Saturday, August 25, 2012

Dk. Slaa awaangukia walimu


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amewasihi walimu nchi kutomaliza hasira zao za kutolipwa vizuri kwa kutowapa elimu bora wanafunzi wao.
Dk. Slaa alisema adui mkubwa wa walimu ni Rais Jakaya Kikwete, CCM na serikali yao ambao mara kwa mara wamekuwa wakiongeza mishahara, marupurupu na posho kwa wabunge lakini hawawajali walimu.
Kauli hiyo aliitoa juzi kwenye mikutano ya hadhara kwenye vijiji na kata mbalimbali za Jimbo la Morogoro Kusini, akiwataka wafanyakazi wasihamishie hasira zao kwa wananchi na badala yake hasira hizo wazielekeze kwenye serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
“Juzi nimesoma kwenye mtandao, naona walimu wanatumiana meseji, ujumbe mfupi kwenye simu zao na kama kweli wataufanyia kazi, maskini watoto wetu hawa walioko shuleni na taifa lote tumekwisha,” alisema.
Alisema ujumbe huo unaowaelekeza walimu kuwafundisha uongo wanafunzi, jambo ambalo linatoa ishara kuwa wana kinyongo na serikali inayopuuza madai ya nyongeza za mishahara, posho na stahiki nyinginezo.
“Chonde chonde walimu wangu naombeni hasira zenu msizihamishie kwa watoto wangu hawa wasiokuwa na kosa lolote, kila mtu mwenye akili timamu anatambua madai yenu ni ya ni ya msingi, mnapaswa mjue adui yenu ni Kikwete na serikali yake.
“Ikabeni koo hiyo serikali lakini timizeni wajibu wenu kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora,” alisema.
Alisema kitendo cha serikali kuongeza mishahara ya wabunge na kufikia milioni 11 huku ikishindwa kutatua madai ya msingi ya kada nyingine kinaonesha inavyowatumia wananchi wake kama makarai ya ujenzi.
Dk. Slaa alisema kada nyingine za utumishi wa umma wakiwamo askari na madaktari zinafanya kazi katika mazingira magumu na wanadharauliwa na serikali licha ya kuwa na mchango mkubwa kwa taifa.
alibainisha kuwa serikali inavyoendelea kuidhinisha marupurupu na mishahara ya wabunge huku ikiendelea kukandamiza masilahi ya makundi mengine ndiyo chanzo kikubwa cha wananchi kupunguza ari ya kujiletea maendeleo.
Katibu Morogoro ajiuzulu
Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda, amejiuzulu nafasi yake na kuahidi kuhamia CCM ndani ya saa 48 zijazo. Luanda alisema Agosti 21 mwaka huu alimkabidhi barua ya kujiuzulu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, yenye kumbukumbu namba AEL/KCDM/KINK/MC/O12.
Katika barua yake hiyo Luanda alitaja sababu zilizomfanya avue ‘gwanda’ kuwa ni kupisha upepo mbaya wa kisiasa ndani ya CHADEMA kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa, kukosa ushirikiano na Mwenyekiti wa CHADEMA wa Mkoa pamoja na kile alichokiita dharau kutoka kwa viongozi wa chama hicho taifa.
Sababu nyingine ni kupisha alichokiita agenda ya siri aliyodai imejificha katika mchakato mzima wa ziara ya CHADEMA mkoani humo kuwa inalenga kuwaondoa viongozi ndani ya wilaya na mkoa wanaodaiwa kukubalika kwa wananchi.
Wakati Luanda akieleza sababu hizo, taarifa za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata zinaeleza kuwa katibu huyo alishindwa kusimamia chama mkoani humo, hali iliyomlazimisha Dk. Slaa kusimamia chaguzi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha chama.
Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, amethibitisha chama kupokea barua ya kujiuzulu kwa Luanda na kueleza kuwa kilichomfanya ajiuzulu ni hofu ya kujulikana kuwa alikuwa hakijengi chama katika mkoa, hasa katika Wilaya yake ya Morogoro Vijijini.
“Huyu bwana mbali ya kuwa katibu wa mkoa pia alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Wilaya ya Morogoro Vijijini, yenye majimbo mawili, kwa sababu ya kushindwa kazi na wajibu wake amesababisha majimbo yote mawili hayana akaunti benki kwa muda wote ambao amekaa madarakani, hivyo yameshindwa kupata mgawo wa ruzuku kutoka makao makuu kama inavyotakiwa,” alisema.
Makene alieleza kuwa hata taarifa ya ukaguzi iliyokuwa ikifanywa na timu ya chama hicho mkoani Morogoro imeshindwa kupata taarifa muhimu kutokana na katibu huyo kushindwa kujua majukumu yake.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment