa alisema kuwa wameshamwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amtake Nape na CCM wathibitishe namna Chadema kinavyopata fedha chafu na kama ikishindikana basi Jeshi la Polisi limchukulie hatua kwa kuwa ni kauli za uchochezi na chuki dhidi ya Watanzania.
Aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, na timu yake wameshindwa kuchukua hatua za awali wakati kuna mtu ana ushahidi wa kuthibitisha namna fedha chafu zinavyoingia nchini.
“Sitaki kuamini kama IGP ana maslahi katika hili, lakini pia sisiti kuamini kuwa hii si kauli ya Nape ni ya kiongozi wake mkuu katika Chama…. sasa kwa hili wanazidi kutudhihirishia kuwa nchi imewashinda kwa kuwa kuna vyombo vya usalama vinavyoongozwa na serikali ya CCM vimeshindwa kuchukua hatua na kuudhihirishia umma ukweli unaosemwa na
Nape,” alisema Dk. Slaa.
Nipashe
No comments:
Post a Comment